Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Chato, Lucas Michael, maarufu Masai kupanda jukwaani na kuzungumza kwenye mkutano wa kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa na kuilalamikia serikali kushindwa kuwarejesha makwao walimu waliostaafu, kulipa madai ya walimu, pamoja na kutopandisha madaraja kwa wakati, serikali imemshitaki.
Katika madai yake, Michael pia alidai kusikitishwa na kitendo cha
serikali ya wilaya ya Chato kuwaandama baadhi ya walimu wanaoonekana
kuunga mkono vyama vya upinzani, huku wanaokiunga mkono CCM wakionekana
wako sahihi, kitendo alichodai ni ukandamizwaji wa demokrasia.
Mwenyekiti huyo wa CWT alihudhuria mkutano wa kampeni za mgombea
huyo wa urais alipofika wilayani Chato Septemba 19, mwaka huu, baada ya
kupokea mwaliko wa Chadema wilayani humo akiwa kama mdau wa elimu.
Kufuatia hatua hiyo, mwenyekiti huyo wa CWT wilaya ya Chato
ameshitakiwa kwenye Tume ya Utumishi wa Umma Idara ya Utumishi wa Walimu
wilayani hapa, kwa madai ya kukiuka maadili na taratibu za utumishi,
kanuni namba 65 (1) na kutakiwa kujieleza.
Hati ya shitaka ambayo imesainiwa na Kaimu Katibu wa Tume ya
Utumishi wa Umma, Frank Angus, Septemba 22, mwaka huu, inadai kuwa
mwalimu huyo alitenda kosa la kujihusisha na masuala ya kisiasa,
kuchukua taarifa za kiutumishi na kuzisema kwenye mkutano wa kisiasa
pamoja na kutumia nafasi yake akiwa mtumishi wa Umma kumnadi mgombea
urais wakati wa kampeni.
Akizungumza na mwandishi jana, Michael alithibitisha
kupokea hati ya shitaka hilo. Hata hivyo, alisema hakuhusika kufanya
kampeni za mgombea urais kupitia Chadema isipokuwa alisimama kuzungumzia
malalamiko ya walimu wa wilaya ya Chato.
Alidai alialikwa kuhudhuria mkutano huo wa kampeni kupitia barua ya
Chadema yenye kumbu kumbu namba Chadema /CHT/G/M/1/015 na ana amini
alitimiza wajibu wake kwa mujibu wa katiba ya CWT.
Naye Katibu wa Chadema Wilaya ya Chato, Mange Ludomya, alisema
mwalimu huyo alialikwa kwenye mkutano huo kama mwenyekiti wa CWT ambacho
ni wadau wa elimu nchini kutokana na umuhimu wake, ikizingatiwa kwamba
kipaumbele cha chama hicho iwapo kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi ni
elimu.
Post a Comment