Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limekanusha taarifa zinazodaiwa kuandikwa katika mtandao mmoja wa kijamii, zikidai kukamatwa kwa baadhi ya watu katika kituo cha polisi wilaya ya Masasi mkoani hapa wakiwa na masanduku na fomu za kupigia kura zipatazo 2000 zikiwa tayari zimetumika.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mtwara, Henry Mwaibambe, alisema taarifa hizo zilidai kuwa, fomu hizo
zilimpa alama ya vema mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Dk. John Magufuli na mgombea ubunge wa jimbo la Masasi kupitia chama
hicho.
Alisema
taarifa hiyo iliendelea kudai kuwa, mkuu wa wilaya ya Masasi aliingilia
kati na watuhumiwa hao ambao hawakutajwa majina waliachiwa huru kwa
dhamana kwa amri ya mkuu huyo wa wilaya ambaye ndiye aliewadhamini na
kwamba masanduku hayo na karatasi yamehifadhiwa katika kituo cha polisi
wilayani humo.
Kamanda
Mwaibambe alisema taarifa hiyo ni uzushi na upotoshaji mkubwa na kwamba
hakuna mtuhumiwa wala masanduku yaliyokamatwa mkoani hapa wala katika
wilaya hiyo.
“Tunachofahamu
kupitia kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (Nec), vifaa vya kupigia
kura bado havijawasili nchini na alituahidi vitaanza kuwasili mwishoni
mwa mwezi huu kutoka nchini Afrika Kusini.” alisema.
Alisema Jeshi la Polisi linamsaka mhalifu huyo wa mtandaoni na akitiwa mbaroni atafikishwa katika vyombo vya sheria.
Post a Comment