Nicodemus Jonas na Khadja Mngwai
Simba
imechunguza tabia na nidhamu ya wachezaji wa Kibongo na kubaini kuwa
wengi wao hufanya mazoezi kwa sababu tu ni sheria na siyo kwa utashi wa
mioyo yao, hivyo imeamua kuja na mkakati wa kuhakikisha kila mmoja
anaitumikia timu kwa moyo mkunjufu.
Uongozi
wa Simba umeanzisha mfumo wa kuwakata mishahara wachezaji wote
watakaoshindwa kufanya mazoezi pasipo sababu ya msingi wala kutoa
taarifa sehemu husika, jambo ambalo linamaanisha inataka kila mmoja kili
yake iwepo kwa ajili ya kuisaidia timu.
Ni
wazi kuwa Simba bado inajijenga baada ya kupotea kimataifa katika
misimu mitatu mfululizo, hivyo inahitaji kuwa na wachezaji wenye ari ya
ushindi kwa timu nzima na wenye nidhamu ya kufanya mazoezi.
Mratibu
wa klabu hiyo, Abass Suleiman Ally, Ijumaa aliwaweka kikaoni nyota wote
na kuwaeleza utaratibu huo na kuwataka kila mmoja anapokuwa na udhuru
ni lazima atoe taarifa sehemu husika na kwamba siyo jukumu la kiongozi
kumuuliza mchezaji kwa nini hajafika mazoezini, vinginevyo wasilaumiane
mwisho wa mwezi wakikuta akaunti zao zinapungukiwa.
“Nilitaka
kuwaweka wazi, kila mchezaji atambue kuwa asipokuja mazoezini, hakuna
tena kiongozi kuanza kumtafuta mchezaji kumuuliza sababu za kutofika,
badala yake mchezaji ndiye atoe taarifa kama atakuwa na udhuru.
Tumepanga
yeyote ambaye atakosa mazoezi pasipo taarifa sehemu husika, wajibu
wangu ni kurekodi watoro na mwisho wa mwezi tusije kulaumiana akikuta
amekatwa mshahara,” alisema Ally bila kufafanua watakuwa wakikata
asilimia ngapi kila mchezaji anapokosa mazoezi.
Post a Comment