Dar
es Salaam. Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mghwira amemtaka Rais
Mteule Dk John Magufuli kutekeleza utashi wa wananchi kwa kuwapatia
Katiba mpya.
Mwenyekiti
huyo, ambaye ameshika nafasi ya tatu katika mbio za urais wa Jamhuri ya
Muungano, pia amemtaka Dk Magufuli kuhakikisha anadumisha umoja wa
kitaifa na kuondoa umasikini, huku akimkabidhi ilani ya chama hicho ili
aitumie katika kipindi chake cha uongozi.
Mghwira
alisema hayo saa chache baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
kumkabidhi Dk Magufuli cheti cha kumtambua kuwa mshindi wa mbio za urais
kwenye hafla fupi iliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es
salaam.
Mgombea
huyo ni mwanamke pekee aliyejitosa kuwania nafasi ya urais katika
uchaguzi wa mwaka huu, alimtaka Dk Magufuli kuanza na jambo lililokuwa
likizungumzwa mara nyingi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu ambalo ni
mabadiliko.
Alisema
miongoni mwa mambo yanayohitaji mabadiliko ya haraka katika uongozi
wake ni kuwapatia wananchi katiba mpya, kudumisha umoja wa kitaifa na
kuwaondolea wananchi umasikini kwa sababu Tanzania ina utajiri mkubwa.
Mghwira,
ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa, alipewa nafasi hiyo ya
kuzungumza kwa niaba ya wagombea urais wa mwaka huu. Wagombea
waliohudhuria kwenye hafla hiyo walikuwa watano baada ya mgombea wa
Chadema, Edward Lowassa, aliyeshika nafasi ya pili, Hashim Rungwe
(Chaumma) na Macmillan Lyimbo wa TLP, kutofika.
Awali
kabla ya hafla hiyo, Mghwira aliliambia gazeti hili kuwa Tanzania ni
tajiri lakini Watanzania wenye nchi yao wamebaki kuwa masikini, hivyo
wananchi wamemchagua Dk Magufuli kwa sababu wana imani naye na hivyo
anatakiwa kuhakikisha hawaendelei kuwa masikini, haki fikra.
“Umasikini
walio nao Watanzania ni wa uongozi bora, nimekubali na nina imani
Watanzania walio wengi wamekubali kuwa Dk Magufuli ndiyo Rais wa Awamu
ya Tano,” alisema.
Wagombea
wengine waliozungumza na Mwananchi walisisitiza kuwapo na amani,
utulivu, kutatua kero tatu za wananchi ambazo zipo tangu nchi ipate
uhuru ambazo ni ujinga, maradhi na umasikini.
Chifu
Lutalosa Yemba, aliyewania urais kupitia ADC, alisema kuwa wakati
wanaingia kwenye kinyang’anyiro hicho, alikuwa na lengo la kuondoa
maadui hao watatu waliodumu kwa miaka mingi nchini. Hivyo Rais wa Awamu
ya Tano ahakikishe anapambana na matatizo hayo.
Kuhusu
kuwa nje ya Ukawa , Yemba alisema hakuingia huko kwa sababu hakuona
kama atakuwa salama kwa sababu hakukuwa na msingi wa umoja huo, ingawa
alisema hana tatizo na uwepo wake na hadhani kuwa vyama vilivyokuwa nje
ya umoja huo vimesababisha wapinzani wasichukue nchi.
Alisema kutokana na uzoefu wake wa kugombea ubunge na urais, uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa huru na wa haki.
Alisema
hapo awali, hata kampeni zilikuwa na vitisho, ilikuwa ngumu kumtaja
kiongozi mwingine jukwaani kwa kuhofia vitisho, lakini mwaka huu kila
mgombea alikuwa huru kuzungumza, kuhoji anapoona hapajakaa sawa.
Lyimo,
aliyegombea kwa tiketi ya TLP, alisema uchaguzi haukuwa huru na haki
kwa sababu kuna dosari na kasoro nyingi huku wananchi wakilazimishwa
kukubali na kuamini wanachotaka watu wachache.
Alisema kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar ni moja tu ya dosari nyingi zilizofumbiwa macho na matakwa ya watawala.
“Nimekubali
matokeo na kushindwa kwa sababu ya kutetea haki za Watanzania walio
wengi ambao hawataki vurugu, wanataka amani itawale. Tangu awali
kulikuwa na harufu ya vurugu, sikutaka niwe chanzo cha vurugu hizo,”
alisema Lyimo.
Janken
Kasambala, aliyewania kiti hicho kupitia chama cha NRA, alisema
uchaguzi umekwisha hivyo Watanzania waweke kando mambo ya siasa badala
yake waungane kupambana kujenga nchi.
“Tuachane
na masuala ya siasa, tufanye kazi, tuungane kujenga nchi, tuachane na
tofauti za kisiasa, kwani tulikuwa tunatafuta mshindi mmoja
atakayeiongoza nchi, na sasa amepatikana,” alisema Kasambala.
Fahmi Dovutwa wa UPDP alisema Watanzania warudi kama zamani waendeleze maisha na kuachana na ushabiki kisiasa.
uliokuwepo wakati wa kampeni kwa sababu Rais amepatikana.
Alisema
hata waangalizi wa kimataifa hawana nafasi ya kuingilia masuala ya
kisiasa ya ndani kwa sababu hata kwao huwa wanaharibu, hivyo wananchi,
viongozi wasifanye maamuzi kwa kuwasikiliza wao badala yake waangalie
mustakabali wa nchi na wananchi wake.
Chanzo na mwananchi.
Post a Comment