Ndugu Waandishi wa Habari,
Umoja wa Vijana wa Chama Cha
Mapinduzi unachukua nafasi hii kukipongeza kwa dhati Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na aliyekuwa mgombea wake wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Rais mteule Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na mgombea mwenza
wake Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kupata ushindi wa kidemokrasia wa
kishindo kwa kupata asilimia 58.46%.
Ushindi huo ni alama na kielelezo
cha kuendelea kukubalika kwa CCM mbele ya Watanzania walio wengi
kutokana na Sera zake, Mipango yake na mikakati ya kuwatumikia wananchi,
kulinda amani, utulivu na kuendeleza Umoja wa Kitaifa nchini.
Ndugu waandishi wa habari,
Kwa upande mwingine tumelazimika
kuwaita hapa leo kuelezea masuala muhimu kadhaa yaliyojitokeza katika
Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka 2015.
Kama ilivyotolewa taarifa na
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha, kwamba
Uchaguzi wa Zanzibar kwa sehemu kubwa ulikumbwa na kasoro nyingi za
kimsingi ambazo zimesababisha Tume kufuta matokeo kwa nafasi za Urais,
Wawakilishi na Madiwani.
Ndugu waandishi wa habari,
UVCCM tumefanya tathmini ya haraka
na kina ili kujua kiini cha tatizo hilo ikiwemo kukusanya taarifa toka
vyanzo mbalimbali ambapo tumebaini na kugundua madhaifu kadhaa
yaliyojitokeza katika hatua za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa
upande wa Zanzibar.
Tumepata wasiwasi wa suala zima la
namna zabuni ya karatasi za kupigia kura ilivyotangazwa na kumpata
mzabuni ambae alipewa kazi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
Ni ukweli usiopingika kwamba ZEC
ilizidiwa nguvu na wanasiasa wa Chama cha Upinzani cha CUF ambao kwa
kiasi fulani wameshinikiza Tume ya Uchaguzi kwa namna moja au nyingine
kuikubali Kampuni ya ya Afrika Kusini ambayo sifa zake zinafahamika kuwa
ina matatizo.
UVCCM tuna mashaka na kampuni hiyo
iliyopewa kazi ya kuchapisha vifaa vya Uchaguzi ambayo kumbukumbu
zinaonyesha iliwahi kuomba kazi ya kutayarisha vifaa kama hivyo katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na kupewa, lakini SMZ baada ya kugundua
kampuni hiyo ina matatizo, ilivunja mkataba na karatasi za kura
zilichapishwa hapa hapa nchini.
Kampuni hii inalalamikiwa kuwa
chanzo cha kuvurugika kwa chaguzi mbalimbali katika nchi za Afrika
ikiwemo Cameroon, Benin, Ivory Coast na baadhi ya nchi za Latini
Amerika. UVCCM tumeshangazwa sana kuona ZEC wakiikubali Kampuni ambayo
tayari SMZ mwaka 2005 waliikataa na kuvunja nayo mkataba.
Kampuni hii inasemekana kwamba
imekuwa inashirikiana na vyama vya upinzani hasa katika nchi za Afrika
chini ya mkakati wa kuvisaidia kushinda Uchaguzi.
Pia tumepata mashaka na watendaji wa
Tume ya Uchaguzi Zanzibar ama walizembea au walikuwa sehemu ya njama za
kutaka kuvuruga uchaguzi. Kwa nini tunasema hivyo? Ni kwa sababu
watendaji wa Tume ya Uchaguzi wanaifahamu vyema Kampuni hii, matatizo
yake, lakini wameshindwa kuishauri Serikali na matokeo yake kuiingiza
nchi katika hasara na mkanganyiko wa kisiasa.
Tunawataka watendaji wa Tume ya
Uchaguzi Zanzibar kujipima kama wanatosha kuendelea kuwa na sifa ya kuwa
Watendaji wa Tume hii sambamba na Makamishna wao ambao nao hawakujituma
zaidi kujiridhisha na utendaji kazi wa Kampuni hiyo kwa kuzingatia
taarifa za nyuma za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hasa pale ilipovunja
Mkataba.
Kwa mwenendo huo na mtazamo halisia
ni wazi kuwa Chama cha CUF kimehusika na njama hizi za wizi wa kura na
ndio maana Katibu Mkuu wake Seif Shariff Hamad akaamua kukiuka taratibu
na kajitangazia ushindi kinyume na Katiba na Sheria za nchi wakati zoezi
la kuhesabu kura likiendelea katika majimbo ya Pemba na Unguja. Ni
kituko na mshangao kuona vyombo vya dola vikimtazama macho mgombea huyo
aliyefanya kosa la jinai bila ya kumchukulia hatua za kisheria na
kumfikisha kwenye mikono ya sheria.
Umoja wa Vijana wa CCM tunaitaka
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Kuunda Tume huru itakayochunguza kwa kina
na undani wa kadhia hii ikiwemo suala zima la namna ilivyoendeshwa
zabuni hadi kufikia kupatikana mzabuni na taarifa yake itolewe kwa umma.
Ndugu waandishi wa habari,
Tumekuwa tukisema mara kadhaa Chama
cha CUF ni chama ambacho kimezoea kuwahamasisha wafuasi wao kufanya
vurugu, ghilba, ubaguzi na masuala mengine ambayo hayaendani na kanuni
za kidemokasia.
Katika kuyathibitisha haya, wakati
wa kazi ya kupigakura na kuhesabu kura huko Kisiwani Pemba, wafuasi wa
CUF wakiwa na jazba wamevamia vituo vya kupigia kura kinyume cha sheria
na kuanza kuwashambulia kwa mapanga Mawakala wa Chama cha Mapinduzi na
kuwatoa nje, huku wengi wao wakijeruhiwa vibaya.
Wafuasi hao wa CUF wakiwa katika
makundi, wameyafanya hayo katika Vituo vya Majimbo ya Tumbe, Micheweni
na Konde katika Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo Mawakala wa CCM
wamewapiga na kuwajeruhi na kusababisha kusimamishwa kwa kazi za
kuhesabu kura.
Hadi sasa Mawakala wetu hali zao sio
nzuri bado wapo hospitalini wakiendelea kupatiwa matibabu. Tumekuwa
tukijiuliza inakuwaje Pemba CUF hawataki vyama vyengine kushiriki
Uchaguzi kwa kuwafanyia vitendo vya kuwapiga, kuwabagua, kuwabughudhi
wakati wao wanashiriki katika kila uchaguzi ndani ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania?
Ndugu waandishi wa habari,
Haikuishia katika Majimbo hayo tu,
bali uvunjaji wa sheria uliendelea katika sehemu mbalimbali za huko
Pemba ambapo wafuasi wa CUF waliokuwa wamekaa pembezoni mwa barabara
karibu na Vituo vya Makangale, Kisiwani kwa binti Abeid, Chonga,
Mtambwe, Wete, Kojani, Mchangamdogo wafuasi hao wa CUF waliwazuia wana
CCM wasiende kupigakura.
Mbali na kufanya hivyo, pia katika
huduma za usafiri wafanyakazi wa gari za abiria za kutoka Wete kwenda
Gando, Konde-Wete, Chake ? Wete kupitia njia kongwe waliwashusha wana
CCM na huku katika vituo vyengine vya kupanda abiria wakiwakataa wana
CCM wasipande magari yao
Hivi wanataka kutuambia kuwa CCM na
vyama vyengine nje ya CUF havina haki ya kushiriki katika Siasa Kisiwani
Pemba? Ubaguzi huu haukubaliki na tunawaomba wapenda demokrasia wote na
Jumuiya za Kimataifa kuchukia vitendo vya kibaguzi na kihuni
vinavyofanywa na wafuasi wa CUF kule Pemba.
Ndugu waandishi wa habari
Tangu siku ya Jumatatu wafuasi wa
CUF kule Pemba wanachanganya maji na dawa ya kusafishia chooni au kwenye
masinki ya kuoshea vyombo wanawamwagia wafuasi wa CCM ama katika makazi
yao au usiku wakiwa wamelala wanawamwagia maji hayo ambayo yanawaletea
madhara ya kuwashwa mwilini.
Ni dhahiri kuwa Chama cha CUF
hakipati kura nyingi kule Pemba kwa ridhaa ya wapigakura, bali ni kwa
kuwashurutisha wapigakura , kutoa vitisho na hata katika baadhi ya
Majimbo wanawake wametishiwa na waume zao wasipopiga kura CUF watapewa
talaka.
Hali kama hiyo pia imejitokeza
katika Shehia za Kijini na Potoa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo
wanaume waliwashurutisha wake zao kwamba watakapofika kituo cha kupigia
kura wadai hawajui kusoma na kuandika au wana matatizo ya kutokuona
vizuri ili waume zao wapige kura kwa Chama cha CUF. licha ya sheria
kuzuia mikusanyiko ya watu karibu na vituo vya kupigia kura huko Pemba
wafuasi wa CUF walikusanyika karibu na vituo vya kupigia kura Katika
majimbo ya Ole, kojani, Chonga, Mkanyageni, Mtambwe, Wete, Jadida, na
Konde,. Vituo vya shengejuu pujini, kiuyu, Minungw'ini kulikuwa na
wafuasi wa CUF waliokusanyika na hata walipotakiwa kuondoka na polisi
hawakutii.
Ndugu waandishi wa habari,
Yote hayo yametendeka mbele ya macho
ya watendaji wa Tume ya Uchaguzi na licha ya mawakala wetu kulalamikia
ukiukwaji huo wa demokrasia hakuna aliyewasikiliza. Ni wazi kuwa
kuliandaliwa mazingira ya wizi wa kura na ukiukwaji wa taratibu na
sheria uliopewa baraka na baadhi ya watendaji wa Tume ya Uchaguzi
Zanzibar.
Umoja wa Vijana wa Chama cha
Mapinduzi tunalaani vikali vitendo vya wafausi wa Chama cha CUF na
tunaziomba pia Jumuiya za kimataifa kuungana nasi katika kulaani vitendo
hivyo ambavyo havikubaliki hata kidogo.
Tunaviomba vyombo vya ulinzi na
usalama kuwasaka wale wote wanaohusika na uharamia huu na kuwafikisha
katika vyombo vya kisheria.
Sote tunafahamu kuwa misingi ya
uchaguzi huru ni pamoja na masuala mazima ya kutotishwa wapigakura,
kutoshurutishwa kupiga kura kwa Chama fulani kwa maana mpigakura awe
huru kuchagua Chama anachokitaka , kuwepo kwa mawakala na watazamaji
wengine wa Uchaguzi mambo ambayo kwa sehemu kubwa hayazingatiwi katika
Majimbo mengi kule Pemba.
Wakati tukijiandaa kurejea Uchaguzi
wa Zanzibar UVCCM. Tume ya Uchaguzi Zanzibar kuwa makini na watendaji
wake hasa wasimamizi wa vituo kule Pemba ambao kwa namna moja au
nyingine wanashirikiana na Chama cha CUF kuvihujumu Vyama vingine hasa
Chama cha Mapinduzi.
Ndugu waandishi wa habari,
Katika hali isiyokuwa ya kawaida na pengine ilijulikana mapema na waangalizi wa Uchaguzi, Makundi ya Waangalizi wa
Uchaguzi hasa wale wa Kimataifa
walikipa kisogo Kisiwa cha Pemba. Tujiulizeni kwa nini waangalizi wengi
walisalia katika Kisiwa cha Unguja na kukiacha Kisiwa cha Pemba?
Hata hivyo tunazo taarifa za uhakika
kuwa baadhi ya waandishi wa habari nao waliondolewa kwa hila na vitisho
huko Pemba kwa madai kuwa kungeweza kutokea machafuko ambayo
yangehatarisha aidha maisha au usalama wao .
Mpango huo wa vitisho tumepata
ushahidi umeratibiwa na kusimamiwa ipasavyo kwa karibu na waandishi
wawili wa habari wa kike ambao ni wafuasi na mashabiki wa CUF waliokuwa
wakipokea maelekezo kutoka kwa Kiongozi mmoja wa Upinzani huko Zanzibar.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU
Post a Comment