Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, anatarajiwa kuzifuta wizara 15 kati ya zilizopo sasa na kubaki na baraza dogo litakalokuwa na wachapakazi makini ili kutimiza dhamira yake ya kubana matumizi na kuinua maisha ya Watanzania.
Kadhalika,
inaelezwa kuwa Dk. Magufuli aliyeahidi kuleta mabadiliko ya kweli
wakati akiomba kura kwa Watanzania kabla ya kuibuka na ushindi wa
asilimia 58.46 dhidi ya wapinzani wake katika uchaguzi mkuu Oktoba 25,
sasa yuko mbioni kutangaza baraza lake la mawaziri litakalokuwa na
wizara 15, idadi inayofanana kwa kiasi kikubwa na ile ya Baraza la
Mawaziri la miaka ya 1980 lililoundwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Baba
wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Serikali
ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, ilimaliza muda wake Novemba 5,
2015 ikiwa na Wizara 30. Kadhalika, alipoingia kwa mara ya kwanza mwaka
2005, Rais Kikwete alikuwa na serikali kubwa yenye mawaziri na naibu
wao zaidi ya 60.
Kufikia
leo, Rais Magufuli aliyeapishwa Novemba 5, mwaka 2015, tayari
ameshamteua Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu wa
serikali yake ya awamu ya tano na Ijumaa iliyopita alizindua rasmi Bunge
la 11.
Chanzo
kimoja cha uhakika kimedokeza jana kuwa hivi sasa, tayari Rais Magufuli
kwa kushirikiana na wasaidizi wake, ameshakamilisha sehemu kubwa ya
mchakato wa kuunda baraza lake la mawaziri na kwamba, kinachosubiriwa
sasa ni kulitangaza wakati wowote kuanzia sasa.
Chanzo
hicho kilidai kuwa Dk. Magufuli ambaye amejichimbia mjini Dodoma tangu
mwishoni mwa wiki iliyopita, anatarajiwa kutangaza baraza lake dogo la
mawaziri wakati wowote kuanzia leo.
“Halitakuwa
sawa na hili alilomaliza nalo Rais Kikwete… na wala halitakuwa na watu
wengi kama lile aliloingia nalo kwa mara ya kwanza Rais Kikwete mwaka
2005. Ni baraza dogo tu na wizara kadhaa hazitakuwapo,” kilisema chanzo
hicho.
Kwa
mujibu wa ibara ya 55 (1) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mawaziri
wanakuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri na pia kwa mujibu wa ibara ya 54,
mawaziri huteuliwa na rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.
“Kuna
mambo madogo bado hayajakamilika… baada ya hapo Mheshimiwa Rais
atalitangaza Baraza la Mawaziri siku yoyote kuanzia leo. Kimsingi
mkakati wake ni kuwa na baraza dogo lenye wizara 15,” kilieleza chanzo
hicho.
Aidha,
ilielezwa zaidi kuwa sura kadhaa katika baraza hilo dogo zitakuwa mpya
na kwamba, mawaziri waliokuwamo katika serikali ya awamu ya nne wana
nafasi ndogo ya kuteuliwa katika baraza hilo.
“Kwa
kiasi fulani Baraza hili jipya linafanana na lile la Serikali ya
Mwalimu Nyerere miaka ya 1980… lina wizara chache sana, zenye lengo la
kubana matumizi ya serikali lakini likiwa na uhakika wa kuchapa kazi
usiku na mchana ili kutimiza lengo la Rais Magufuli katika kuwaletea
maisha bora Watanzania,” chanzo kiliongeza.
Kumbukumbu
zinaonyesha kuwa miaka ya 1980, Mwalimu Nyerere alikuwa na serikali
yenye wizara 15; ambazo ni Wizara ya Elimu; Wizara ya Mipango; Wizara ya
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Wizara ya Mambo ya Ndani; Wizara ya
Ujenzi; Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Kazi na Ustawi wa
Jamii.
Wizara
nyingine wakati huo ni Wizara ya Habari na Utamaduni; Wizara ya Afya;
Wizara ya Nishati, Madini na Maji; Wizara ya Sheria; Wizara ya Viwanda
na Biashara; Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha.
Post a Comment