Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

ENEO LA IKULU LAUZWA KINYEMELA

Eneo ilikokuwa ijengwe Ikulu ndogo ya mkoa wa Mbeya limeendelea kumegwa na kuuzwa kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni maafisa wa ardhi jiji la Mbeya kutumia fursa ya eneo hilo kujinufaisha kwa kuuza viwanja.

Inaelezwa kuwa baadhi ya maafisa ardhi wa halmashauri ya jiji wamepima viwanja kwenye eneo hilo wakishirikiana na wakazi ambao ilikuwa walipwe fidia kwa mashamba yao,na wakazi hao wanatumiwa kutafuta wateja wa viwanja hivyo ili ionekane wao ndiyo walioviuza kwa watu wanaojenga sasa.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amosi Makalla leo (Agosti 15) ametembelea eneo hilo lililopo Veta jijini Mbeya na kujionea majengo yaliyojengwa kwenye ardhi iliyokuwa sehemu ya uwanja wa kujengwa Ikulu ndogo ya mkoa.

Diwani wa kata ya Ilomba Dickson Mwakilasa amemwambia mkuu wa mkoa kuwa eneo lilikojengwa nyumba za watu binafsi lilikuwa la serikali na kilichotakiwa ni kulipa fidia kwa wakazi waliokuwa na mashamba maeneo ya jirani.

Baadhi ya watu waliokuwa wakimiliki mashamba ndani ya eneo hilo ambao ilikuwa walipwe fidia na serikali wamemweleza mkuu wa mkoa kuwa walichoambiwa wakati wakifuatilia fidia yao ni kuwa wizara imeruhusu maeneo yasiyolipwa fidia yarudishwe kwa wamiliki wa awali na ndipo ofisi hiyo ikaenda kuwapimia na kuwamilikisha kisheria viwanja hivyo kabla ya baadhi yao kujenga na wengine kuwauzia watu wengine wakiwemo vigogo ambao hawakutajwa kwa majina.

Mmoja wa waliokuwa na mashamba ya kulipwa fidia mzee Abeli Mwaigomole,amesema aliambiwa na maafisa ardhi kuwa serikali haitalipa tena fidia hivyo badala yake wenye maeneo waruhusiwe kuyaendeleza.

Naye Didas Makoma ambaye anaendelea na ujenzi wa nyumba yake ya kisasa kwenye eneo hilo amesema anachojua yeye ni kuwa wizara iliruhusu maeneo hayo yaendelezwe kwakuwa serikali haitaweza tena kulipa fidia lakini akasema nyaraka za ruhusa hiyo hana bali zipo ofisi ya ardhi na alizonazo yeye ni za kumilikishwa ardhi pekee alizopewa na ofisi hiyo.

Kufuatia hali hiyo,mkuu wa mkoa wa Mbeya Amosi Makalla amelazimika kuwahoji maafisa wa halmashauri ya jiji lakini wote wakaonekana kutoijua vyema historia ya eneo hilo hivyo ikamlazimu mkuu huyo wa mkoa kutafuta kufuatilia kwa haraka nyaraka husika.

Amesema anachotaka kujua ni ramani inayoonesha ukubwa wa eneo la awali na pia matumizi yaliyopangwa huku akisema anachojua yeye mpaka sasa ni kuwa maafisa ardhi wameuza kinyemela sehemu ya uwanja wa Ikulu ya mkoa.

Kwa upande wake afisa habari wa halmashauri ya jiji la Mbeya,Jackline Msuya amesema halmashauri kama taasisi iliyopewa maagizo na mkuu wa mkoa,itahakikisha ndani ya siku chache inatekeleza maagizo hayo na kutoa taarifa iliyo na usahihi wa jambo hilo.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top