Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Rais Magufuli apokea Tsh. Milioni 545 za tetemeko la ardhi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 27 Septemba, 2016 amepokea msaada wa Shilingi Milioni 545 kutoka kwa Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi kwa ajili ya kusaidia wananchi wa Mkoa wa Kagera waliopatwa na maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 10 Septemba, 2016.

Hundi ya fedha hizo imekabidhiwa leo Ikulu Jijini Dar es Salaam na Balozi wa India hapa nchini Mhe. Sandeep Arya na baadaye Rais Magufuli akaikabidhi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.

Katika barua yake kwa Rais Magufuli iliyosomwa na Balozi Sandeep Arya, Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi amesema Serikali na Wananchi wa India wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kutokea kwa maafa hayo yaliyosababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali.

"Tunaziombea amani na uvumilivu familia zote zilizopatwa na madhara na pia tunapenda kuwahakikishia kuwa tupo pamoja na marafiki zetu Serikali ya Tanzania katika kipindi hiki kigumu" amesema Waziri Mkuu Modi.

Kwa Upande wake Rais Magufuli amemshukuru Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi na Serikali yake kwa kutoa mchango huo na kutuma salamu za rambirambi, na amesema Serikali yake imeguswa na moyo wa upendo waliounesha.

"Mhe. Balozi Sandeep Arya naomba unifikishie shukrani zangu za dhati kwa Waziri Mkuu Mhe. Narendra Modi, mwambie kwa niaba ya Serikali yangu tunamshukuru sana kwa kutoa msaada huu muhimu kwa ajili ya Watanzania wenzetu waliopatwa na maafa kule Kagera.

"Mwambie ameonesha moyo wa upendo na ushirikiano kwetu na tumefarijika kwamba marafiki zetu mmeguswa kwa namna ya kipekee na tatizo lililoipata nchi yetu" amesema Rais Magufuli.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Amantius Msole na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Bw. Steven Makonda baada ya kubaini kuwa wamefungua akaunti nyingine ya benki kwa kutumia jina linalofanana na akaunti rasmi ya kuchangia maafa iitwayo "Kamati Maafa Kagera" kwa lengo la kujipatia fedha.

Taarifa iliyotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa muda mfupi baada ya kupokea hundi ya msaada kutoka kwa Waziri Mkuu wa India imeeleza kuwa pamoja na kutengua uteuzi huo Rais Magufuli ameagiza vyombo vya dola vichukue hatua dhidi ya wote waliohusika katika njama za kufungua akaunti hiyo.

Aidha, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Mkoa wa Kagera Bw. Simbaufoo Swai kutokana na kuhusika katika njama hizo.

Hata hivyo Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wananchi na taasisi mbalimbali kuendelea kuchangia misaada kwa ajili ya walioathirika kwa kutumia akaunti rasmi ya "Kamati Maafa Kagera" ambayo imetangazwa na Serikali.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

27 Septemba, 2016
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru Balozi wa India hapa nchini Sandeep Arya mara baada ya kupokea mfano wa hundi yenye thamani ya Shilingi za Kitanzania milioni 545 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akijadiliana jambo kwa furaha na Balozi wa India hapa nchini Sandeep Arya mara baada ya kupokea mfano wa hundi yenye thamani ya Shilingi za Kitanzania milioni 545 Ikulu jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kulia ni Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje Balozi Dkt. Aziz Mlima.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top