Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Rais Magufuli aonyesha jeuri ya fedha

NI wazi kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imeanza kudhihirisha kwa vitendo, kauli kwamba deni la Tanzania nje ya nchi ni himilivu baada ya kuanza kulipa sehemu ya deni ikiwa na chini ya mwaka mmoja madarakani.

Takwimu zilizotolewa mwishoni mwa wiki na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu zimebainisha hali ya uchumi kuimarika kwa kasi, hatua ambayo imewezesha serikali kuanza kulipa madeni na kutekeleza mipango mikubwa ya maendeleo.

Akithibitisha uwezo wa serikali kuanza kulipa deni la nje na la ndani ambalo limekuwa likipigiwa kelele nyingi na wabunge hususani wa kambi ya upinzani kuwa halihimiliki huku serikali ikisisitiza kuwa ni himilivu, Gavana Ndulu amesema tayari serikali imeanza kulipa madeni hayo kwa kasi.

Gavana Ndulu alisema juzi kuwa BoT imeanza kulipa madeni yote ya ndani na nje kwa fedha zake za ndani ambapo tayari imeshalipa kiasi cha Sh bilioni 96 za deni la ndani huku ikilipa dola za Kimarekani milioni 90 (sawa na Sh bilioni 190) za deni lake la nje.

Alisema kufuatia serikali kulipa Sh bilioni 96 za deni la ndani, deni hilo linasalia kiasi cha Sh trilioni 9.9 huku deni la nje linalofikia dola milioni 620 zikiwamo fedha za mkopo kutoka Benki ya Stanbic, likipunguzwa kwa dola milioni 90.

Ndulu aliwahakikishia wananchi kuwa, uchumi wa Tanzania uko imara, kukiwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni zinazofikia dola bilioni 4, huku ikiendelea kutumia fedha zake za ndani kuendesha shughuli za nchi bila kutumia mkopo kutoka nje, licha ya kwamba inahitajika hususani ile nafuu.

“Hakuna fedha hata senti kutoka nje tuliyotumia tumelipa madeni makubwa na mnaona bado tuna kiasi kikubwa, niseme tu kwa sasa serikali inajiendesha kwa fedha yake ya ndani,” alisema Ndulu.

Kuimarika kwa Pato Akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa alisema katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu, pato la Taifa limeendelea kukua kwa kasi ya asilimia 7.9 ikilinganishwa na asilimia 5.8 ya robo ya pili ya mwaka jana.

Chuwa alisema kutokana na kasi ya uchumi inavyokwenda kwa sasa, huenda ifikapo Desemba mwaka huu, kwenye taarifa ya robo ya tatu ya mwaka pato la Taifa likaongezeka zaidi.

Alisema kwa mujibu wa takwimu zilizopo, pato hilo la Taifa limefika jumla ya thamani ya Sh trilioni 11.7 ikilinganishwa na Sh trilioni 10.9 katika kipindi kama hicho cha mwaka jana.

Naye Gavana Ndulu akizungumzia hali ya uchumi juzi, alisema ukuaji wa Pato la Taifa katika nusu ya kwanza ya mwaka ya Januari hadi Juni, umeongezeka na kufikia asilimia 6.7 kutoka asilimia 5.7 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2015.

Alisema katika robo ya pili ya mwaka 2016, ukuaji wa Pato la Taifa unakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 7.9 ikilinganishwa na ongezeko la asimilia 5.8 kwa kipindi kama hicho mwaka 2015.

Alisema shughuli zinazochangia ukuaji huo wa uchumi kwa kiasi kikubwa kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2016 ni uchukuzi na uhifadhi wa mizigo asilimia 16.0, ujenzi asilimia 10.7 na kilimo asilimia 10.3.

Akizungumzia mafanikio hayo jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana alisema hizo ni dalili za wazi kabisa kwamba sasa serikali ina uwezo mkubwa wa kifedha kuliko ilivyokuwa huko nyuma.

“Ukiangalia takwimu za ukuaji wa uchumi na miradi mikubwa inayofanyika ni uthibitisho tosha kwamba kauli ya Rais Magufuli kwamba serikali ina uwezo wa kulipa madeni lakini pia kununua ndege na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa fedha za ndani, inawezekana,” alisema Bana.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top