Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

MAALIM SEIF AIBUKA NA TAMKO .... HILI HAPA ...HITIMISHO LA MAELEZO YA KATIBU MKUU WA CUF, MAALIM SEIF SHARIF HAMAD- PEACOCK HOTEL. 27/11/2016

Ndugu Wahariri na Waandishi wa Habari,

Sote tunafahamu na ni mashahidi kuwa Profesa Ibrahimu Lipumba alijiuzulu kwa matashi yake mwenyewe, mchana kweupe mbali na sisi wote kama viongozi wenzake kumnasihi na kumshauri kutofanya hivyo kwa wakati ule. Wanachama wa rika zote na viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali walimnasihi sana sana kuacha kufanya hivyo lakini alikataa katakata na kuendelea na msimamo wake wa kung’atuka katika uongozi wa Chama katika Hotel hii hii ambayo leo tunazungumza nanyi. Hoja yake wakati ule ilikuwa kwamba Dhamira na nafsi yake zinamsuta. Kwamba hakubaliani na masuala kuhusu UKAWA, hasa ya kusimamisha mgombea mmoja wa nafasi ya Urais.Tarehe 5/8/2015 aliandika barua hiyo ya kujiuzulu.

Alituacha katika wakati mgumu sana tukiwa katika maandalizi makubwa ya kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana na katika kipindi ambacho Makamu Mwenyekiti wetu, Mheshimiwa Juma Duni Haji alishahamia CHADEMA kwa makubaliano kuwa Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kukidhi matakwa ya kikatiba na sheria za Uchaguzi. Sote ni mashuhuda wa mafanikio ya Ushirikiano wa vyama vyetu katika UKAWA. Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC ulimpa mgombea wetu Mheshimiwa Edward Lowassa asilimia 39.% ya kura, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa katika historia ya chaguzi zote zilizopita. Huko Zanzibar CUF tumeshinda nafasi ya Urais na kushuhudia CCM na Dola kulazimisha kwa kumuamuru Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar –ZEC, kufuta uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 na matokeo halali ya uchaguzi wa Oktoba 25, 2016. Mheshimiwa Edward Lowassa amemshinda Mhe. Magufuli katika matokeo ya kura za urais Zanzibar. Kwa mashirikiano yetu tumeweza kufanya Kampeni kubwa za kisasa zilizoleta ushindani mkubwa na kufanikiwa CUF kupata wabunge katika majimbo kumi (10) ya Tanzania Bara na kuongoza Halmashauri nne nchini. Grafu ya mafanikio kwa CUF na kwa watanzania wapenda mabadiliko imepanda kwa kiwango cha kuridhisha. Bila shaka kujiuzuru kwa Profesa Lipumba imeleta athari kwa CUF na upinzani kwa jumla, ikiwemo kupoteza baadhi ya majimbo na madiwani, kwani CCM waliitumia nafasi hiyo kueneza propaganda chafu wakati wa kampeni. Hakuna Mtanzania ambaye mwenye chembe kidogo kabisa ya kupenda mabadiliko ya kisiasa nchini ambaye hakuumizwa na maamuzi ya ‘Bwana yule’ Chama cha CUF ni Chama cha kidemokrasia, maamuzi yetu yote hupitishwa na vikao rasmi vya Chama ambavyo kwa ngazi ya Taifa ni Kamati ya Utendaji au Baraza Kuu la Uongozi.

Nasikitika kusema kuwa sababu za kujiuzulu kwake sasa zimekuwa zikibadilika siku hadi siku. Mara  Wazanzibar hawamtaki yeye, Mara Maalim Seif Hamtaki Profesa Lipumba, mara inataka iaminishwe kuwa kuna mgogoro baina ya Maalim Seif na Profesa Lipumba. Amekuwa akifanya propaganda za kuwagawa wanachama katika misingi ya Utanganyika na Uzanzibari. Katika vikao vyake vya ndani anasema tunataka kujitoa katika makucha ya Wazanzibari, eti rasilimali za Chama zitumike Tanganyika, eti Wazanzibari wanapendelewa, na eti Chama kimeuzwa na au kinataka kuuzwa kwa CHADEMA na LOWASSA. Wakati mwingine anazungumzia udini. Ndugu zangu haya yote si kweli hata kidogo na hayana mashiko. Profesa Lipumba bado hajasema sababu za kujiuzulu kwake. Aseme sababu za kujiuzulu kwake, asirukeruke.

Suala la UKAWA nani aliyeleta UKAWA ndani ya CUF ?  UKAWA umeanzia Bunge la Katiba. Katibu Mkuu Maalim Seif hakuwa mjumbe wa Bunge la Katiba. Yeye Profesa Lipumba ndiye aliyekwenda kumuona Lowassa na kumtaka ikiwa CCM itamuengua ajiunge na UKAWA. Akashauri ajiunge na NCCR–Mageuzi na CHADEMA na CUF tumuunge mkono. Ni yeye aliyemgotoa kwa waandishi wa Habari. Leo hii yule aliyekuwa anamuita msanii na angemfanya waziri wa sanaa ili aandae mashindano ya warembo ndiye amekuwa rafiki mkubwa wa ‘Bwana yule’ na ndiye aliyesimamia uharibifu wa matokeo ya uchaguzi Zanzibar. Na kama anasema amekosana na Katibu Mkuu Maalim Seif jambo ambalo halijawahi kutokea, na yeye mwenyewe amewahi kukaririwa akisema hivyo. Siku za hivi karibuni lugha imebadilika. Anazungumzia ubaguzi, ‘Usultan’ na ‘Udikteta’ ambao nao ndani ya dhati ya nafsi yake anajua pia kuwa suala hilo ndani ya CUF halipo, Je? aliyawasilisha katika kikao gani cha Chama ili kuyazungumzia masuala haya  kama yalikuwepo ili kuyapatia ufumbuzi? Mahala gani Duniani kuna kiongozi wa juu wa taasisi kubwa kama ya CUF ambaye aliandika barua ya kujiuzulu na kuiacha ofisi yake kwa muda wa miezi kumi, taasisi ikachagua au kuteua kiongozi mbadala wa nafasi hiyo kasha baadae mtu huyo akalazimisha kurejea katika nafasi yake? Profesa LIpumba hakufukuzwa, alijiuzulu kwa hiari yake sasa inakuaje kulazimisha lazima aendelee kuwa mwenyekiti wa Taifa. Mimi naamini hang’ang’anii kwa nia njema. Labda alidhani alipojiuzulu Chama kingeyumba na kufanya vibaya katika uchaguzi. Pia alidhani UKAWA ungeyumba. Matokeo yake yakawa tofauti sana. Ilipoonekana kuwa Wazanzibari na CUF tumekaza uzi katika kudai haki yetu ya kuporwa ushindi wetu, Profesa Lipumba ndio akaja na mpya ya muongo kutengua barua ya kujiuzulu. Nia ikiwa tuache kudai haki yetu na tushughulikie kinachoitwa mgogoro katika Chama. Tunaendelea kudai haki yetu na papo hapo kujidhatiti kuimarisha umoja ndani ya Chama. Chama cha CUF kina ngazi za maamuzi Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lenye wajumbe 63 kwa uwiano sawa kwa pande zote mbili za Muungano. Wajumbe wane (4) wamehama Chama, Mjumbe mmoja amefukuzwa chama na wajumbe sita wamesimamishwa uanachama. Kati ya wajumbe 53 waliobaki wajumbe 46 walikubaliana kwa pamoja na kuazimia kumvua uanachama Profesa Lipumba, kutokana na kukuthiri kwa vitendo vya ukiukaji wa katiba na kanuni za chama, na dhamira ovu iliyojidhihirisha dhidi ya Chama. Si Maalim Seif aliyefanya hivyo, Ni maamuzi ya kikao halali. Mashirikiano ya UKAWA yalipata Baraka ya Baraza KUU la Uongozi Taifa na baadae Mkutano MKUU wa Kawaida wa Chama uliofanyika Ubungo Plaza Mwezi June 28-30 Mwaka 2014 wa kujaza nafasi za uongozi kwa kipindi cha miaka mitano. Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu muhimu tuzingalie changamoto na mapungufu yaliyojitokeza katika ukawa mwaka jana 2015 kuelekea Uchaguzi Mkuu na turekebishe dosari hizo tusonge mbele.

Katika kuendeleza hujuma za wazi dhidi ya CUF Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ilimuandikia Meneja wa Benki ya NMB tawi la Ilala amtambue Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF na aruhusu kufungua akaunti mpya ya Chama itakayosimamiwa nay eye Profesa Lipumba ili aweze kupewa ruzuku ya Chama hali akijua hata kama angekuwa ni Mwenyekiti halali wa CUF kwa mujibu wa taratibu na katiba ya CUF Mwenyekiti hausiki na mambo ya fedha, iliposhindikana kumfungulia Profesa Lipumba akaunti Msajili amezuia ruzuku kwa CUF ili tukwame. Profesa Lipumba hana mamlaka ya chochote kwa sasa katika Chama kwa kuwa Baraza Kuu la Uongozi Taifa limeshamchukulia hatua za kinidhamu na yeye amekata rufaa kwa Mkutano Mkuu wa Taifa juu ya maamuzi hayo. Baraza Kuu la Uongozi Taifa kwa mujibu wa katiba ibara ya 118 limeteua Kamati ya Uongozi Taifa inayoongozwa na Mheshimiwa Julius Mtatiro. Kamati hii ni halali na inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

Ndugu wahariri na waandishi wa Habari,
Tumekuelezeni haya si kwa lengo la kulalamika tu, bali tunaweka kumbukumbu sahihi ya mtiririko wa matukio katika historia ya demokrasia na kuendeleza utaratibu wetu tangu kuasisiwa kwa CUF. Na kutoa tanbihi kwa Jeshi la Polisi na taasisi nyengine za kitaifa kama Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kufuata sharia zilizopelekea kuundwa huko badala ya kuwa ni sehemu ya kutengeneza machafuko na mifarakano kwa maslahi ya kisiasa.  Vyombo vya dola havikutarajiwa kuweza kukubali kutumiwa kwa maslahi ya kundi Fulani la kisiasa.
Itakumbukwa kuwa CUF imevuka vigingi vizito katika nyakati tofauti kila ilipojaribiwa ikiwa kwa uadui wa ndani au wa nje. Na kwa ithibati, dhati na imani kubwa ni kwamba mwisho wa vitimbi hivi vyote, CUF itaibuka mshindi. Tunatoa wito kwa wanachama, wapenzi wa CUF, na watanzania wote kwa ujumla wapenda mabadiliko, waendelee kuwa na Subira. Hakika hili litapita. Subra uvuta kheri.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

HAKI SAWA KWA WOTE

MAALIM SEIF SHARIF HAMAD
KATIBU MKUU
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top