Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Faru John kupimwa DNA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda tume kuchunguza taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti Serengeti pamoja na kutafuta kaburi la faru huyo.

Amesema timu hiyo ya wataalamu tayari imeshafika Sasakwa  VIP Grumet kwa ajili ya kutafuta kaburi na kuchukua vinasaba vya masalia ya faru John na kisha watakwenda kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kuchukua vinasaba vya watoto wake  na kuvilinganisha na pembe hiyo ili  kubaini kama kweli pembe aliyopelekewa ni  ya faru John au la.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumapili, Desemba 18, 2016 wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kikazi mkoani Arusha. Ziara hiyo ililenga kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuona utoaji wa huduma kwa wananchi.

"Tume niliyounda kwa ajili ya uchunguzi wa faru John imetua VIP  Grumet Serengeti kujiridhisha kama kuna kaburi la faru John na kama lipo wachukue vinasaba na baada ya hapo watakwenda Creter na kuchukua vinasaba vya watoto wa faru John na kuvipima kwa pamoja. Lengo ni kutaka kubaini kama pembe iliyowasilishwa kwangu Disemba 9 mwaka huu ni ya faru John,” alisema.

Waziri Mkuu alisema wakati faru John akiwa V I P Grumet taarifa zilisema ni mgonjwa na daktari alipompima mara ya kwanza akabaini faru huyo hakuwa na ugonjwa wowote.”Daktari alimpima tena kwa mara ya pili taarifa zikasema tena si mgonjwa  ghafla wakasema amekufa. Hili  haliwezekani,”.

Waziri Mkuu alisema ameiagiza timu hiyo kufanya kazi ya uchunguzi wa taarifa hizo kikamilifu kwa sababu Serikali imetumia fedha nyingi kuwaleta faru hao kutoka nchini Afrika Kusini. Ni lazima nyara hizo za Serikali zilindwe kwa manufaa ya Taifa.

Waziri Mkuu alipokea taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti Desemba 9, 2016 katika kikao kilichofanyika kwenye makazi ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na baadhi ya watendaji wa wizara yake, Baada ya kupokea taarifa hiyo Waziri Mkuu alisema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake.

Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Maghembe alisema hadi kufikia Desemba 2015 wakati faru John anahamishwa alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.

“Kati ya faru 37 waliokuwepo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26 sawa na asilimia 70.2. Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Waziri Maghembe.

Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru John ilianza kudorora na alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka huu.
 
 Taarifa hiyo iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru. Kamati hiyo inaundwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Mkurugenzi Mkuu wa NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.

 Akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert Mande alimweleza kwamba pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.

Desemba 6, mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru maarufu kwa jina la ‘John’ kutoka kwenye hifadhi hiyo ifikapo Alhamisi, Desemba 8.

Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

IMETOLEWA NA:                                                        
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top