Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Magufuli aanza kuinyoosha CCM

CCM imeanza mchakato wa kuwashughulikia wasaliti ndani ya chama hicho, walioisumbua kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. 

Hatua hiyo ni miongoni mwa mambo ambayo Kamati Kuu ya CCM iliyoketi jana jijini Dar es Salaam ikiongozwa na mwenyekiti wake, Rais John Magufuli ilijadili ikiwa ni sehemu ya tathmini ya uchaguzi huo. 

Tangu uchaguzi huo umalizike ambapo mgombea wa CCM, Rais Magufuli aliibuka na ushindi wa asilimia 58.46 dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyepata asilimia 39.97, madai ya kuwapo wasaliti waliomuunga mkono yalitawala na kuwekwa mikakati ya kuwashughulikia kupitia vikao. 

Mbali na kusababisha ushindani mkali dhidi ya CCM, Lowassa aliyehama chama hicho baada ya kuenguliwa katika mchakato wa urais na kwenda Chadema, aliviwezesha vyama vinavyounda Ukawa kupata wabunge 116, idadi kubwa kuwahi kufikiwa tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe. 

Pamoja na Lowassa kuhamia upinzani, mwanasiasa huyo aliendelea kuungwa mkono ndani ya CCM na mara kadhaa ametoa kauli zinazoonyesha kuwa bado ana wafuasi ndani ya chama hicho. 

Wakati akikabidhi chama kwa Rais Magufuli, mwenyekiti aliyemaliza muda wake na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alimkabidhi pamoja na ripoti ya uchaguzi ikiwa na orodha ya wanaodaiwa kukisaliti chama kutoka maeneo mbalimbali nchini wakisubiri hatua za vikao vya juu.

 Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema tathmini hiyo inafanyika kwa lengo la kukiimarisha chama kwa chaguzi zijazo. 

“Agenda iliyozungumzwa leo ni tathmini ya uchaguzi wa mwaka 2015. CCM iliagiza ngazi zake za mashina, kata wilaya na mikoa, wafanye tathmini ya uchaguzi wa mwaka 2015 wa madiwani, wabunge na rais. 

“Tathmini hiyo ilikuwa ni pana, imefanyika kwa kipindi cha mwaka mzima. Mikoa na wilaya zake na kata zao na matawi yake na mashina yake, wameagizwa wakaleta Kamati Kuu ya chama,” alisema Nape ambaye pia ni waziri wa habari, utamaduni, michezo na sanaa. 

Alisema tathmini hiyo ilipitiwa na sekretarieti ya chama kabla ya kupelekwa kwenye Kamati Kuu ambako nako itapelekwa kwenye Halmashauri Kuu kwa maamuzi zaidi. 

“Baada ya kujadiliwa na Kamati Kuu itapelekwa kwenye kikao cha NEC ambacho ndicho kikao cha maamuzi , kitatoa maelekezo ya mambo ya kufanya na hatua za kuchukua,” alisema Nape. 

“Nisingependa kuzungumzia sana nisije ku-pre empty NEC, ninachoweza kusema ni kwamba chama kimepokea tathmini, wanachama wametoa mawazo yao, maoni yao wameleta kwenye vikao, tusubiri maamuzi ya vikao. Ndiyo siri ya uimara wa CCM,” alisema bila kuzungumzia ajenda nyingine zilizojadiliwa. 

Hatua ya CCM kufanya tathmini hiyo imekuja wakati wakiwapo baadhi ya makada ambao hawakuridhishwa na uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho kukata jina la Lowassa. 

Katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM uliofanyika Julai 2015, baadhi ya wajumbe akiwamo Dk Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa ambaye ni mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, walipinga hadharani hatua ya kukata majina ya wagombea kinyume cha kanuni za chama hicho, hali iliyoelezwa kuwakera viongozi wakuu wa chama hicho. 

 Akihutubia mkutano wa kumkabidhi uenyekiti wa CCM Julai 23, 2016 mjini Dodoma, Mwenyekiti mstaafu Jakaya Kikwete alisema mchakato wa kumpata mgombea urais wakati huo ulikuwa mtihani mgumu uliotishia kukigawa chama hicho. 

“Mi nadhani katika historia ya CCM hakuna wakati kulikuwa na tishio la kugawanyika kama mwaka jana. 

“Tumeingia kwenye NEC haijapata kutokea ya namna ile. Lakini tukasema hatutayumba, maadamu sisi viongozi juu tumeshikamana, tutashinda,” alisema Rais Kikwete. 

Lakini akihutubia mkutano huo baada ya kukabidhiwa uenyekiti Julai mwaka huu, Rais Magufuli aliwataka wanachama wanaokisaliti chama hicho kutubu au  waondoke mara moja. 

“Tunataka tukomeshe usaliti ndani ya chama. Katika uongozi wangu na ninaomba Mungu anisaidie na mnisaidie tushikamane ndugu zangu, nitahakikisha usaliti unakomeshwa,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:

 “Ndani ya chama chetu pamekuwa na tabia ya baadhi ya wanachama kusaliti chama. Asubuhi anakuwa CCM usiku yuko Chadema, au yuko chama kingine. Wasaliti wa namna hii hawatakuwa na nafasi katika uongozi wangu. Kama wapo wenye tabia hiyo, ni vema wakajirekebisha na kutubu kuanzia leo. 

“La sivyo watupishe ikiwezekana hata leo, waondoke. Ni vema kuishi na mchawi kuliko kukaa na msaliti. Na hili lazima niliseme na ninalisema kwa dhati. Narudia tena, kama wapo watubu kuanzia leo.” 

Alisema katika uongozi wake anataka wanachama waadilifu wanaofuata Katiba na maadili ya chama chetu, siyo ndumilakuwili.

 “Hatuhitaji CCM pandikizi na wana CCM masilahi ambao wapo CCM kwa sababu wanamwabudu mtu fulani kwa masilahi yao binafsi. Ninahitaji wana CCM ambao siku zote, usiku, mchana, mvua ikinyesha, jua likichoma, njaa ikiuma, shibe wameshiba, watabaki CCM bila kuyumba.” 

 Akizungumzia baadhi ya wanachama waliokihama chama hicho wakati wa uchaguzi na kurejea, Rais Magufuli aliwafananisha na ng’ombe waliokatika mikia. 

“Sisi wachunga ng’ombe, nafahamu hata mzee wetu Kikwete kwa sababu ana ng’ombe. Ng’ombe akikatika mkia humzuii kuingia zizini, japo wenzake watajua huyu hana mkia,” alisema Rais Magufuli ambaye pia alisema yeye hana uvumiliku wa Kikwete, na kuwa kama angekuwa yeye wale walioimba wana imani na fulani (Lowassa), nusu au robo wangepotea. 

Alikuwa anamaanisha wajumbe wa Halmashauri Kuu walioimba wimbo wa “Tuna imani na Lowassa” mara baada ya Kamati Kuu kukata jina la mwanasiasa huyo. 
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top