Dar es Salaam. Japokuwa bei ya sembe imeendelea kupanda kwa miezi miwili sasa na kuzua hofu, Serikali imesema ni hali ya kawaida kwa miezi ya Desemba na Februari kila mwaka ila imepanga kuingiza sokoni unga kupitia Bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Tate Ole Nasha alipotafutwa na mwandishi wa habari hizi ili aweze kufafanua kuhusu kupanda kwa bei ya unga na hatua zinazochukuliwa na Serikali kudhibiti hali hiyo.
Ole Nasha alikuwa akitoa ufafanuzi wa habari ya uchunguzi iliyoripotiwa na gazeti hili jana kuhusu kupanda kwa bei ya sembe kutoka kati ya Sh800 na 1,000 kwa kilo hadi kufikia Sh1,500, huku mfuko wa kilo 25 ukiuzwa Sh29,500 badala ya kati ya Sh22,000 na Sh24,000.
Uchunguzi wa Mwananchi uliofanywa kuanzia mapema mwezi uliopita umebaini kuwa mikoa maarufu kwa uzalishaji mahindi ya Ruvuma, Njombe, Mbeya na Rukwa imeingiliwa na walanguzi ambao wananunua mahindi na kuyasafirisha kwenda nchi jirani zenye uhaba wa chakula. Katika Mkoa wa Arusha bei ya unga na mahindi imepanda kutokana na kiasi kikubwa cha mazao hayo, kuuzwa nchi jirani ya Kenya. Katika masoko ya Kilombero na soko kuu la Arusha kwa sasa kilo moja ya unga inauzwa kati ya Sh1,100 na 1,300 kutoka kati ya Sh850 na Sh1,000 ya Juni mwaka huu.
Vilevile, bei ya gunia moja imepanda kutoka Sh50,000 hadi kufikia Sh75,000 hali ambayo inatishia bei kupanda zaidi kabla ya kuanza kilimo na mavuno.
Kwa mujibu wa kitengo cha intelejensia ya biashara ya mazao cha nchini Kenya (RATIN) Juni mwaka huu Kenya ilinunua tani 13,103 za mahindi kutoka Tanzania.
Waziri Ole Nasha alikiri kuwa ni kweli bei ya unga wa sembe katika mikoa mbalimbali nchini imepanda lakini alisisitiza akisema kwa miezi hii ni jambo la kawaida na kwa mwaka huu inatokana na mazao ya vyakula yaliyovunwa msimu uliopita kukaribia kwisha hivyo wanasubiri kuvuna msimu mpya.
Pia, aliafikiana na uchunguzi wa Mwananchi akisema hali ya chakula kwa nchi jirani si nzuri hivyo baadhi ya wafanyabiashara hununua mazao ya vyakula na kusafirisha kwenda kuuza nje ya nchi. “Ndiyo maana katikati ya mwaka huu Serikali ilipiga marufuku uuzaji wa vyakula nje ya nchi ili kukabiliana na hali inayojitokeza sasa,” alisema.
Ole Nasha alitaja sababu nyingine kuwa ni tabia ya wafanyabiashara kuficha mazao hususani mahindi wakisubiri kuangalia hali ya hewa itakuwaje, kama kutakuwa na ukame wauze kwa bei ya juu na kama kutakuwa hakuna wauze kwa bei ya kawaida.
“Halijakuwa tatizo kubwa kiasi cha kuwachukulia hatua wanaofanya hivyo, iwapo hali itakuwa mbaya kuna sheria za kuwabana na ni rahisi kuwabaini pia,” alisema Ole Nasha.
Suluhisho
Ole Nasha amesema Serikali imeweka mipango mitatu ya kukabiliana na tatizo hilo. Kwanza wanakamilisha taratibu ndani ya Wizara ili muda mfupi ujao kupata mahindi kutoka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na kukabidhi kwa Bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko.
Alisema bodi hiyo itasaga mahindi hayo na kuingiza unga sokoni na kwa kufanya hivyo bidhaa hiyo itakuwa nyingi na hatimaye bei itapungua. Aliutaja mkakati mwingine wa kunusuru kupanda kwa bei ya vyakula kuwa ni kujizatiti kuhakikisha NFRA inakuwa na chakula cha kutosha.
“Hivi tunavyoongea wanaendelea na kununua chakula kwa wakulima. Hatua ya tatu ni wiki ijayo timu yenye wajumbe kutoka Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Waziri Mkuu na mikoa itafanya tathmini ya kina kuhusu hali ya chakula, kubaini upungufu,” alisema.
“Baada ya kubaini upungufu kitaingizwa chakula cha kutosha sokoni kwa bei ambayo wananchi wanamudu kununua.”
Lakini Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dk Bilinith Mahenge amesema pamoja na bei ya mahindi kupanda mara kwa mara, bado mkoa uko salama na una akiba ya kutosha ya chakula.
“Nimeshaagiza vyombo vya dola kusaidiana na maafisa uhamiaji kuhakikisha hakuna mahindi yanayovushwa kwenda nje hadi wafanyabiashara watakapopata kibali kutoka Wizara ya Chakula,” alisema
Wachuuzi
Mchuuzi wa mahindi kutoka mkoani Kilimanjaro Eliakimu Yunus aliliambia gazeti hili kuwa bei ya mahindi imepanda kutoka Sh 50,000 kwa gunia la kilo 100 hadi Sh 75,000. Alisema bei hiyo imepanda zaidi ndani ya mwezi mmoja kwani hapo awali walikuwa wananunua Sh65,000.
“Inavyoonekana kuna tatizo, pamoja na kuuza bei hiyo hatupati faida ya kutosha tunafanya biashara kwa mazoea, tunarudisha mtaji na kulinda goli,” alisema Yunus.
Mfanyabiashara mwingine wa mahindi kutoka mkoani Tanga, Rajabu Kitapa alisema bei ya mahindi kwa gunia la kilo 100 linauzwa kati ya Sh 68,000 na Sh70,000 tofauti na miezi miwili iliyopita ambapo liliuzwa kwa chini ya Sh 60,000.
Mmiliki wa mashine za kusaga nafaka wa mkoani Kigoma Miriambu Obinga alisema mwezi uliopita debe la mahindi liliuzwa Sh 12,000 lakini sasa limepanda hadi Sh 14,000.
Loading...
Post a Comment