Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Waziri Mkuu atinga gereza la Ukonga


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam na kukagua eneo la ujenzi wa makazi ya askari wa Magereza unaotarajiwa kuanza baada ya wiki tatu zijazo.

Akizungumza na askari wa magereza kabla ya kufanya ukaguzi huo jana Jumamosi, Desemba 24, 2016 Waziri Mkuu alisema ziara aliyoifanya , ni ufuatiliaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati alipoenda kukagua gereza hilo.

Novemba 29, mwaka huu, Rais Magufuli alifanya ziara kwenye gereza hilo na kupokea taarifa ya uhaba wa nyumba za kuishi askari wa jeshi hilo zipatazo 9,500 na akaagiza zitafutwe sh. bilioni 10 haraka ili kupunguza tatizo hilo.


Akizungumzia kuhusu ujenzi huo, Waziri Mkuu alisema amefarijika kukuta Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wako eneo la kazi na wameanza kusafisha eneo hilo.


“Nimefarijika kukuta TBA wako kazini na nimeelezwa hatua inayofuata ni upimaji wa sampuli za udongo kabla hawajaanza kujenga msingi. Nawapongeza TBA kwa kazi nzuri wanazofanya za ujenzi wa nyumba zenye viwango na kwa haraka kama tulivyoona kule Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nyumba za Magomeni Kota,”alisema.


Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua mchango uliofanywa na Serikali ya awamu ya nne katika suala la makazi ya askari kama vile wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) na Jeshi la Polisi. 


“Nia ya Serikali ni kuhakikisha makamanda wote wanapata nyumba nzuri ili waendelee kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa wakiwa na uhakika familia zao zimetulia kwenye makazi bora”.

Alisema katika ziara alizozifanya kwenye mikoa mbalimbali, alitembelea magereza ya Isanga, Msalato (Dodoma), Lindi, Singida na Keko (Dar es Salaam) alikuta nyumba za askari hazina viwango na kama zipo zimechakaa sana.


Mapema, akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa nyumba hizo, Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Juma Malewa alisema wanamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa makazi ya askari na kwamba jeshi hilo litafanya kazi zote zisizo za kitaalamu ili kuokoa fedha za Serikali na badala ya kulipwa watu binafsi, fedha hizo zitatumika kuongeza nyumba zaidi.


“Tumekubaliana na TBA kazi zote zisizohitaji utalaamu kama kufyatua matofali, kubeba mizigo au kufyeka zitafanywa na askari wetu pamoja na wafungwa ili tuokoe gharama zote hizo na badala ya kulipa watu binafsi, fedha hizo zitumike kujenga nyumba nyingine 80,”alisema huku akishangiliwa.


Alisema wamejipanga kufanya kazi hizo kwa saa 24 kila siku ili kuokoa muda ambao TBA walikuwa wameuweka wa kukamilisha ujenzi ndani ya miezi minane.


Alisema wako tayari kuanzisha kambi za ujenzi kwa kutumia wafungwa na askari ili wafanye kazi zisizohitaji utaalamu na fedha zitakazopatikana, badala ya kuwalipa watu binafsi zitumike kujenga nyumba zaidi za askari.


Naye mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TBA, Bw. Baltazar Kimangano alisema wanataraji kuanza ujenzi ndani ya wiki tatu baada ya kupokea matokeo ya uchunguzi wa sampuli za udongo kutoka taasisi ya BICO ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.



Alisema wanataraji kujenga majengo (block) manne ya ghorofa sita kila moja ambayo kwa ujumla yatakuwa na nyumba 240 zenye ukubwa wa vyumba viwili vya kulala. Pia watajenga majengo (block) mengine mawili ya ghorofa sita kila moja ambayo yatakuwa na nyumba 80 zenye ukubwa wa vyumba vitatu vya kulala.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua gwaride lililoandaliwa na Jeshi la Magereza wakati alipowasili kwenye gereza la Ukonga jijini Dar es salaam kukagua maadlizi ya ujenzi wa nyumba za makazi ya Askari Magereza Desemba 24, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea heshima kutoka kwa gwaride lililoandaliwa na Jeshi la Magereza wakati alipowasili kwenye gereza la Ukonga jijini Dar es salaam kukagua maadlizi ya ujenzi wa nyumba za makazi ya Askari Magereza Desemba 24, 2016.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokwenda kwenye Gereza la Ukonga kukagua maandalizi ya ujenzi wa nyumba za makazi ya askari Magereza Desemba 24, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua maadalizi ya eneo la ujezi wa nyumba za askari magereza katika gereza la Ukonga jijini Dar es salaam Desemba 24, 2016. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni na kushoto kwake ni Kaimu Kamishina Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Ali Malewa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Maofisa wa Jeshi la Magereza baada ya kukagua maandalizi ya eneo zitakapojengwa nyumba za makazi za Askari magereza katika gereza la Ukonga jijini Dar es salaam Desemba 24, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top