Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba jana ‘alimkalia kooni’ Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (Chadema) kwa kauli yake kwamba wabunge wanaogopa kujadili mauaji yanayoendelea Kibiti wakihofia yatahamia kwao.
Mwigulu alichukizwa na kauli hiyo jana bungeni wakati wa mjadala kuhusu kuridhia itifaki ya udhibiti wa mazingira ya bahari na ukanda wa Pwani ya Magharibi ya Bahari ya Hindi kutokana na vyanzo na shughuli zinazofanyika nchi kavu.
Nyingine ni itifaki ya Kusimamia Upatikanaji na Mgawanyo sahihi wa faida zinazotokana na matumizi ya rasimali za jenetiki.
Wakati akichangia, Lema alisema wabunge wasishangae mauaji yanayotokea Kibiti yakisambaa nchi nzima.
“Kila mtu anaogopa kujadili suala la Kibiti, Bunge linaogopa kujadili wanaona wakianza kujadili jamaa anaweza kuhamia huku,”alisema Lema.
Akijibu, Waziri Mwigulu pamoja na mambo mengine, alisema Serikali haitaacha eneo hata moja la nchi likatawaliwe na wahalifu.
“Tutashughulika na mmoja mmoja, watu wetu watafanya kazi katika mazingira salama.
“Unaongea kimzaha mzaha, taswira iliyoko ndani inahusiana na siasa, leo ukituambia yale ya Kibiti yanaendelea na maeneo mengine tunaendelea kutafuta uhusiano, kama leo kauawa wa CCM, kaacha mwingine kule…. kuna haja ya kutusaidia kwa nini unasema yanaendelea, kwa nini unadhani wanashindwa…
“Katika panga kazi zetu tunahakikisha wananchi wa maeneo yote wanakuwa salama…sentesi kama hizi hata kama zinasemwa bungeni nadhani kuna umuhimu ndugu zetu hawa wakasaidia kujua kiini ama kinatoka bungeni ama kinatoka wapi, lakini sasa wanahangaika na watu wengine,” alisema.
Wilaya za Mkoa wa Pwani za Rufiji, Kibiti na Mkuranga zimekumbwa na mauaji ya viongozi wa vijiji na vitongoji tangu Mei mwaka jana na hadi sasa zaidi ya watu 30 wameuawa.
Mauaji mengi yamekuwa yakifanyika usiku kwenye nyumba za viongozi na watu wengine ambao wamewahi kushika uongozi, idara ya maliasili na polisi.
Bunge jana liliridhia itifaki ya udhibiti wa mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani ya Magharibi ya Bahari ya Hindi kutokana na vyanzo na shughuli zinazofanyika nchi kavu na ile ya itifaki ya Kusimamia Upatikanaji na Mgawanyo sahihi wa faida zinazotokana na matumizi ya rasimali za jenetiki.
Post a Comment