Wabunge wakiwa ndani ya Bunge
Na
Emmanuel J. Shilatu
Wabunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliipitisha bajeti ya mwaka 2012/ 2013 ambapo
jumla ya Tsh. Trillioni 15 zimepita huku wabunge wa vyama vya upinzani John
Shibuda wa Maswa Mashariki kupitia tiketi ya Chadema na John Cheyo, Mbunge wa
Bariadi Mashariki kupitia chama cha UNDP wakipiga kura za NDIYO na hivyo kuipa
nguvu ya ushindi Bajeti hiyo.
Upigaji huo wa kura
uliokuwa wa kuitwa kwa jina Mbunge mmoja mmoja na kupiga kura kwa kusema kwa
sauti kama ni NDIYO au HAPANA uliwashirikisha jumla ya Wabunge 297 kati ya 357
ambapo Wabunge 225 walisema ndiyo na Wabunge 72 walisema hapana na Wabunge 54
hawakuwepo Bungeni.
Katika upigaji kura
huo, uligubikwa na dosari ndogo za majina ya Wabunge wanne kutokuonekana na
hali ya kukatika umeme ukijitokeza na kupunguza utulivu ndani ya Bunge. Wabunge
ambao walisahaulika ni Mh. Ali Juma Haji, Mh. Shukuru Kawambwa, Mh. Haji Seif
na Mh. Joseph Mbilinyi wa Mbeya Mjini.
Mara baada ya matokeo
ya kupitishwa kwa Bajeti hiyo kutangazwa na Spika Anne Makinda wabunge wa CCM
walikuwa wakishangilia kwa kusema “CCM CCM” na wengineo walijibu “JUU”. Wao
wapinzani waliitikia kwa kusema “Magamba”
Wabunge walio wengi wa
upinzani waliikataa Bajeti hiyo kwa kusema "hapana" isipokuwa Mh.
John Shibuda na Mh. John Cheyo walioamua kuweka kando itikadi za kisiasa na
kutanguliza uzalendo mbele kwa kuiunga mkono Bajeti hiyo.
Bajeti hiyo ambayo
ilisomwa Juni 14, 2012 iliwapa fursa kwa wabunge kuipitia na kutoka mapendekezo
yao ya maboresho ambapo Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa aliyaridhia
mapendekezo ya Wabunge na akahaidi kuyaingiza kwenye Bajeti.
Vipaumbele vya Bajeti
hiyo ni miundombinu, kilimo, viwanda na rasilimali watu. Ukitizama vipaumbele
hivyo utagundua ya kuwa haviendani kabisa na mahitaji ya kimsingi ya kijamii na
hata pia hayaendani na mtazamo wa Serikali iliyopo madarakani.
Jamii ilitarajia Bajeti
hii ingekuja na suluhisho la mahitaji yao msingi ya uondoaji wa matatizo ya
umeme, matatizo ya maji na pia maboresho ya kilimo lakini vitu vyote hivyo
havikupewa kipaumbele kwenye Bajeti hiyo. Hii inamaanisha ya kuwa Watanzania
wataendelea kuogelea kwenye dimbwi la matatizo yao yale yale yanayowasumbua.
Alikadhalika Bajeti
hiyo imeshindwa kuendana na mtazamo wa serikali ambao ulikuwa ni mapinduzi ya
kijani kupitia kilimo kwanza ambacho ndicho tegemezo kwa Watanzania zaidi ya
asilimia 80. Lakini jambo la kushangaza kilimo hakijapewa kipaumbele kwenye
Bajeti hii na hivyo kuwapa mzigo wa kimaisha kwa Watanzania wanaoikitehemea kilimo
kama kwa biashara (kiuchumi) na hata kwa chakula. Kazi tunayo Watanzania!
Nasema kazi tunayo
Watanzania nikiwa na maana ya kuwa ule mfumuko wa bei uliofikia asilimia 20
ambao ulipanda kutokana na kuadimika na kuongezeka kwa bei za vyakula, utaendelea
kutusakama na hivyo kuongeza maisha magumu kwa Watanzania.
Pia Bajeti hii haina
utofauti sana na zile za miaka ya nyuma kwa upande wa mategemeo ya vyanzo vya
mapato vilivyozoeleka kuwa ni sehemu mojawapo inayomkandamiza Mwananchi wa
kawaida.
Serikali imeendeleza
wimbi la kuongeza kodi kwenye bidhaa zile zile za kila siku za bia, sigara,
mvinyo, soda, magari kuukuu. Pia safari hii wameongeza gharama za simu. Hii ina
maana ya kuwa maisha ya Mtanzania yatazidi kubanwa zaidi ya awali kwani gharama
za simu zilizoongezeka zitazidi kupoteza ndoto za Maisha bora kwa kila
Mtanzania kwani watu wengi sana hutumia simu kama sehemu mojawapo ya
utengenezaji kipato kwani wengi wao hufanya biashara kupitia simu. Kazi tunayo
Watanzania.
Pia changamoto nyingine
ambayo itajitokeza na kuzima ndoto za maisha bora kwa kila Mtanzania ni suala
zima la utengwaji mdogo wa pesa za kimendeleo ambapo katika Bajeti hii ya 2012/
2013 imetengwa asilimia 30 tu (kwa ajili
ya maendeleo) na asilimia 70 za bajeti zimepelekwa kwenye matumizi ya kawaida.
Pesa hizi za kimaendeleo zimeshuka kutoka trilioni 4.9 za bajeti ya mwaka jana
hadi kufikia trilioni 4.5 kwa mwaka huu.
Hii ina maana ya kuwa
utekelezaji wa shughuli za kimaendeleo utashuka na matokeo madogo ya
kimaendeleo yatajitokeza. Pia Serikali imeonelea ni bora iongeze pesa za posho
za vikao, vitafunwa, kuongeza semina kwa wakubwa, kuongeza mashangingi kuliko
kwenda kununua madawa mahospitalini, kuwaboreshea mishahara watumishi wa umma,
kujenga nyumba za Waalimu. Hiyo ndiyo bajeti yetu, ilyojaa changamoto tele.
Wajibu
wa Serikali kwa Bajeti hii
Tumeshuhudia kwa
iliyopita utafunwaji wa pesa za umma ulivyofanyika kwa kiwango cha kutisha kama
ambavyo Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali alivyobainisha kwenye
ripoti yake. Na bajeti ya mwaka huu kiwango cha bajeti kimeongezeka kwa
takribani trilioni 2.
Kuongezeka huko
hakutakuwa na maana endapo hakutakuwa na mikakati thabiti ya kuibana bajeti
dhidi ya mchwa wanaoingiza pesa za umma mifukoni mwao kutokana na kukosa
uzalendo kwa Taifa lao. Serikali ina wajibu wa kuwa wakali sana katika bajeti
hii ili matokeo chanya yaonekane kwa walio wengi.
Tatizo lingine
lililojitokeza kwenye bajeti iliyopita ni hali ya kutumia zaidi kuliko mapato.
Hii ilisababisha ongezeko la mfumuko wa bei na pia ongezeko la deni la Taifa
ambalo linatugharimu kulipa jumla ya trilioni 29 ambazo ni sawa na asilimia
19.3 za bajeti ya mwaka huu. Tunalipa pesa zote hizo kutokana na kutumia zaidi
kuliko mapato yaliyopo.
Serikali ina wajibu
mkubwa wa kuhakikisha inathibiti matumizi yake ya ndani ili yaendane na
uhalisia wa kipato chetu. Serikali isikilize kilio cha walio wengi kwa
kuhakikisha wanapunguza safari za wakubwa nje ya nchi tena wakiwa na timu kubwa
ya wasafiri, ihakikishe inapunguza semina, kupunguza kiwango cha posho wanazojilipa.
Hayo yote yakifanyika bila shaka mipango yetu kimatumizi itaendana na mapato
yetu.
Bajeti hii imembana
Mtanzania kutokana na ufinyu wa pesa za maendeleo. Njia pekee ambazo Mwananchi
wa kawaida atanufaika na bajeti hii ni kupitia mambo makuu mawili ambayo
serikali inaulazima wa kuyatimiza. Kwanza; ni kuhakikisha inathibiti vilivyo
mfumuko wa bei kwa kutekeleza ahadi ya kuongeza pato la Taifa kwa kuhakikisha
wanaongeza mapato ya ndani. Pia wahakikishe wanaongeza mikopo kwa sekta binafsi
kwa asilimia 20 ya pato la Taifa.
Pili; ni kuhakikisha
inatekeleza kwa vitendo ahadi ya kuongeza ajira mpya 71756 walizohaidi ili
kukabiliana na janga hili la kitaifa. Endapo Serikali itafanikiwa kuongeza
ajira mpya ni dhahiri itapunguza kundi kubwa la watu tegemezi katika jamii.
Bajeti imepangiliwa
lakini upangiliaji huo hautakuwa na maana endapo Serikali haitatimiza wajibu wa
kujikita katika kuboresha miundombinu ya barabara, umeme, maji, kilimo na
mawasiliano hawatakuwa wametimiza wajibu kwa bajeti hiyo.
Utamu
wa Bajeti
Licha ya madudu mengi
ya bajeti hii lakini pia haijakosa mazuri yake. Bajeti hii imenifurahisha
kutokana na uamuzi wa serikali kuanzisha kodi ya ongezeko la Thamani (VAT)
maalum ya asilimia 10 kwa wale ambao walikuwa hawatozwi kwa sasa. Hatua hii
itasaidia kuongeza mapato ya Serikali yaliyokuwa yakipotea.
Pia bajeti hii imeondoa
kodi ya ongezeko la Thamani (VAT) kwenye
malighafi za pamba na hivyo kumpa manufaa mkulima wa pamba. Hata hivyo bajeti
hii imefanya punguzo la kodi kwenye umeme, mafuta mazito, ving’amuzi, machinga
na saruji na hivyo kutoa fursa kwa Watanzania wengi kuweza kujenga nyumba na
kuondokana na nyumba za nyasi na matope.
Halikadhalika serikali
imehaidi katika bajeti hii kudhibiti kazi za wasanii kwa kuweka stika katika
bidhaa za kazi zao. Hali hii itamsaidia Msanii kuweza kunufaika na jasho lake.
Si hayo tu, pia
serikali imewatangazia neema Wafanyakazi wote nchini juu ya upandaji wa
mishahara yao na pia utaratibu wa makato umerekebisha ambapo makato ya P.A.Y.E
yatawahusu wale wenye mishahara ya kuanzia 170,000 tofauti na hali ilivyokuwa
ambapo walikuwa wanakatwa kuanzia 130,000. Hizi ni neema kwa Wafanyakazi.
Serikali pia imehaidi
kufuta misahama mingi ya kodi iliyokuwa inatolewa kwa watu, taasisi na
viongozi. Hali hiyo itasaidia kuimarisha vyanzo vyetu vya ndani kimapato.
Ndugu zangu, nimeamua
kuyaelezea baadhi tu ya mazuri ya bajeti hii, endapo serikali itakuwa
utekelezaji wake, tupate pa kuanzia na kuwabana kwa kile walichohaidi.
Post a Comment