KWA takribani muda wa
juma moja sasa kumekuwepo na taarifa katika vyombo vya habari na njia mbalimbali
za upashanaji habari, kuwa kampuni moja ya meli inayodaiwa kutoka Iran,
inayojulikana kwa jina la NITC (National Iranian Tanker Company), inatumia
bendera ya Tanzania, isivyo kihalali na kinyume kabisa na sheria za nchi na zile
za kimataifa, kwa malengo ambayo hayajulikani.
Pamoja na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kutoa taarifa kwenye Baraza la Wawakilishi tarehe 2 Julai
2012 kukanusha taarifa hizo, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kinaitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia
kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Waziri wa Uchukuzi kutoa taarifa kwa umma juu ya
hatua ilizochukua kuchunguza madai hayo.
Aidha, Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ieleze iwapo utaratibu huo umezingatia kwa
ukamilifu United Nations Convention law of the Sea, kifungu cha 91, Geneva
Convention of Registration kifungu cha 6 na maazimio mengine ya kimataifa kuhusu
usajili wa meli kubwa pamoja na usafirishaji wa mafuta.
Maelezo yaliyotolewa na
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar inayoongozwa na CCM na CUF yanaibua
maswali kutokana na
kampuni ya Philtex ya Dubai inayoelezwa kupewa uwakala na Mamlaka ya Usafiri wa
Baharini- Zanzibar Maritime Authority (ZMA) kufanya kazi na makampuni mengine
hivyo taarifa hizo hazijitoshelezi katika kuondoa uwezekano kwamba meli za NITC
zilipeperusha bendera ya Tanzania.
Ili kujisafisha juu ya
tuhuma hizo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilipaswa kushirikiana na Serikali ya
Muungano kufanya uchunguzi wa kubaini msingi wa tuhuma hizo na kuchukua hatua
iwapo meli za NITC zilipeperusha bendera ya Tanzania bila ridhaa ya
serikali zote mbili.
Ikumbukwe kwamba hii si
mara ya kwanza kwa baadhi ya maofisa wa ZMA kutuhumiwa kuruhusu vitendo vilivyo
kinyume na sheria kama ilivyojitokeza wakati wa kashfa ya kuzama kwa meli ya
Spice Islender.
Kwa upande mwingine,
Serikali ya Muungano nayo haiwezi kukwepa kuwajibika kwa kuzingatia kuwa kuwa
baadhi ya taarifa hizo katika vyombo vya habari vimewanukuu mawaziri wa serikali
wakionekana kujikanyanga na kujikanganya juu ya suala hili nyeti la bendera ya
taifa, ambayo ni moja ya utambulisho wetu rasmi kama Watanzania, kutumika kwa
malengo yasiyojulikana na kampuni ya nje.
Moja ya vyombo vya habari
hapa nchini, vimewanukuu mawaziri husika, Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe
na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe, juu ya suala
hilo.
Wakati Waziri Mwakyembe
amenukuliwa akisema kuwa anazo taarifa za suala hilo, lakini asingeweza
kulitolea kauli mpaka Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wa Tanzania Zanzibar
azungumze, Waziri Membe yeye mbali ya kukiri kuwa kitendo hicho ni kosa
kisheria, anasema habari hizo zilikuwa za kushtushwa na ngeni kabisa, huku
akisema kuwa vyombo husika vitalichunguza kwa makini.
Ukimya wa serikali yetu
ambayo kwa hakika unatokana na udhaifu wake katika kuchukua maamuzi, sasa
umesababisha kitendo hicho kutafsiriwa kuwa Tanzania inaibeba na kuisaidia Iran
kukwepa vikwazo ambavyo nchi hiyo inatishiwa na mataifa ya Magharibi, hasa
Marekani na Umoja wa Ulaya, kutokana na malumbano ya muda mrefu ambayo
yanatokana na mataifa hayo kutumia mabavu na vitisho kuzichagulia baadhi ya nchi
nyingine duniani, nini cha kufanya na rasilimali zake mathalani mzozo
unaoendelea na Iran kuhusu urutubishaji wa madini ya urani.
Si nia ya CHADEMA kuingia
katika mgogoro wa Iran na Mataifa ya Magharibi hapa kupitia mjadala wa madai
hayo yaliyoandikwa kwenye vyombo vya habari; lakini CHADEMA kinatoa tamko
kufuatia ukimya na kigugumizi kinachoikumba Serikali ya CCM, kila inapohitajika
kufanya maamuzi ya haraka, hasa kuwalinda watu wake na hadhi ya utaifa wao na
nchi yao ndani na nje ya nchi.
Ni kutokana na udhaifu wa
serikali hii, ambayo umekuwa ukijidhihirisha pia kwa kushindwa kupanga bajeti
inayojitegemea hasa kwa kutumia utajiri mkubwa wa rasilimali ambazo nchi hii
imebarikiwa, hali inayotufanya tuonekane taifa ombaomba na kupoteza heshima
mbele ya mataifa makubwa na madogo, kuwa hatuna uwezo wa akili kuweza
kujitegemea.
Utegemezi huu umefanya
baadhi ya raia wa Nchi nyingine mathalani Mbunge aitwaye Howard Berman wa Bunge
la Marekani, akiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Nje, kupata uwezo wa
kuandika barua ya dharau na kejeli kwa Rais Jakaya Kikwete, juu ya suala hilo la
Meli za NIT kutuhumiwa kupeperusha bendera za Tanzania.
Kupitia tamko hili,
CHADEMA tunaitaka serikali kutoa kauli madhubuti juu ya suala hilo ambalo tayari
limechukua sura ya mjadala wa kimataifa usiokuwa na tija yoyote kwa mustakabali
wa Watanzania. Suala la bendera ambayo ni utambulisho wa taifa letu, haliwezi
kuwa suala la mchezo tu, ambapo mawaziri wazima hawawezi kutoa kauli za kina na
kuchukua hatua zinazostahili.
Imetolewa tarehe 2 Julai
2012 na:
Hamad Mussa
Yussuf
Naibu Katibu Mkuu
Zanzibar
Post a Comment