KLABU ya Azam FC leo inacheza fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya mabingwa mara nne, Yanga SC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Azam inakuwa
klabu ya pili kihistoria, nje ya Simba na Yanga kucheza fainali ya michuano
hiyo, baada ya Moro United mwaka 2006, ambayo ilifungwa 2-1 na Polisi Uganda,
Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam mbele ya rais Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa
anakimbiza mwaka wake wa kwanza tangu aingie Ikulu.
Hii timu
ambayo inakimbiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004 na ipo kwenye mwaka
wa tano tangu ianze kucheza Ligi Kuu mwaka 2008.
Kocha
Muingereza, Stewart Hall wa Azam FC iliyoitoa AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC) ili kuingia fainali, kwa kuifunga mabao 2-1, mabao yake
yakifungwa na John Bocco ‘Adebayor’ na Mrisho Ngassa, anasema kwamba Yanga ni
timu nzuri na fainali hiyo itakuwa ‘classic’, yaani baab kubwa.
Katika miaka
yake mitano ya kucheza Ligi Kuu, nuru ilianza kumulika kwenye anga zao mapema
mwaka huu walipotwaa Kombe la Mapinduzi na baadaye Aprili, wakakata tiketi ya
kucheza Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, wakiwapiku vigogo,
Yanga.
Katika dunia
ya leo, ambayo napokea mageuzi kisoka, hususan barani Afrika, timu kama Berekum
Chelsea ya Ghana ikisumbua katika Ligi ya Mabingwa, kuna dalili za kutosha Azam
inaelekea huko.
Azam FC,
kama ilivyokuwa kwa Mtibwa Sugar, nayo ilianzishwa na kikundi cha wafanyakazi wa
kampuni ya Mzizima Flour Mill, kampuni tanzu ya Bakhresa, makao yake makuu
yakiwa Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam.
Lengo la
wafanyakazi hao wa kampuni inayomilikiwa na Said Salim Bakhresa, awali ilikuwa
ni kucheza kwa ajili ya kujiburudisha, baada ya kazi.
Lakini baada
ya kuona wana timu nzuri, Oktoba 16, mwaka 2004, waliisajili rasmi kwa ajili ya
kushiriki Ligi Daraja la Nne, wakitumia jina la Mzizima FC.
Baadaye
Mkurugenzi Mkuu wa makampuni ya Bakhresa, Abubakar Bakhresa, aliona ni vyema
timu hiyo ihusishe wafanyakazi wa kampuni zote za Bakhresa, na kutumia jina la
moja ya bidhaa zao kubwa, Azam.
Kampuni
nyingine za Bakhresa ni Food Products Ltd, Azam Bakeries Ltd, Omar Packaging
Industries Ltd na kadhalika.
Wazo lake
lilikubaliwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo, ndipo timu hiyo ikaanza kuitwa Azam
SC, badala ya Mzizima. Lakini baadaye Juni 11, mwaka 2007, ilibadilishwa jina
tena na kuwa Azam FC.
Azam
ilikwenda kwa kasi nzuri kuanzia Daraja la Nne na hadi mwaka 2008, ilifanikiwa
kucheza Ligi Kuu, ikipandishwa na makocha King, aliyekuwa akisaidiwa na Habib
Kondo. Baada ya kupanda, Azam ilimuajiri kocha wa zamani wa Simba SC, Mbrazil
Neider dos Santos, aliyekuwa akisaidiwa na Sylvester Marsh na Juma Pondamali
upande wa kuwanoa makipa.
Baadaye
ilimuongeza kocha wa viungo, Itamar Amorin kutoka Brazil pia, ambaye awali ya
hapo alikuwa msaidizi wa Marcio Maximo katika timu ya taifa ya Tanzania, Taifa
Stars.
Ilisajili
pia wachezaji nyota, wazoefu, wakiwamo kutoka nje ya Tanzania, ambao
walichanganywa na chipukizi wachache walioipandisha timu hiyo, kama John Bocco
‘Adebayor’.
Wakati Azam
inapigana kwenye Ligi Daraja la kwanza ili kupanda Ligi Kuu, kikosini ilikuwa
ina wakongwe kama Shekhan Rashid na Suleiman Matola, viungo wa zamani wa klabu
ya Simba.
Malengo
makuu ya Azam ni kuifanya timu iwe ya kulipwa, wachezaji wakihudumiwa vizuri,
chini ya makocha bora, nao waweze kufanya vizuri na kuitangaza kimataifa timu
hiyo na soka ya Tanzania kwa ujumla.
Aidha, kwa
kuwa inataka kutambulika kimataifa, ina kitengo maalumu cha soka ya vijana,
kilicholenga kuibua vipaji vya chipukizi wa soka na kuwakuza katika misingi na
maadili ya mchezo wenyewe, ili baadaye wauzwe Ulaya.
Mmoja kati
ya mabosi wa Azam, Yussuf Bakhresa, ni wakala wa wachezaji anayetambuliwa na
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambaye anaweza kuwafanya yosso wa klabu
hiyo waende Ulaya moja kwa moja.
Kikosi cha
kwanza cha Azam Ligi Kuu kilikuwa kinaundwa na wafuatao; Kassim Kilungo, Said
Bakar Nachikongo, Abdul Azizi Hamza, Shaaban Abdallah Kisiga ‘Malone’, Ally
Suleiman Alawy, John Raphael Bocco ‘Adebayor’, Salum Machaku, Shekan Rashid
Abdallah, Jamal Simba Mnyate, Yussuf Juma Gogo, Zuberi Ubwa, Yahaya Said Tumbo,
Said Khamis Sued, Salum Abubakar Salum, Luckson Jonathan Kakolaki, Adam Shomari
Ngido, Abdulhalim Chilumbe, Ngoy-Pichou Botwetwe, Mussa Khalid Kipao, Iddi
Abubakar Mwinchumu, John Faustin Mabula, James Adriano Kilongola, Malika Philipo
Ndeule, Paulo John Nyangwe, Abubakar Pawasa na Vladimir Niyonkuru.
Azam pamoja
na kumilikiwa na kampuni ya bilionea, zaidi ya basi lake ‘kali’, haina uwanja
wake, Azam Complex, uliopo Chamazi, Mbagala, Dar es Salaam, ambao kwa msimu huu
imeshuhudiwa hadi vigogo, Simba na Yanga wakiutumia kwa mechi zao za Ligi
Kuu.
Kwa sasa
Kocha Mkuu wa Azam, Muingereza Stewart Hal. Naam, hao ndiyo Azam FC, wana Lamba
Lamba.
Hivi
karibuni, Azam watafanya ziara ya kujiandaa na msimu mpya Falme za Kiarabu na
inawezekana wakaondoka baada tu ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na
Kati, Kombe la Kagame inayofikia tamati leo mjini Dar es Salaam.
Malengo ya
Azam ni kutwaa Kombe la Kagame leo na kuhakikisha mwakani wanacheza hatua ya
makundi ya Kombe la Shirikisho- pamoja na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara.
Hao ndio Azam, wanaoelekea anga za Berekum Chelsea ya Ghana. "
HII NDIO YANGA
Kikosi cha Yanga msimu uliopita |
Na
Mahmoud Zubeiry
MICHUANO ya
Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame inatarajiwa kufikia
tamati leo kwa fainali itakayowakutanisha mabingwa watetezi, Yanga na Azam FC ya
Dar es Salaam, Uwanja wa Taifa.
Yanga
wanaodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, wanaingia kwenye mechi hiyo wakiwa
na matumaini makubwa ya kutetea taji lao, baada ya kuonyesha soka ya kuvutia
katika mechi mbili zilizopita, wachezaji wake wakicheza kwa ari na kujituma
chini ya kocha mpya kutoka Ubelgiji, Thom Saintfiet.
Yanga
ilikaribishwa kwenye michuano ya mwaka huu na kipigo cha 2-0 kutoka kwa Atletico
ya Burundi katika Kundi C, kabla ya kushinda 7-1 dhidi ya Waw Salaam ya Sudan
Kusini, na 2-0 dhidi ya APR ya Rwanda, ilishinda kwa penalti 5-3 dhidi ya
Mafunzo katika Robo Fainali, kufuatia sare ya 1-1 na ikashinda 1-0 dhidi ya APR
katika Nusu Fainali ndani ya dakika 120.
Michuano
hii, imemuibua kinara mpya wa mabao Yanga, Said Bahanuzi ‘Spider Man’, ambaye
katika mabao 11 iliyofunga Yanga hadi sasa kwenye michuano ya mwaka huu, yeye
amefunga matano, mengine matano Hamisi Kiiza ‘Diego’ na lingine moja Nizar
Khalfan,
Washambuliaji
hawa wawili, Kiiza na Bahanuzi kwa ‘njaa yao ya mabao’ wanatarajiwa kuwa chachu
ya ubingwa kwa Yanga leo.
SIRI
YA JEURI YA YANGA
Yanga
inajivunia udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake,
Kilimanjaro Premeum Lager, ambao ni wa kwanza tangu wapoteze udhamini wa kampuni
ya Shivacom.
Ikumbukwe,
Kilimanjaro Premium Lager ilianza kuidhamini Yanga Agosti 18, mwaka 2008, katika
mkataba uliosainiwa kwenye hoteli ya Movenpick (sasa Serena), mjini Dar es
Salaam.
Kilimanjaro
Premium Lager, ambao ni wadhamini wakuu wa wapinzani wa jadi wa Yanga, Simba SC,
imekuwa ikihakikisha udhamini wake unafika maeneo yote muhimu katika shughuli za
uendeshwaji wa klabu.
Na
inaaminika udhamini huo ndiyo chachu ya mafanikio ya miaka ya kmaribuni ya klabu
hiyo, ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu katika kipindi cha miaka
mitano (2008, 2009 na 2011) sambamba na ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati,
Kombe la Kagame mwaka jana.
ILIVYOTWAA
KOMBE MWAKA JANA:
Yanga
ilifanikiwa kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama
Kombe la Kagame, baada ya kuifunga Simba bao 1-0, katika Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Shukrani
kwake mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana, Kenneth Asamoah aliyefunga bao hilo,
pekee dakika ya 108, akiunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa kitaalamu na
kiungo Rashid Gumbo.
Kabla ya
taji hilo walilotwaa Jumapili sambamba na dola za Kimarekani 30, 000, sawa na
Sh. Milioni 45 za Tanzania, Yanga walitwaa tena Kombe hilo kwa mara ya kwanza
mwaka 1975 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, wakiifunga Simba mabao 2-0 na
baadaye mara mbili mjini Kampala, Uganda mwaka 1993 na 1999, mara zote
wakiifunga SC Villa ya huko.
Ulikuwa
mchezo mgumu ambao ulidumu kwa dakika 120, timu zikionyesha kucheza tahadhari,
kabla ya Asamoah kumaliza kazi.
Kikosi
kilichoipa Yanga kombe la nne la Kagame kilikuwa; Yaw Berko, Nsajigwa Shadrack,
Oscar Joshua, Chacha Marwa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’/Rashid
Gumbo, Godfrey Taita/Julius Mrope, Nurdin Bakari, Davies Mwape, Jerry
Tegete/Kenneth Asamoah na Hamisi Kiiza.
Yanga
iliyokuwa Kundi B la michuano ya mwaka huu, ilifuzu kama kinara wa kundi baada
ya kujikusanyia pointi saba kutokana na kushinda mechi mbili na kutoka sare
moja.
Katika Robo
Fainali, Yanga ilikutana na Red Sea ya Eritrea na kushinda kwa penalti 6-5,
kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 za mchezo
huo.
Katika Nusu
Fainali, Yanga ilikutana na St George ya Ethiopia na kushinda tena kwa penalti
5-4, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120, kabla ya kuiteketeza
Simba SC katika fainali.
Ikumbukwe
katika michuano ya mwaka huu, Yanga iliingia kama ‘viti maalumu’, kwani Simba SC
ndio walikuwa wawakilishi halisi kama mabingwa wa Bara.
Ili
kushiriki mashindano ya mwaka huu, ilibidi Yanga wailipe CECAFA dola za
Kimarekani 20,000 kama faini ya kugomea mechi ya mshindi wa tatu wa michuano
hiyo, mwaka 2008 mjini Dar es Salaam.
Yanga
ilitakiwa kucheza na Simba mwaka huo kuwania nafasi ya tatu, ikiwa chini ya
Mwenyekiti aliyekuwa na misimamo mikali, Wakili Imani Omar Madega, Yanga iligoma
kwa sababu hawakukubaliana na TFF juu ya mgawanyo wa mapato ya milangoni.
ZANZIBAR
MWAKA 1975:
Iliingia
kama bingwa wa Tanzania baada ya kuifunga Simba SC katika fainali ya Ligi mwaka
1974 Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, wakati watani wao hao waliingia kama mabingwa
watetezi wa michuano.
Yanga
ilipangwa Kundi B pamoja na Express ya Uganda na Mufulira Wanderers ya Zambia.
Yanga ilianza kwa kuifunga Express FC mabao 4-0 na baadaye kutoka sare ya 1-1 na
Mufulira, hivyo kuongoza Kundi hilo na kukata tiketi ya kuingia Nusu
Fainali.
Katika Nusu
Fainali, Yanga iliifunga Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 na kukata tiketi ya
kuingia fainali Janauri 13, mwaka huo ilipokutana na watani wao wa jadi, Simba
SC.
Mabao ya
Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) yaliipa Yanga ushindi
wa 2-0 na taji la kwanza la michuano hiyo.
KAMPALA,
UGANDA MWAKA 1993:
Ilikwenda
kama bingwa wa Bara na watano wao, Simba walikwenda kama watetezi wa taji na
huko Yanga walipangwa Kundi A pamoja na wenyeji SC Villa na Malindi ya
Zanzibar.
Katika
mchezo wa kwanza, Yanga ilifungwa 3-1 na Villa, siku hiyo kabla ya kuibuka na
kuifunga Malindi mabao 2-1, yote yakitiwa kimiani na Said Nassor Mwamba
‘Kizota’, sasa marehemu, hivyo kukata tiketi ya kuingia Nusu
Fainali.
Katika Nusu
Fainali, Yanga ilikutana na Express FC na kushinda mabao 3-1, hivyo kutinga
fainali ambako ilikutana tena na SC Villa.
Kwa
kuzingatia matokeo ya mchezo wa awali kwenye Kundi A, Yanga haikupewa nafasi
kabisa ya kufurukuta mbele ya SC Villa, lakini mambo yalikuwa tofauti, mabao ya
Said Mwamba na Edibily Lunyamila, yaliipa timu hiyo ushindi wa 2-1 pamoja na
taji la pili la michuano hiyo.
Marehemu
Kizota aliibuka mfungaji bora wa michuano hiyo.
KAMPALA,
UGANDA MWAKA 1999:
Ilikwenda
kama bingwa wa Bara, ikiwa mwakilishi pekee na ilitua huko, huku mashabiki wengi
wa soka Uganda wakiwa na kumbukumbu ya kile kilichofanywa na klabu hiyo mwaka
1993.
Timu
zilizoshiriki michuano hiyo ni Vital'O ya Burundi, Mebrat Hail ya Ethiopia, AFC
Leopards ya Kenya, Kiyovu Sport, Rayon Sport za Rwanda,
Naadiga
Dekedaha ya Somalia, KMKM ya Zanzibar, Al Hilal ya Sudan, Yanga, wenyeji
Express na SC Villa za Uganda wakati Red Sea ya Eritrea ilijitoa dakika za
mwishoni.
Kwa matokeo
hayo, Kundi D ilimokuwa Yanga lilibakiwa na timu mbili tu, yaani mabingwa hao wa
Bara na mabingwa watetezi.
Mechi ya
kwanza, Yanga ilifungwa 3-0 na Rayon Januari 4 na ziliporudiana siku mbili
baadaye, Yanga walilipa kisasi kwa ushindi wa 3-0 pia, mabao
ya
Sekilojo
Chambua dakika ya 23 na 57 na Kali Ongala dakika ya 59.
Katika Robo
Fanali, Yanga ilikutana na Al Hilal Januari 10 na kushinda mabao 2-1, wafungaji
Salvatory Edward dakika ya 14 na Edibily Lunyamila dakika ya 89 kwa
penalti.
Katika Nusu
Fainali, Yanga ilikutana na Vital’O ya Burundi Januari 13 na kushinda mabao 3-2,
wafungaji Kally Ongara dakika ya 16, Bakari Malima dakika ya 78 na Said Mhando
dakika ya 90.
Hivyo kwa
mara ya pili, Yanga ilikutana na SC Villa kwenye fainali kukumbushia vitu vya
mwaka 1993 na safari hii mambo yalikuwa mazito zaidi, kwani dakika 120
zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1 Lunyamila akiisawazishia Yanga
dakika ya 42, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kufunga dakika ya saba tu ya
mchezo huo.
Mchezo
ukahamia kwenye mikwaju ya penalti na Manyika Peter akaingia kwenye orodha ya
makipa hodari wa kupangua penalti baada ya kupangua mikwaju miwili, Yanga
ikishinda kwa penalti 4-1, Uwanja wa Nakivubo.
Hivyo ndivyo
Yanga ilivyotwaa mataji yake manne ya Kombe la Kagame- na leo wanacheza fainali
ya pili mfululizo nyumbani dhidi ya Azam, wakijaribu kuifukuza rekodi ya watani
wao wa jadi, Simba SC waliotwaa taji hilo mara sita, je wataweza? Bila shaka
dakika 90, 120 au mikwaju ya penalti itatoa majibu leo.
Chanzo: Bin Zubeiry Blog
Post a Comment