HATIMAYE wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameibuka na kumsafisha Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, huku wakidai taarifa ya Kamati teule iliyokuwa ikiongozwa na Waziri wa sasa wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ilijaa upotoshaji.
Sakata hilo, lilibuka juzi usiku, katika kikao cha Wabunge wa CCM, ambacho kilikuwa kinajadili tatizo la umeme, hali iliyomfanya Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), kuibuka na na hoja ya kutaka viongozi wa wizara hiyo wawajibishwe.
Hoja ya Sendeka, ilimlenga Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi, wawajibishwe kwa kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho, kilisema kuwa hoja hiyo ya Ole Sendeka, ilionekana ni mwiba kwake, hali iliyomfanya Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), kunyanyuka na kumuumbua ole Sendeka.
Lugola, alisema alifuatwa na Ole Sendeka, huku akiahidi kumhonga fedha ili aweze kumuunga mkono hoja yake ya kutaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliachim Maswi, wawajibishwe na Bunge.
“Hoja ya Ole Sendeka, ilimfanya Kangi Lugola kunyanyuka na kuanza kutoa maelezo ambayo kulikuwa na lengo la kutaka kukwamisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini. Alipinga wazi kuwawajibisha viongozi wa wizara hiyo, huku akifananisha kinachotaka kufanywa ni sawa na lililomtokea Lowasa.
“Alisema katika ripoti ile ya kamati teule ya Bunge, ilipelekea kumwajibisha Lowassa na baada ya muda iligundulika ilijaa upotoshaji mwingi na kusisitiza katu wabunge hawapo tayari kurudia makosa ya mwaka 2008, ambapo vilitolewa vielelezo vya mitaani,” alisema mtoa habari huyo.
Baada ya maelezo ya Lugola, naye Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango (CCM), aliunga mkono hoja hiyo na kusema kuwa mwaka 2008, Bunge liliaminishwa Lowassa, alikuwa mhusika na Richmond, kutokana na jambo hilo kukosa ushahidi alitahadharisha kutorudiwa kwa makosa tena.
“Kilango, alisema wabunge waliamini alikula fedha kwa kulipwa na Richmond, lakini hakuna ukweli, hivyo hakuna sababu ya kumwajibisha Waziri wa Nishati wala Katibu Mkuu wake.
“Baada ya hapo aliinuka Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy Mohammed (CCM), ambaye alisema katu hayuko tayari kuunga mkono hoja ya Ole Sendeka, kwani tangu alipondolewa Lowasa katika nafasi ya uwaziri mkuu nchi imekuwa ikiyumba.
“Mjadala ulikuwa mkali ndugu yangu, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alisema wabunge hawako tayari kurudia makosa ya Richmond, hatakuwa tayari kuubariki mpango huo aliouita mchafu,” kilisema chanzo hicho.
Awali kabla ya kikao hicho, Kamati ya Nishati na Madini iliamua kuunda tume maalum ya kumchunguza Maswi kwa tuhuma za kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Maswi, anadaiwa kukiuka sheria hiyo, wakati akitoa zabuni ya ununuzi wa mafuta ya kuzalisha umeme wa dharura katika Kampuni ya Puma, ambayo ilipewa vibali vya kuiuzia Serikali lita milioni 9 mwaka 2011 na lita nyingine kama hizo mwaka huu.
Habari za kuaminika zilizopatikana jana kutoka mkoani Dodoma zinasema, hatua ya kuundwa kamati ndogo imetokana na kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kikiwa na nia moja tu ya kumaliza mpasuko uliopo.
“Kikao cha Waziri Mkuu na wabunge wa CCM, kilikumbwa na mambo mengi mno, mojawapo ni kutaka kuona Maswi anawajibishwa haraka iwezekanavyo.
“Lakini hoja hiyo, ilionekana kupingwa na Waziri Mkuu na baadaye alikubali iundwe kamati ndogo ya kumchunguza Maswi na maazimio yote yatakayowasilishwa serikalini au bungeni, yatafanyiwa kazi mara moja,
“Nakwambia kauli ya Pinda, ilionekana wazi kupoza machungu ya wabunge, yeye alionekana kuwa muwazi kwa kuwaahidi kuwa kila pendekezo dhidi ya Maswi, litafanyiwa kazi barabara.
“Unajua Kamati ya Nishati na Madini haijafurahishwa kabisa na mwenendo uliopo pale kwa Maswi, inaonekana kuna mambo yanakwenda shaghala baghala tu.”
Habari za uhakika ambazo MTANZANIA ilizipata kutoka ndani ya kikao hicho, zinasema Pinda alikiri waziwazi kuwa Maswi ameteleza katika uamuzi wake aliochukua.
“Katika kuonyesha kwamba hakuridhika na hali hiyo, Pinda alikiri kuwa Maswi amefanya makosa kwa sababu wakati anaunda tume kufanya uchunguzi pale TANESCO, Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), haikujulishwa.
“Hata CAG alimwambia Pinda kwamba ripoti yoyote kuhusu TANESCO, ikipelekwa kwake hataitambua na anashangaa mno kutohusishwa kwenye uchunguzi huo.
“Kulikuwa na mvutano mkubwa mno, pale Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM) aliposimama na kutoa msimamo wake.
“Yeye hakutaka kuficha au kumung’unya maneno, alitamka waziwazi na kusema alishiriki na kusimamia suala la Kampuni ya Richmond na hatimaye Waziri Mkuu aliyekuwepo aliwajibika, licha ya kutohusika moja kwa moja na sakata lile, lazima Maswi naye afuate mkondo huo.
“Lakini ghafla, Sendeka aligeuka na kuwataka wabunge wasishikie bango zaidi, baada ya kutaka Bunge liunde kamati teule ya kumchunguza Maswi.
“Sikubaliani na hoja eti Maswi ameokoa fedha za umma zaidi ya Sh bilioni 3 kwa maslahi ya nchi, hoja yangu ni kwamba wakati tenda inatangazwa PUMA waliomba kwa bei kubwa tofauti na makampuni mengine…Maswi alipaswa kuwaita wasambazaji wengine awataarifu na kuwaangalia sheria inayompa mamlaka inasemaje, sambamba na Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA),” kilisema chanzo chetu.
Habari zinasema baada ya mnyukano huo, Maswi naye aliamua kufunga na kuwarushia vijembe wabunge.
“Eeeh kaka Maswi aliwatupia lawama wabunge kwamba si waadilifu, wapo ambao wamekuwa wakipokea rushwa, pamoja na maneno yake makali kwa wabunge, Maswi alikiri kuvunja utaratibu kwa maslahi ya taifa,” kilisema chanzo chetu.
Source: Mtanzania
Post a Comment