Kituo
cha Umeme wa gesi asili wa megawati 105.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akipata maelezo kutoka kwa
Meneja wa Kituo cha Umeme wa gasi asili wa megawati 105, John Mageni wakati wa
hafla uya uzinduzi wa kituo hicho uliofanyika Ubungo jijini Dar es Salaam
jana
Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo,akiendelea kupata maelezo kutoka kwa Meneja wa Kituo
cha Umeme wa gasi asili wa megawati 105, John Mageni
Picha Zote na Mdau Dande Francis
--
DAR ES
SALAAM,Tanzania
SHIRIKA la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), limefungua rasmi kituo cha kufua umeme wa gesi asilia wa megawati 105 eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam Jana.Akizungumza katika ufunguzi huo jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema kituo hicho ni mali ya serikali ambacho kimegharimu dola za Marekani 124,895,988 huku akiishukuru Serikali ya Norway waliodhamini upatikanaji wa mkopo huo.
Prof. Muhongo alisema hiyo ni dalili tosha
kwamba wamedhamiria kubadili mtindo wa upatikanaji wa umeme kutoka chanzo
kikubwa kimoja cha umeme wa maji ambao kwa sasa unazalisha MW 561 ya umeme
wote.Alisema kufuatia uzinduzi huo, mitambo yote ya gesi iliyopo Mkoa wa Dar es
Salaam na Mtwara itazalisha umeme wa jumla ya MW 1375 huku akieleza takwimu hizi
zinaonesha ni jinsi gani serikali inavyojitahidi kupunguza utegemezi wa umeme wa
maji.
Alisema hadi kufikia jana Tanzania imegundua gesi asili ya jumla ya futi za ujazo trilioni 26.99 sawa na mapipa ya mafuta bilioni 4.86 huku akiahidi kuwa utafutaji huo wa gesi unaendelea.
“Iwapo tutatumia gesi iliyohakikiwa hadi leo
hii ya wingi wa futi za ujazo trilioni 1.142 kwenye mitambo yetu yote inayofua
umeme wa gesi kwa kutumia futi 150 kwa siku, gesi hiyo iliyohakikiwa tutaitumia
kwa muda wa miaka miwili ijayo,” alisema Muhongo.
Alisema serikali inatayarisha sera ya gesi kwa
kutumia wataalamu Watanzania ambayo itajadiliwa na wadau wengi wakiwamo wenyeji
wa Mtarwa na Lindi ili kuwezesha kuwa na msingi mzuri wa maandalizi ya muswada
wa gesi na kanuni zake kwa manufaa ya nchi.
Prof. Muhongo aliongeza kuwa mbali ya gesi
serikali pia imeamua kutumia makaa ya mawe kuzalisha umeme na ifikapo mwaka
2015/2016 umeme utaanza kutokana na makaa hayo yenye wingi usiokuwa chini ya MW
200.
Alisema serikali pia imeamua kutumia vyanzo
vingine vya kupata umeme wa uhakika kutoka kwenye upepo, jua na jotoardhi
jitihada zote ni kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana ili kutimiza
malengo ya maendeleo ambapo hadi kufikia mwaka 2025 nchi iwe ni miongoni mwa
zenye kipato cha kati cha dola za Marekani 3,700-12,000.
“Ili kuwepo na maendeleo, tunahitaji umeme wa uhakika, tunahitaji taifa lenye kipato cha kati kuwepo na MW 3000-5000, tuige mfano wa Kenya ambapo kwa sasa wenzetu wamepiga hatua ikiwa umeme wa upepo wanazalisha MW 1,000,” alisema Muhongo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Injinia
William Mhando, alisema kuwa hawatarudi nyuma kutokana na kupata fundisho katika
athari kubwa za ukosefu wa umeme iliyotokea mwaka 2010 hadi
2011.
Alisema kuhakikisha uzinduzi wa kituo hicho unafikiwa ni jitihada kubwa zilizofanyika bega kwa bega na mhandisi mshauri kutoka nchini Norway na Ujerumani.
Alisema
kituo hicho cha Ubungo kina mitambo mitatu ambayo kila mmoja unazalisha MW 35
kila mmoja na kufanya kufikia MW 105, iliyoingizwa katika gridi ya
taifa.
Post a Comment