Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

SAKATA LA WABUNGE WALA RUSHWA LAZIDI KUSHIKA KASI

* WABUNGE WATOA ANGALIZO

* MBATIA AICHOKONOA KAMATI YA NGWILIZI

* CUF YALAANI


Baadhi ya wabunge waliokuwa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika wa Bunge Anne Makinda, mwishoni mwa wiki kwa tuhuma za kuhongwa, wametaka kuundwa kwa kamati teule ya Bunge kuchunguza tuhuma mbalimbali.

Baadhi ya wajumbe wamesema siyo haki kuihukumu kamati nzima kwa madai ya rushwa kwa kuwa hakuna mahali popote panapothibitisha kuwa kamati imedai rushwa.

Wamesema ili kutenda haki kwa wajumbe wengine, kuna umuhimu wa kuwataja kwa majina wabunge wa kamati hiyo wanaodai rushwa.

Wanmeongeza kwamba katika mazingira kama hayo kwa nini Bunge lisiunde kamati teule kuchunguza mambo yote, aliyehongwa kufanya biashara na Tanesco au kama Katibu Mkuu wa wizara, Eliakim Maswi, alikiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma wakati wa mchakato wa kuipa zabuni kampuni ya Puma kuiuzia serikali mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura.

Wabunge hao wamesema kuundwa kwa kamati teule pia kungeweza kusaidia kuwabaini wenye makosa na kuwasafisha wengine.

Tuna taarifa kama gazeti kuwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walipokutana wiki iliyopita chini ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, walikubaliana kwamba iundwe kamati ndogo ya wajumbe wa makati iliyovunjwa kutoka CCM kuchunguza sakata ya zabuni kwa Puma.

Katika mazingira kama hayo, haionyeshi kama ukweli unaweza kubainika kwa kuchukua wabunge wa chama kimoja kuchunguza suala nyeti kama hilo bali kamati teule ya wabunge kutoka vyama vyote ndiyo inayoweza kuchunguza tuhuma hizo kwa kwa na uhuru na kupata ukweli.

Hata hivyo, baadhi ya mapendekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na kamati hiyo kabla ya kuvunjwa ni kuundwa kwa kamati teule ya Bunge ambayo ingechunguza pamoja na mambo mengine, tuhuma zinazoelekezwa wizarani, ubadhirifu na hujuma katika Tanesco na baadhi ya wabunge kufanya biashara na Tanesco.

Habari za uhakika zinasema kuwa Kamati teule ilipomuita Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu Maswi, kuzungumzia nani anafanya biashara na Tanesco, hawakuthibitisha mbele ya kamati.

Kama gazeti hatuungi mkono upande wowote kati ya wanaotuhumu na wanaotuhumiwa, lakini katika mazingira kama haya, kuundwa kwa kamati huru teule kutasaidia kuweka kila kitu sawa kwa kuwa itakuja na ukweli na umma kuuelewa.

Spika Makinda ameivunja kamati hiyo kutokana na tuhuma kuwa baadhi ya wajumbe wake kuhongwa na makampuni ya mafuta nchini ili wamwajibishe Katibu Mkuu Maswi.

Pia, Spika ameipa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwachunguza wabunge hao na matokeo yake kurejeshwa bungeni.

Uamuzi huo wa Spika juzi ulifuatia Mbunge wa Namtumbo CCM, Vita Kawawa, kutaka kamati hiyo ivunjwe na suala la rushwa lipelekwe katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo CCM, Hassan Ngwilizi.

MBATIA: SPIKA AIMULIKE KAMATI YA NGWILIZI




Mbunge wa kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, amemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuisafisha Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kabla ya kuwapa kazi ya kuwachunguza wabunge wanaotuhumiwa kuhongwa katika sakata la ubadhirifu Tanesco.

Mbatia aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

“Kuna baadhi ya wajumbe wamehusishwa na vitendo vya rushwa katika kamati hii, haina usafi, kwanza itakaswe kabla ya kuanza uchunguzi wa jambo hili,” alisema.

Pia alimtaka Spika Makinda, kutumia maamuzi ya mabunge mengine duniani katika kulifanyia maamuzi suala hilo.

Alisema mabunge hayo yalichukua hatua za kuwafukuza wabunge waliobainika kuhongwa papo kwa papo bila kuchukua muda mrefu.

Alitoa mfano wa Bunge la Uingereza ambalo katika kipindi kati ya mwaka 1624 hadi kufikia mwaka 1926 lilitoa maazimio 56 na kutekelezwa bila kuchukua muda.

Alilitaja Bunge la India kuwa mwaka 2005 lilifukuza wabunge 11 ambao walithibitika walipewa fedha na wafanyabiashara ili watetee kwa manufaa ya maslahi yao.

Alisema hilo pia lilishawahi kutokea hapa nchini mwaka 2005 ambapo aliyekuwa Spika Samwel Sitta, aliwahi kuwapeleka mahakamani wabunge wanne waliofunga ndoa na raia wa Somalia ili wapate hati za kusafiria za kidiplomasia bila kuchukua muda mrefu.

Alisema Chama cha Wananchi (CUF) kiliwaondoa katika orodha ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi kwa kosa hilo na kuvitaka vyama ambavyo wabunge ambao wanatuhumiwa kuhongwa kuachia ngazi kabla ya kuumbuliwa.

“Natoa wito kwa wabunge wa chama changu, ambao wanajua kuwa walihusika kwa namna yoyote na rushwa, waachie ngazi kabla ya kuumbuliwa,” alisema Mbatia.

Alisema sheria inatamka wazi kuwa mbunge yeyote anayekamatwa rushwa kifungo chake ni zaidi ya miaka mitano jela.

Aidha, Mbatia alitaka Spika kuzivunja kamati ambazo alidai zinafikia sita zilizokosa uadilifu.

Naye Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, alimtaka Spika kuwataja wabunge waliohusishwa na rushwa ndani ya wiki moja la sivyo atapeleka hoja binafsi bungeni.




CUF YALAANI WANAOPOKEA RUSHWA
Chama cha Wananchi (CUF) kimelaani tabia ya baadhi ya wabunge ambao wanapokea rushwa kutoka kwa viongozi wakuu wa wizara kwa lengo la kuficha maovu yanayofanyika ndani ya wizara hizo.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro, alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa waandishi wa habari.

Mtatiro alidai kuwa kuna wabunge ambao walimfuata Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, awape fedha ili wasiibue vitendo vya ubadhirifu ndani ya wizara hiyo wakati wa mjadala wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/13 ambayo iliwasilishwa na kujadiliwa bungeni Ijumaa na Jumamosi wiki iliyopita.

Katibu huyo alilaani mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya wabunge kwa kupokea rushwa ya baadhi viongozi ili wasiumbue maovu yao kwa maslahi yao binafsi na kumiliki hisa katika miradi mbalimbali ikiwemo ya umeme.

Imeandikwa na Sharon Sauwa, Dodoma na Hadija Kitwana na Nuru Mfaume, Dar.

CHANZO: NIPASHE
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top