Na. Emmanuel
J. Shilatu
Mara baada
ya kufanikiwa kuziondoa tawala mbovu, nyonyaji na za kidhalimu za Wakoloni hapa
nchini, aliyekuwa akiongeza harakati hizo ambaye pia ni Baba wa Taifa letu
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema ya kuwa “tumefanikiwa kuwaondoa
wakoloni na hivyo tupo huru na Uhuru ni kazi”. Hapa Mwalimu Nyerere alikuwa na
maana ya kuwa ili tuweze kupiga hatua kimaendeleo ni lazima tuutumie huu uhuru
wetu vilivyo kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa yote ili kuleta maboresho
katika Nyanja zote za kimaisha yaani uchumi, kijamii na kisiasa.
Na ndio
maana yeye kama kiongozi alianza kuonyesha
mfano wa dhahiri kwa kuanzisha mapambano
kwa vitendo dhidi ya maadui zetu watatu ambao ni ujinga, maradhi, na umaskini.
Sehemu ya mafanikio yake ni kwa kupitia kuanzisha maazimio, mashirika, kauli
mbiu na sera mbalimbali. Hayo yoote (yaani tangu kusaka uhuru wa Tanganyika)
aliweza kufanikiwa kutokana na kufanya mambo kwa matendo zaidi kuliko maongezi
(porojo) zisizoisha.
Pia Mwalimu
Nyerere alikuwa na falsafa (dhana) ya kimaendeleo ambapo aliamini kuwa
maendeleo sahihi hayawezi yakapatikana nje ya uwepo wa mambo manne ambayo ni
“Watu”, “ardhi”, “siasa safi”
na “uongozi bora”
Ndio “Watu”
ni kiungo kimojawapo cha hakikisho la maendeleo chanya yeyote yale ndani ya
familia, jamii na Taifa kwa ujumla. Kama tutakuwa na miundombinu bora ni watu
wamechangia uwepo wake; kama tutakuwa na mazao ya kutosha kwa ajili ya chakula,
kiada na biashara ni watu ndio wamechangia hayo; Endapo kuna amani na utulivu
nchini basi ujue watu wamechangia hayo; ama taifa likiwa na wasomi wa kutosha
ni watu mbalimbali ndio wamechangia hilo.
Licha ya
kwamba Taifa letu Tanzania
lina watu zaidi ya Milioni 40 lakini hao watu wamekuwa ndio kikwazo kikubwa
katika uletaji wa maendeleo ya kweli na ya dhahiri. Tatizo lililopo ni uibukaji
wa umaskini mkubwa wa utegemezi na utajiri mkubwa wa porojo ndani ya jamii na
kila Mwana jamii ni mwathirika wa hili si Kijana wala Mzee awe ni Mwanamke au
Mwanaume.
Utakuta
vijana wengi kutwa wanashinda kwenye kucheza “pool table” na kukaa vijiweni tu;
Wazee ama akina Baba nao kutwa wanacheza “bao” ama “draft” tu; na akina Mama
nao kila kukicha wapo vibarazani wakisutana na kupashana umbea tu. Hayo ndio
maisha ya kila siku ya baadhi ya wanajamii ya kutokupenda kufanya kazi kwa
bidii.
Jamii
inachojua ni utegemezi pekee. Kivipi? Kwa jinsi tuanavyoishi utadhani
tunawangojea baadhi ya watu kutoka nje ili waje watuletee maendeleo yaani
imefika kipindi kwa mtu hata kutandika kitanda chake mwenyewe anacholalia
imekuwa ni kazi kuubwa kwake. Pia suala la maendeleo ya nchi yetu wenyewe
tumewaachia viongozi pekee huku tukijiengua katika kapu la dhana ya neno
“Serikali” wakati kiuhalisia na kikatiba pia ni kwamba Serikali inaundwa na
viongozi pamoja na Wananchi.
Hii yote
inatokana na jamii kuziasi mitazamo miongozo na falsafa za Mwalimu Nyerere
(mathalani ile ya “Uhuru ni kazi”) hali inayosababisha kiwango cha idadi ya
watu maskini kuzidi kukua nchini licha ya kujaariwa rasilimali na mali za asili
kwa kuyachakachua maendeleo yetu wenyewe. Kisa? Porojo kutawala maisha yetu.
Hali hii
tuliyonayo ya kutaka kuongea ongea ovyo huku parojo zikituendesha katika
masuala ya kimsingi ya maisha yetu, tunataka tuwaambukize hata na viongozi
wetu. Imefika kipindi kigezo ama kipimo cha uwezo wa Kiongozi unapimwa na
utokeaji wa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari ama uongeaji, uropokaji na
ubwatukaji wa mara kwa mara kwenye jumba letu tukufu la kutunga sheria na wala
si utendaji wake kazi na uletaji wa maendeleo katika jamii yaani ni usanii,
usanii mtupu. Hii ni hatari sana.
Hivi
tunachotaka kutoka kwa Kiongozi ni mazungumzo pekee ama matendo yake ya
kimaendeleo? Ama uwezo wa kiongozi bora upo kwenye mazungumzo tu ama
utakelezaji wa kimaemdeleo? Hivi uhodari wa mbunge wangu unatoka na amezungumza
mara ngapi Bungeni ama amenipunguziaje zigo langu la matatizo ya kimsingi? Bila
shaka majibu ni hapana ila ajabu ya firauni ni kuwa kwa miaka ya hivi karibuni kumeibuka
dhana mfu ya kupima uwezo wa Kiongozi si
kwa uletaji wa maendeleo bali ugwiji wake wa kuzungumza Bungeni kwa kuchangia
hoja kuulizwa maswali ya msingi na kadhalika.
Mtazamo huu unaonyesha kuwa kiongozi bora
anapimwa kwa uwezo wake wa kuongea Bungeni na si utetaji wa maendeleo; Pili,
wanawafundisha viongozi wetu tabia mbaya ya kuwa wawe ni wazungumzaji tu na si
watendaji; Tatu, inavyoonyesha hawaijali thamani ya maisha ya Mtanzania bali ya
Yule anayeiwasha vipaza sauti mara kwa mara pale mjengoni.
Katika kipindi fulani cha nyuma tafiti
mojawapo nchini walitoa matokeo yao ya utafiti ambapo waliueleza Umma kuwa Mh.
Edward Ngoyai Lowassa ndiye anayeongoza pale Bungeni kwa kutokuongea pale
Bungeni tangu 2005. Jamani hivi ni kweli?
Lowassa
wanayemzungumzia ni yule yule ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza katika
serikali hii ya awamu ya nne kwa takribani miaka miwili. Kikatiba, Waziri Mkuu
ndiye Kiongozi wa shughuli nzima za Serikali Bungeni. Hivi inawezekana vipi kwa
kiongozi mkubwa kama huyo (Waziri Mkuu)
kutokuongea lolote lile kwenye mikutano na vikao vya Bunge? Amu hoja au maswali
mazito yahusuyo serikali yakiwashinda Mawaziri, M/Waziri au Mwanasheria Mkuu
huwa yanatolewa ufafanuzi na nani?
Suala la kuongea mno Bungeni sio hoja ya
kuwaletea neema ya kimaendeleo bali Wapiga kura wanahitaji matendo na wala sio
maneno matupu . Wapo Wabunge ambao sio waongeaji lakini kwenye majimbo yao wameleta neema ya
ajabu kupitia uongozi wao.
Mathalani
Mh. Nimrod Mkono ambaye ni Mbunge wa Musoma Vijijini katika kipindi cha ubunge
wake amewaletea neema kubwa Wapiga kura wake. Amewajengea shule ya sekondari
kubwa na ya kisasa na kuikabidhi kwa Serikali, amejenga maabara ya kisasa iliyojitosheleza kila kitu mihimu, amejenga
nyumba za walimu. Pia amewanunulia gari la kubebea wagonjwa kwa wana wa jimbo
la Musoma vijijini na kadhalika. Pamoja na kutokuongea kwake Bungeni lakini
Wapiga kura wake hauwaelezi kitu kwani ni Mkono, Mkono tu. Hivyo kutokuongea
Bungeni sio tatizo.
Pia
mwangalie Mohamed Dewji “MO” (Mbunge wa Singida Mjini) ambaye yeye si muongeaji
lakini nyakati zote ameonyesha nia ya dhati ya kuwapenda na kuwathamini wapiga
kura wake. “MO” amejitolea kwalipia ada ya vyuoni wale wote wa jimbo lake waliobahatika
kupata elimu ya juu (chuoni), kwa wale pia ambao wana vigezo amewaahidi kuwapa
ajira za kudumu kupitia makampuni yake, hata hivyo pia amekamilisha miradi
mingi ya maendeleo ambayo ilikuwa inasuasua.
Hao ni
baadhi tu ya wale ambao sio waongeaji lakini ni watendaji haswaa ambao Wapiga
kura wao wanajivunia nao. Lakini wapo wale ambao ni mafundi wa kuongea hadi
kuwa wabwatukaji pale Bungeni lakini uongeaji wao huo haujawasaidia lolote lile
Wapiga kura wao.
Licha ya
ufundi wao wa kuongea lakini wameshindwa kuwatatulia kero za maji, umeme,
hospitali, shule ama masoko kwa ajili ya bidhaa zao; wengine waliahidi
kuwajengea majosho ya kuogesha ng’ombe wao, kuwajengea machinjio ya kisasa na
hata wengine wameshindwa kuikamilisha mradi wa ujenzi wa kawaida cha kusindika
Tangawizi tu. Wengine ndio wameua kabisa sekta ya kilimo katika majimbo yao hali ambayo
inawafanya Wananchi waishi maisha magumu na yasiyoelezeka.
Nimelazimika kuyaeleza haya kutokana na
mitazamo isiyo na tija kwa jamii inayozaa matukio ya uletaji ushabiki wa
kisiasa kwenye chombo muhimu cha kutunga sharia za nchi ambapo Wabunge
wanawatelekeza wapiga kura wao kwa kutokupigania maslahi yao na badala yake
wanaendekeza ushabiki wa kichama ndani ya Bunge.
Ni aibu isiyoelezeka kumuona Mbunge anawasha
kipaza sauti na kuanza kutoa maneno ya kebehi kwa kufuata utashi wa kisiasa.
Huko ni kuwapotezea muda wapiga kura wao.
Dhana ya hiyo ya kushabikia waongeaji ndani
ya Bunge imewafanya Wabunge wengi wasiwe watiifu mbele ya kiti cha Spika kwa
kujiamulia kuwasha vipasa sauti na kila mmoja kuanza kuzungumza na hatimaye
kuligeuza Bunge kuwa gulio na si tena mhimili wa dola.
Utoto wa Wabunge haustahili kuvumiliwa hata
kidogo kwa kuwa wao ni Watu wazima na watu wamewaamini kiasi cha kuwapatia
madaraka.
Endapo Mbunge atakuwa anatumia muda mwingi
kwa ajili ya kuzomea zomea ndani ya Bunge ama kutoa lugha za kebehi na dharau
ndani, atapata wapi wasaa wa kuwasemea matatizo ya Wapiga kura wao? Je, sisi
Wananchi wa kawaida tunanufaikaje na matokeo hayo ya kitoto yanayofanywa na
Wabunge wetu tuliowachagua?
Kimsingi, umaarufu wa Mbunge hauji kwa
kuzunumza kwa jazba wala kutoa lugha za maudhi awapo Bungeni, umaarufu wa Mbunge
utatokana na kutekeleza ahadi ahadi ya kukidhi matarajio kwa waliomchagua.
Ni vyema Wabunge wakatambua ya kwamba fursa
na uhuru waliopewa na watu waliowaamini una mipaka na una mwisho wake, ni vyema
wakautumia huo uhuru kabla wakati haujawapita kwani wakati ni ukuta,
wakishindana nao wataumia.
Ndugu zangu, kuna haja kubwa ya kuwa makini
sana wakati wa upigaji kura ili kuepukana na wabunge wasijali maslahi ya
Wananchi bali maslahi yao na ya chama chao, kuwaepuka viongozi watovu wa
nidhamu dhidi ya kanuni na utaratibu husika. Bila ya hivyo, tutazidi kuwa
maskini!
Post a Comment