WALALA HOI WALALAMIKA, WALITOA SH30,000 ZA MAOMBI ‘ZIMEENDA NA MAJI MANISPAA ya Temeke imetoa orodha ya majina ya wananchi waliopewa viwanja katika manispaa hiyo, ambayo inaonyesha kuwamo kwa vigogo wanaojumuisha mawaziri, wabunge, watendaji wakuu wa Serikali pamoja na baadhi ya watoto wa vigogo hao.Katika orodha hiyo, jumla ya watu 1,800 walipatiwa viwanja hivyo, huku majina hayo ya vigogo yakiwa ni zaidi ya 50, ambao baadhi wamejiandikisha wenyewe, wengine wake zao, ndugu na watoto wao. Majina hayo ambayo gazeti hili iliyaona jana, yamebandikwa kwenye ubao wa matangazo wa manispaa hiyo, ili wananchi walioomba viwanja hivyo waweze kuangalia kama wamo katika orodha ya waliopatiwa viwanja hivyo. Baadhi ya wananchi waliofika kusoma majina hayo walisikika wakilalamikia hali hiyo, huku wakisema kuwa kinachoonekana ni vigogo kupendelewa na kuwanyima wananchi wa kawaida. Katika orodha hiyo, majina yanayosomeka ni pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama; Naibu Spika, Job Ndugai; Waziri wa Mawasiliano, Sanyansi na Teknolojia, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima. Kwa upande wa Makatibu Wakuu wa Wizara wapo, Dk Florence Turuka (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Ramadhan Kijjah; Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Omary Chambo na Dk Idris Rashid ambaye ni Gavana wa Zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Pia wamo Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi, Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa; Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleinan Kova. Wengine ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Haruna Masebu; Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh na Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH),Marina Njelekela. Kwa upande wa wabunge wamo Dk Augustine Mrema (Vunjo - TLP), Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe; Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Sylvester Koka; Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan; Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Dk Cyril Chami na Mbunge wa Singida Kusini (CCM), Mohamed Misanga. Wengine ni Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila; Mbunge wa Igunga (CCM), Dk Peter Kafumu na Mbunge wa Bukene (CCM), Seleman Zedi. Wabunge wa Viti Maalumu (Chadema), Maulida Komu na Suzan Lyimo, Viti Maalumu CCM, Dk Mary Mwanjelwa na Zakhia Meghji ambaye ni mbunge wa kuteuliwa. Orodha hiyo pia inaonyesha majina ya ukoo yanayofanana na majina ya baadhi ya viongozi ambao ni Miraji Kikwete, Khalfan Kikwete, Juanita Mramba, Suzan Mkapa, Zainab Mkomwa, George Rupia, Maimuna Mfutakamba, Mary Membe, Pharles Ngeleja, Judith Kahama na Wilfred Mwanri. Mkurugenzi apatwa kigugumizi Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Magreth Nyalile alipoulizwa kuhusu orodha hiyo alisema kuwa, majina hayo hajayaona na kwamba waliobandika wamefanya uamuzi huo bila ya yeye kuupitia. “Majina yenyewe sijayaona, hivyo basi siwezi kujua ni kina nani waliopewa viwanja hivyo, kwa sababu wako zaidi ya 1,000, jambo ambalo litakuwa vigumu kwangu kubaini tatizo hilo,” alisema Nyalile. Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo hawezi kusema lolote kwa sababu yuko nje ya ofisi kwa ajili ya shughuli nyingine za ujenzi wa taifa. Hata hivyo, Nyalile alisema mchakato wa ugawaji wa viwanja hivyo ulifuata taratibu za kisheria na kwamba hakuna mtu au kiongozi yeyote aliyependelewa, jambo ambalo linaweza kusababisha mgongano wa hapa na pale. Nyalile alisema kuwa kama kuna viongozi walipewa kwa njia zisizo sahihi, au kwa rushwa wakati wa uwasilishaji wa majina hayo, walipaswa kutoa taarifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria. Wananchi walalama Baadhi ya wananchi walikuwa wakiangalia majina hayo katika ubao huo walidai kuwa, baadhi ya maofisa wa halmashauri hiyo wamedaiwa kupewa rushwa wakati wa ugawaji wa viwanja hivyo. “Walitangaza kama kiini macho, lakini tayari walikuwa na majina yao ili waweze kuwapatia na jambo ambalo limejionyesha wazi kwenye majina ya watu waliopewa viwanja hivyo,” alisema mwananchi mmoja (jina tunalihifadhi) na kuongeza: “Kutokana na hali hii, hatuna imani na viongozi wowote wa Serikali kwa sababu inaonyesha wazi kuwa, kila mmoja anaangalia masilahi yake na si wananchi wasio na kipato”. Aliongeza kuwa, wananchi hawana imani na viongozi wao, hivyo Serikali inapaswa kuingilia kati kwa sababu hali hiyo inaweza kusababisha matatizo. Mwananchi mwingine aliyekuwa akifuatilia jina lake alisema: “Wewe unachokiona ni nini hapo kama siyo yaleyale ya ubinafsi! Wewe unaamini kabisa kwamba kweli hawa viongozi wetu hawana nyumba au hawana viwanja hapa Dar es Salaam. Aliongeza: ”Kama manispaa walitangaza viwanja ili wajiuzie wangesema tu badala ya kuchukua fedha zetu Sh30,000 halafu viwanja wakajigawia wenyewe.” Mgawo wa Viwanja Mapema mwezi Juni mwaka huu, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ilitangaza kwamba imepima viwanja 1,800 katika eneo la Gezaulole ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa Mradi wa Upimaji Viwanja. Fomu za maombi ya kununua viwanja hivyo zilianza kutolewa Juni 11 na kila mwombaji alipaswa kulipia ada ya maombi ya kiasi cha Sh30,000 katika ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke iliyopo mkabala na Uwanja Taifa jijini Dar es Salaam. “Fedha hizo hazitarejeshwa na mwombaji atajaza nakala mbili za fomu ya maombi na kuzirejesha zikiwa zimebandikwa picha 3 za ukubwa wa pasipoti. Mwisho wa kurudisha fomu hizo ni tarehe 18.06.2012 saa 8 mchana,” linasomeka tangazo rasmi la manispaa hiyo. Wakazi wenye nyumba na mashamba ndani ya eneo la mradi ambao walikuwa wametambuliwa kabla ya zoezi la upimaji kuanza, pia walitakiwa kununua fomu za maombi kwa utaratibu uleule. LA LEO IJUMAA MLOLONGO mrefu zaidi wa majina ya vigogo umebainika kugawiwa viwanja katika eneo la Gezaulole, jijini Dar es Salaam, ambapo safari hii imo familia ya Rais mstaafu wa Awamu ya Pili Ali Hassani Mwinyi. Jana, gazeti hili lilichapisha katika ukurasa wa mbele habari iliyoonyesha baadhi ya majina ya vigogo waliogawiwa viwanja na kufanya wananchi wa kawaida kulalamika. Katika uchunguzi zaidi, imebainika kuna orodha ndefu ya majina ya vigogo waliopewa viwanja katika mradi huo wa Gezaulole ambayo inahusisha mawaziri, wabunge, wakuu wa taasisi za Serikali na familia za baadhi ya watu maarufu. Kwa upande wa familia maarufu, imo ya mzee Mwinyi ambaye pia amegawiwa eneo, wengine wana majina ya ukoo yanayofana na ya kwake ambao ni, Asina Mwinyi, Maimuna Mwinyi, Salama Mwinyi na Steven Ali Mwinyi, huku kutoka katika familia yenye jina la Kikwete yumo Ali J. Kikwete. Viongozi wengine maarufu waliogawiwa viwanja hivyo ni Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emanuel Nchimbi, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Manejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima. Kwa upande wa watendaji wa taasisi za dola, yumo Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilila, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, Kamishna wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Polisi, Clodwig Mtweve, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime, Balozi wa Tanzani nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya, SACP Hamdan Makame, ACP John Gudaba, ACP Saada Juma Haji na ACP Mohamed Usi. Mlolongo huo pia unaonyesha majina ya baadhi ya wabunge ambao ni Murtaza Mangungu wa Kilwa Kaskazini (CCM), Mohamed Misanga, (Singida Kusini CCM), Jenister Mhagama (Peramiho CCM), Kheri Ameir (Matemwe, CCM), Kaika Telele (Ngorongoro, CCM), Amina Clement (Koani, CCM) na Ali Hamis Seif (Mkoani, CUF) Pia kuna orodha ya wabunge wa Viti Maalum CCM ambao ni Subira Mgalu, Alshaiymaa Kweygir, Elizabeth Batenga, Josephine Genzabuke, Betty Machangu, Lediana Mng’ong’o na Mwanakhamis Kassim Said. Wabunge wengine wa Viti Maalum CCM ni Mariam Mfaki, Mariam Kasembe, Agnes Hokororo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa pamoja na Suzan Kiwanga ambaye ni mbunge wa Viti Maalum, Chadema na Ania Said Chaurembo ambaye ni mbunge mstaafu. Majina mengine ambayo koo zake ni za watu maarufu ni pamoja na Ahmed Dau, David Kandoro, Asila Ditopile, Alice Koka, Gemini Suchak, Fidelis Owenya, Filoteus Msigwa, Evelyne Manumba, Fatma Ismail Rage, Jamhuri Kihwelo, Issack Mwang’onda, Hijjal Makamba, Joseph Nyambibo, Mbwana Samata, Mohamed Mzimba na Mohamed Mtonga. Wengine ni pamoja na Masanja Manumba, Mariam Mkama, Mansour Al-Maamry, Onesmo Mtasiwa, Musa Chagonja, Omary Shein, Shimbo Shimbo, Sikitu Kijazi, Solomon Kivuyo, Thomas Nyalile na Aisha Sululu (diwani Jangwani, CCM). Pia wamo maofisa watatu wa Bunge ambao ni Herman Berege, Anslem Mrema na Theonest Ruhilabake pamoja na mmoja wa maofisa waandamizi ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Boniface Njombe. Wananchi waja juu Baadhi ya maofisa wa Manispaa ya Temeke walisema fomu zilizochukuliwa ni zaidi ya 20,000 na kwamba kila fomu ilikuwa ikiuzwa Sh30,000, hivyo kufanya fedha zilizokusanywa kuwa zaidi ya Sh600 milioni. Tayari mlolongo huo wa majina ya vigogo umesababisha baadhi ya wananchi waliokuwa wakisoma majina hayo kulalamikia mchakato wa utoaji viwanja hivyo, huku wengine wakidai kuwa, warejeshewe fedha zao. “Tumelipa Sh20,000 kila fomu ya kuombea kiwanja na wananchi tuliojitokeza ni karibu 30,000, lakini majina yanaonyesha kuwa asilimia kubwa ya waliopata ni vigogo ambao tunaamini wana viwanja mahali pengine,” alisema mwananchi mmoja(jina limehifadhiwa). Mwananchi huyo alisema kuwa, hakukuwa na umuhimu wa kutangaza zabuni hiyo kwa sababu tayari walikuwa na majina yao, hivyo walitakiwa kuwakabidhi viwanja vyao badala ya kuwasumbua na kuwatoza fedha. “Hali hii inaonyesha kuwa Serikali ipo kwa ajili ya watu wachache, wenye fedha na si wananchi wa kawaida,” aliongeza. Mwananchi mwingine (jina tunalo), alisema idadi kubwa ya watu waliokabidhiwa viwanja hivyo ni watoto wa vigogo na wabunge. Aliongeza kuwa hali hiyo inaonyesha wazi kuwa, hakuna kiongozi atakayewatetea wananchi, kwa vile kila mmoja wao yupo kwa ajili ya kupigania maslahi yake. “Wabunge ambao tuliwategemea kutetea maslahi ya wananchi ndio wanaoongoza kwenye orodha ya kujichukulia viwanja, hii inaonyesha wazi kuwa hakuna kiongozi atakayeacha shughuli zake ili kutetea maslahi ya wananchi,” alisema. Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Manispaa hiyo vinaonyesha kuwa, halmashauri hiyo imeingiza zaidi ya Sh600 milioni kutokana na uuzaji wa viwanja hivyo. chanzo: Mwananchi |
Loading...
Sakata la Vigogo waliojigawia viwanja Dar lazidi kunoga
BLOG RAFIKI
-
-
-
-
-
Rais Samia amlilia King Kikii2 hours ago
-
VOA Express2 hours ago
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
Post a Comment