Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

HUYU NDIYE SHUJAA CHIFU MKWAWA



Taifa likiwa kwenye maadhimisho ya kuwakumbuka Mashujaa wa Taifa hili, nimeonelea ni vyema niwaletee shujaa Mkwawa ili upate kumjua kiunaga ubaga.

Mkwawa au kwa jina defu Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga (1855 – 19 Julai 18981) alikuwa chifu na kiongozi mkuu wa Wahehe katika Tanzania wakati wa upanuzi wa ukoloni wa Ujerumani wakati wa mwisho wa karne ya 19. Mkwawa aliongoza upinzani wa Wahehe dhidi ya Wajerumani.
Jina la Mkwawa ni kifupi cha Mukwava ambalo ni kifupi cha Mukwavinyika iliyokuwa jina lake la heshima likimaanisha "kiongozi aliyetwaa nchi nyingi". Mkwawa alizaliwa mnamo mwaka 1855 mahali palipoitwa Luhotakaribu na Iringa mjini. Alikuwa mtoto wa chifu Munyigumba aliyeaga dunia mwaka 1879.
Babake Munyingumba aliwahi kuunganisha temi ndogo za Wahehe na makabila ya majirani kuwa dola moja. Aliiga mfumo wa kijeshi wa Wasangu waliowahi kuwa kabila lenye nguvu waliowahi kujifunza mfumo huu kutoka Wangoni na impi za Shaka Zulu. Hadi miaka ya 1870 eneo la Wahehe ilipanushwa mbali kuanzia kusini hadi katikati ya Tanzania ya leo.
Baada ya kifo cha chifu mzee watoto walishindana kati yao juu ya urithi wake na Mkwawa alishinda akawa kiongozi mpya. Aliendelea kupanusha utawala wake. Hadi mwisho wa miaka ya 1880 alitawala sehemu muhimu za njia ya misafara kati ya pwani na Ziwa Tanganyika. Misafara hii iliyobeba bidhaa za nje kama kitambaa, visu na silaha kutoka pwani ikirudi na watumwa na pembe za ndovu ilipaswa kumlipia hongo ikanunua pia wafungwa wa vita zake. Hapo athiri na uwezo wake wa kulipa jeshi kubwa ikapanuka.

Mkwawa na upanuzi wa Wajerumani
Tangu miaka ya 1885 Wajerumani walianza kuunda koloni yao katika Tanzania bara. Mwaka 1888/89 utawala wao ulitikisihwa na vita ya Abushiri lakini baada ya kushinda upinzani wa Waafrika wa pwani Wajerumani walilenga kuimarisha utawala wao juu ya sehemu za bara.
Mkwawa aliwahi kusikia mapema habari za Wajerumani akajaribu kuwasiliana nao lakini bila kuelewana. Aliamua kujenga boma imara lenye kuta za mawe kwenye makao makuu yake huko Kalenga karibu na Iringa. Katika mwezi wa Februari 1891 alituma wajumbe kwa kambi la Wajerumani huko Mpwawa wakapokelewa na gavana Mjerumani. Wakati huohuo Mkwawa aliendelea kutuma askari zake hadi Usagara iliyotazamiwa na Wajerumani kama eneo lao. [1] Katika kipindi hiki gavana mpya Julius von Soden alifika Dar es Salaam. Hakuwa na mamlaka juu ya mkuu mpya wa jeshi Emil von Zelewski aliyepokea amri zake kutoka Berlin moja kwa moja. Baada ya kusikia habari za mashambulio ya Mkwawa katika Usangara aliomba na kupata kibali cha "kuwaadhibu Wahehe".

Mapigano ya Lugalo
Emil von Zelewski, kiongozi Mjerumani wa Lugalo
Katika mwezi wa Julai 1891 von Zelewski aliongoza kikosi cha maafisa Wajerumani 13 na askari Waafrika hasa kutoka Sudan 320, pamoja na wapagaji 113. Walikuwa na bunduki za kisasa, bunduki za mtombo na mizinga midogo. Zelewski aliwadharau Wahehe kama washenzi ambao walikuwa na mikuki na pinde tu. Kwa hiyo hakuuona haja ya kutuma wapelelezi wa awali. Njiani aliangamiza vijiji alivyokuta na katika mwezi wa Agosti alipoona Wahehe 3 waliomkaribia aliagiza kuwaua bila kuongea nao. Kumbe walikuwa mabalozi wa Mkwawa aliyetaka kujadiliana na Wajerumani.
Tarehe 17 Agosti 1891 Zelewski na jeshi lake walipita kwenye manyasi marefu karibu na Lugalo. Mkwawa alikuwa alimsububiri na Wahehe 3,000 walionyamaza hadi Wajerumani waliotembea kwa umbo la safu ndefu walikuwa karibu kabisa wakawashambulia. Wajerumani walikosa muda kuandaa silaha zao wakashtushwa kabisa. Sehemu kubwa ya askari waliuawa katika muda wa dakika chache pamoja na jemadari von Zelewski. Sehemu ya kombania ya nyuma ilirudi nyuma na kusimama kwenye kilimo kidogo walipoweza kutumia bunduki la mtombo wakajitetea na kuua Wahehe wengi. Sehemu hii ilijumlisha maafisa 2 na maafande 2 Wajerumani waliweza kukimbia na kujiokoa pamoja na askari 62 na wapagaji 74.

 Kipindi cha vita dogo

Baada ya mapigano Mkwawa alihesabu wafu wake waliokuwa wengi. Alikataza bada za kilio kwa sababu alitaka kuficha idadi ya askari waliokufa. Akaelewa sasa ya kwamba silaha za Wazungu zilikuwa hatari alituma tena mabalozi kwa gavana von Soden walioeleza ya kwamba Wahehe walikuwa walijitetea tu dhidi ya shambulio walitaka amani. Lakini madai ya Wajerumani yalikuwa magumu eti kuwaruhusu wafanyabiashara kupita bila matata na kutoshambulia majirani tena.
Mkwawa hakuwa tayari kuahidi yote akachelewesha mikutano. Wakati huu kamanda mpya Mjerumani Tom von Prince alijenga boma jipya la Wajerumani katika Uhehe na Mkwawa alijibu kwa kusambulia vikosi vidogo vya jeshi la kikoloni. Gavana Soden alidai kutoendelea na mapigano. [2]. 1893 gavana von Soden aliondoka Afrika na gavana mpya von Schele alitaka kulipiza kisasi akaamuru mashambulio dhidi ya Mkwawa.

 Anguko la Kalenga

Mwezi wa Oktoba 1894 von Schele aliongoza kikosi cha maafisa Wajerumani 33 na askari Waafrika pamoja na wagajai zaidi ya 1000 kuelekea Kalenga. Walikuwa na mizinga 4 na bunduki bombomu. Walipofika mbele ya Kalenga Wahehe walijisikia salama kutokana na kuta imara lakini Wajerumani walijipanga kilomita kadhaa nje ya mji wakaanza kufyatulia mizinga yao na kuua watu ndani ya mji. Wakati wa giza kwenye asubuhi wa 30 Oktoba 1894 askari wa jeshi la Schutztruppe walipanda ukuta katika sehemu ulipodhoofishwa tayari na kuingia mjini. Hadi jioni walikuwa waliteka mji wote. Gombora na mikuki ya Wahehe hazikuweza kushindana na bombomu za Wajerumani. Mkwawa mwenyewe aliamua kukimbia pamoja na 2000 - 3000 askari lakini kabla ya kukimbia alimwua mganga mzee aliyewahi kutabiri ya kwamba atawashinda Wajerumani waliokuja. Gavana von Schele aliandika taarifa kwa serikali ya Ujerumani "tulizika maadui 250, wengine walichomwa katika nyumba zao, wanawake na watoto 1500 kutekwa nyara" [3].
Mkwawa alijificha msituni pamoja na askari zake akasubiri. Gavana von Schele alishindwa kuendelea na mashambulio wa sababu gharama za vita zilishinda makaisio yake na wabunge wa upinzani katika Reichstag huko Berlin walipinga vita ya kikoloni; walikataa kuongeza makisio na kiongozi wa wasoshalisti August Bebel aliita mtindo wa kuchoma mji na kuteka nyara watoto na wanawake "ushenzi mkuu".

 Amani fupi

Baada ya kuondoka kwa Wajerumani Mkwawa aliweza kurudi na kujenga tena nyumba mahali pa Kalenga. Katika Septemba 1895 Mkwawa alikuwa tayari kujadiliana na Wajerumani na tar 12 Oktoba walipatana amani. Wajerumani walimkubali Mkwawa kama chifu wa Wahehe , Wahehe waliahidi kukabidhi gobori zote, kuonyesha bendera ya Kijerumani na kuwaruhusu wafanyabiashara na wasafiri kupita Uhehe. Mkwawa alimwagiza mjomba wake kutia sahihi akakataa mwenyewe akisema hii ingemwua. Hata hivyo miezi kadhaa baadaye alitafuta msaada wa Wajerumani kwa shambulio dhidi ya Wabena.
Afisa mmoja Mjerumani aliyefika Kalenga mpya alizuiliwa kuingia na kumwona chifu akaambiwa alipe hongo ya bundiki 5 wa kuingia katika eneo la Mkwawa. Hapo maafisa wa jeshi la Wajerumani waliolinda mpaka ambao bado walitafuta nafasi ya kulipiza kisasi kwa Lugalo waliamua chifu alivunja mkataba. Kapteni Tom von Prince alijenga boma jipya karibu na Kalenga alianza kuwasiliana na machifu wadogo wa Wahehe. Mkwawa alijaribu kujenga mapatano na majirani lakini Wabena na makabila mengine walikumbuka vita na mashambulio ya awali kutoka Uhehe walipendelea kushikamana na Wajerumani. Mkwawa aliwaua machifu wawili wahehe waliowahi kukaa na von Prince lakini aliona hawakuwa wa pekee waliosita kumtii tena. Alipata habari ya kwamba mdogo wake Mpangile alishikamana na Wajerumani. Wakati wa Septemba 1896 Wahehe waligawanyika na sehemu kubwa ya viongozi waliochoka vita ilikuwa tayari kuwakubali Wajerumani.[4]. Wajerumani waligawa eneo lao. Wasangu walirudishwa katika eneo lao la awali wakarudi kutoka Usafwa katika mji mkuu wa Utengule Usangu. Mpangile alisimikwa kama kiongozi mpya wa Uhehe penyewe lakini baaa ya siku 50 alisimamishwa na kuuwa na Wajerumani waliomshtaki eti anamsaidia kakaye kisiri.

 Mafichoni na kifo

Mkwawa alikuwa aliondoka sehemu za Iringa mwezi wa Agosti 1896 alipoona mgawanyiko. Alifuata mwendo wa mto Ruaha akilindwa na wenyeji waliokuwa tayari kumficha na na kumlinda dhidi ya vikosi vya Wajerumani waliomtafuta. Disemba 1896 alihamia milima ya Uzungwa alipojificha. Kutoka hapa alitelemka mara kwa mara kwenye mabonde alipopata vyakula na kushambulia vikosi vidogo vya askari vya Kijerumani.
Katika Julai 1897 kikosi kikubwa cha Wasangu pamoja na Wahehe chini ya uongozi wa Wajerumani walikuta kambi la Mkwawa mlimani wakashambulia lakini Mkwawa aliweza kukimbia. Mwaka 1898 Mkwawa aliendelea kujificha kwenye misitu akiongozana na watu wachache sana. Aliishi hasa kwa njia ya kuvinda. Wakati wa Julai 1898 aliongozana na wavulana 4 pekee halafu Wazungwa 2 mume na mke. Tarehe Julai 16 Wajeumani waliowahi kusikia habari zake walimkuta huyu mama Mzungwa alipotafuta chakula wakamkamata akawaambia Mkwawa alielekea kusini. Wakamfuata na tar 18 Julai Mkwawa alimwua mume Mzungwa kwa hofu ya kusalitiwa. Aliendelea na wavulana 2 tu walioitwa Musigombo na Lifumika. Watoto waliogopa angeweza kuwaua pia. Hapo Lifumika aliamua kukimbia asubuhi ya tar 19 Julai. Lakini siku ileile alipotelemka kutoka mlimani alikutana na kikosi cha Wajerumani akakimbia lakini wakamshika wakamlazimisha kuwaambia habari za Mkwawa. Kijana alimwambia sajenti Mjerumani kuwa chifu alikaa mgonjwa mahali kwa umbali wa masaa 3.
Walimlazimisha kuwaongoza. Njiani walisikia kwa mbali sauti ya bunduki, risasi 1. Wakaendelea na baada ya masaa mawili walikuta maiti za Mkwawa na kijajana mwingine. Inaonekana waliwahi kujiua na sauti ya bunduki ilikuwa Mkwawa aliyejipigia risasi.[5].

 Fuvu la Mkwawa

Fuvu la Mkwawa katika Makumbusho ya Kalenga karibu na Iringa, Tanzania
Kichwa cha mtemi kinasemekana kilikatwa na Wajerumani na kutumwa Berlin kilipohifadhiwa katika makumbusho, awali Berlin na baadaye Bremen.
Waingereza waliochukua utawala wa koloni mwaka 1918 baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia walitaka kuonekana kama mabwana wema. Mkuu wa serikali ya kikoloni ya Tanganyika alipendekeza kurudisha fuvu kwa sababu Wahehe walishirikiana na Waingereza wakati wa vita. Hivyo kuna kipengele 246 katika mkataba wa Versailles kinachosema: "Katika muda wa miezi 6 baada ya kuthebitishwa kwa mkataba huu ... Ujerumani itakabidhi fuvu ya Sultani Mkwawa iliyohamishwa kutoka Afrika ya Mashariki ya Kijerumani na kupelekwa Ujerumani kwa serikali ya Mfalme wa Uingereza."
Wajerumani walikataa habari za fuvu hii na Waingereza waliamua ya kwamba ilishindikana kuikuta. Lakini baada ya vita kuu ya pili ambako Ujerumani penyewe ilivamiwa na wanajeshi wa Uingereza gavana Twining wa Tanganyika alikumbuka habari za fuvu akatembelea Ujerumani na kutazama mafuvu ya makumbusho ya Bremen.Katika mkusanyiko wa fuvu 2000 zilikuwa 84 zenye namba zilizoonyesha zilitoka kiasili katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Hapa alizipanga kufuatana na ukubwa na kutazama zile zilizokuwa na vipimo vya karibu na ndugu za Mkwawa aliowahi kupima kabla ya safari yake. Hapa aliteua fuvu yenye shimo kwa sababu taarifa ya kale ilisema Mkwawa alijiua kwa kujipigia risasi kichwani.
Fuvu hii ilipelekwa Tanganyika tarehe 9 Julai 1954 na kuhifadhiwa katika jengo la makumbusho ya Mkwawa kwenye kijiji cha Kalenga.

chanzo: Wikipedia.com
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top