MISAADA inayotolewa na kada wa CCM na mfanyabiashara maarufu hapa nchini,
Mustafa Sabodo, kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), sasa inaonekana
kuwagawa makada wa chama hicho tawala.
Baadhi ya makada wamekuwa wakitaka Sabodo atimuliwe kwenye chama hicho kwa
madai ni msaliti na mwenye lengo la kuiimarisha CHADEMA inayoonekana kutishia
utawala wa CCM.
Miongoni mwa makada wa CCM ambao kwa wakati tofauti walitaka Sabodo atimuliwe
ndani ya chama hicho ni pamoja na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Stephen
Mashishanga na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja.
Harakati za makada hao kutaka Sabodo atimuliwe jana ziligonga mwamba baada ya
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kuunga mkono
hatua za Sabodo kukisaidia CHADEMA.
Nape aliwataka Watanzania wengine waige mfano huo, kwakuwa itikadi za kisiasa
haziwezi kuwakwamisha wananchi wasishirikiane.
Katika taarifa yake iliyowekwa katika mtandao wa kijamii wa Daily Nkoromo,
Nape alisema kuwa haoni tatizo kwa Sabodo kukisaidia CHADEMA hasa katika suala
la upatikanaji wa visima kwa kile alichoeleza watakaonufaika na visima hivyo ni
Watanzania wote pasipo kujali vyama vyao.
Kauli hiyo ya Nape ambaye ndiye msemaji wa CCM, inapingana na kauli za makada
wengine ndani ya chama hicho juu ya mtazamo wa kuendelea kumkumbatia Sabodo
anayejipambanua na wafanyabiashara wengine katika kuhakikisha mageuzi ya kweli
yanapatikana nchini.
Nape alisema uamuzi wa kutoa ufafanuzi huo ni kutokana na maswali mbalimbali
yanayoelekezwa kwake na watu tofauti juu ya hatima ya michango inayotolewa na
Mustapha Sabodo kwa CHADEMA, pamoja na matamshi yake dhidi ya CCM.
“Kuna watu wengi wanauliza nini maoni yangu juu ya uamuzi wa mzee Sabodo
kusaidia vyama vya upinzani na hasa CHADEMA.
Kimsingi sioni tatizo katika hili, la muhimu ni yeye kuendelea kuwa
mwanachama muaminifu wa CCM,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Nape.
Alisema kama kuna mwanachama wa CCM atakayekuwa na shaka juu ya uungwana huo
wa mzee Sabodo itampasa arejee maamuzi ya serikali ya kuruhusu mfumo wa vyama
vingi na aangalie utaratibu wa kuvipatia vyama ruzuku, kwa kile alichoeleza kuwa
ulikuwa na lengo la kudumisha umoja kwa kuviwezesha kufanya kazi ya kuikosoa
serikali na kuhimiza maendeleo.
Aliongeza kuwa wenye fikra ya kuona mzee Sabodo anakisaliti Chama Cha
Mapinduzi watakuwa si wanasiasa wa kweli na Wana CCM waaminifu wanaoitakia mema
Tanzania.
“Hivi kwanini tunataka kuwafikisha Watanzania mahali wasisaidiane kisa
siasa!....wapo wanaohoji kwanini mzee Sabodo ametoa visima kwa CHADEMA? Sasa
najiuliza visima vitakapoanza kufanya kazi watumiaji wataulizwa itikadi zao au
kila mwananchi ana uhuru wa kutumia? Tatizo hapa ni nini? Narudia sioni tatizo
kwa mzee Sabodo kusaidia vyama vya upinzani ili mradi pesa hizo ni zake!"
alisema Nape.
Mzee Sabodo licha ya kuwa ni kada wa CCM mara nyingi amekuwa akijitokeza wazi
wazi kuisaidia CHADEMA katika masuala mbalimbali ya kifedha.
chanzo: Tanzania Daima
|
Post a Comment