* AGOMA KUJIUZULU KUTOKANA NA UZEMBE WA WATENDAJI WAKE WALIOPELEKEA KUZAMA KWA MELI YA M.V SKAGIT
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema hawezi kujiuzulu kutokana na ajali ya Mv Skagit kwa sababu hahusiki na suala hilo.
Pia, amesema kitendo cha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano Zanzibar, Hamad Masoud kwasababu ya ajali hiyo kimechelewa kwa kuwa alitakiwa afanye hivyo tangu wakati wa ajali ya Mv Spice Islanders.
Dk Mwakyembe alisema hayo jana bungeni alipokuwa akijibu hoja za wabunge katika hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2012/13.
Alisema kujiuzulu ni kitendo cha heshima na inashangaza sana mtu anapojiuzulu kiuwajibikaji halafu anaanza kulalamika kwa pembeni.
“Kwa hili langu halina msingi wowote wa mimi kuweza kujiuzulu kwa kuwa Rais wa Zanzibar amelizungumzia vizuri na pia Rais wa Jamhuri ya Muungano amelizungumzia pia,”alisema Dk Mwakyembe.
Alisema uhusiano wake kimamlaka na upande wa Zanzibar unaishia Chumbe tu kwa kuwa hana mamlaka kwa upande huo mwingine wa visiwani.
Dk Mwakyembe alisema, sheria za awali iliyokuwa inasimamia pande hizo mbili ilikuwa inasimamia vyombo vya majini kwa umakini na kwamba baada ya kutenganishwa kwa mamlaka za usimamizi, kila mamlaka ikawa na sheria zake.
“Uhusiano wangu kwa upande wa Zanzibar mwisho wangu ni Chumbe hivyo sijiuzulu, sheria yetu iko strictly(makini) kwenye masuala ya vyombo vya majini lakini ya Zanzibar haibani hivyo,”alisema Dk Mwakyembe.
chanzo: Mwananchi
Post a Comment