Ngassa sasa wa Azam |
Na
Mahmoud Zubeiry
MRISHO Khalfan Ngassa ameuzwa Simba kwa dau la Sh. Milioni
25 mchana wa leo, Azam imethibitisha.
Habari za ndani kutoka Azam, ambazo BIN
ZUBEIRY imezipata kutoka klabu hiyo, zimesema kwamba Simba wamelipa
fedha hizo na wamesainiwa fomu za uhamisho na sasa Mrisho anafuata nyayo za
baba yake Khalfan Ngassa, ambaye aliichezea Simba SC 1991/1992.
Azam ilifikia uamuzi wa kumuuza Ngassa, baada ya
mchezaji huyo iliyemsajili kutoka Yanga miaka miwili iliyopita, kubusu jezi ya
Yanga baada ya kufunga bao la pili katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki
na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC).
Na uamuzi huo, ni wa mzee Said Salim Bakhresa
mwenyewe, ambaye alikerwa na kitendo hicho akawaagiza wanawe, Wakurugenzi wa
bodi ya timu wamuuze mchezaji huyo popote, haraka iwezekanavyo.
Ngassa alikuwa amebakiza mwaka mmoja katika mkataba
wake aliosaini na Azam FC, akitokea Yanga miaka miwili iliyoipita kwa dau la
Sh. Milioni 55, lakini wasiwasi unakuja kwamba, Ngassa ana mapenzi na Yanga na kwa
Simba kumsajili, kuna hatari yaliyotokea akiwa Azam, yatajirudia hata akiwa kwa
Wekundu wa Msimbazi.
NGASA APINGA KUUZWA KWAKE
MSHAMBULIAJI mpya wa Simba SC, Mrisho Khalfan Ngassa
amepiga hodi Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji kupinga kuuzwa
kwake katika klabu hiyo, akitokea Azam FC bila kuhusishwa.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Ngassa amesema
kwamba hajafanya mazungumzo na Simba SC wala Azam FC juu ya uhamisho. “Mimi
sijui chochote, na sikatai kuhamishwa, kwa sababu mimi soka ni kazi yangu na ninaweza
kucheza popote, ila taratibu zifuatwe tu,”alisema.
Ngassa amesema baada ya kuona mambo yanakwenda
kinyume cha utaratibu, ameamua kulifikisha suala lake Kamati ya Sheria, Maadili
na Hadhi za Wachezaji ili haki itendeke.
Chanzo: Bin Zubeiry
Post a Comment