Loading...
SERIKALI INATEKELEZA AHADI YAKE YA KUONGEZA MATABIBU
Na Veronica Kazimoto – MAELEZO
Serikali inafanya kila jitihada ili kuhakikisha kwamba Zahanati zinazojengwa katika kila kijiji zinapata watumishi wa kutosha wa kutoa huduma za afya kwa wananchi wanaoishi katika vijiji hivyo. Akijibu swali bungeni leo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Aggrey Mwanri amesema jitihada mojawapo inayofanywa na serikali ni kuongeza udahili wa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu katika fani ya afya.
“Mkakati unaofanywa na Serikali kuongeza watumishi wa katika Zahanati mbalimbali nchini ni kuongeza udahili wa wanafunzi vyuo vikuu hususani katika fani ya afya,” amesema Naibu Waziri huyo.
Mwanri amesisitiza kuwa jitihada nyingine ni kuwapanga madaktari wanaohitimu moja kwa moja katika vituo vya kazi na kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Akiizungumzia Halimashauri ya Wilaya Lushoto, Mwanri amesema katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 Halimashauri hiyo iliomba kibali cha kupata watumishi 45 wa kada za afya na mpaka sasa watumishi 31 wamekwisharipoti ambapo watumishi 14 hawajaripoti. Watumishi hao ambao tayari wameripoti watapangwa katika Zahanati na vituo vya afya vilivyomo katika halimashauri hiyo ili kukidhi mahitaji ya Zahanati zilizopo.
Mwanri amefafanua kuwa Zahanati ya Mlingano yenye watumishi watatu na Zahanati ya Kwai yenye watumishi 11inayomilikiwa na Shirika la dini katika Halimashauri ya Lushoto, zote zimeshaanza kutoa huduma za afya katika vituo hivyo. Nia ya Serikali kujenga Zahanati katika kila Kijiji ni kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ambapo lengo ni kumfanya mgonjwa asitembee umbali wa zaidi ya kilometa 5 kufuata huduma hiyo.
Post a Comment