Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala Pamela Kalala (kushoto),akitoka
katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana,baada
ya kusomewa shitaka la kuomba rushwa ya Shilingi milioni tatu. HAKIMU
Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Pamela Kalala amepandishwa
kizimbani kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa mke wa mmoja
wa washtakiwa aliokuwa akisikiliza kesi yao. Hakimu Kalala alipandishwa
kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana asubuhi na
kusomewa mashtaka matatu ya kuomba rushwa ya Sh3 milioni na kupokea
rushwa ya Sh900,000 kwa nyakati tofauti. Mwendesha Mashtaka wa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Allen Kasamala alidai mbele
ya Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo
kwa nyakati tofauti Februari, mwaka huu. Katika kosa la kwanza, Kasamala
alidai kuwa mshtakiwa huyo aliomba rushwa ya Sh3 milioni kutoka kwa
Josephine Omar ambaye ni mke wa mmoja wa washtakiwa katika kesi namba
703 ya mwaka 2008 inayohusu kujipatia fedha kwa njia zisizo halali.
Kasamala alidai kuwa mshtakiwa alimwomba Josephine kiasi hicho cha
rushwa ili kumshawishi ampendelee mumewe katika kutoa uamuzi wa kesi
hiyo aliyokuwa akiisikiliza. Katika shtaka la pili, Kasamala alidai kuwa
Februari, tarehe isiyofahamika, mshtakiwa alipokea rushwa ya Sh800,000
kutoka kwa Josephine na katika kosa la tatu, alidai kuwa Februari 6,
mwaka huu mshtakiwa alipokea rushwa ya Sh100,000 kutoka kwa mwanamke
huyo. Kasamala alidai kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo akiwa
mwajiriwa wa Idara ya Mahakama kwa wadhifa wa Hakimu Mkazi. Alisema
Kalala alitenda makosa hayo kinyume cha Kifungu cha 15 cha Sheria ya
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007. Hata
hivyo, mshtakiwa alikana mashtaka yote na upande wa mashtaka ulidai kuwa
upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Hakimu Katemana alimwachia
mtuhumiwa huyo kwa dhamana, baada ya kutimiza masharti ambayo ni pamoja
na kusaini bondi ya Sh1 milioni na kuwa na mdhamini mmoja anayefanya
kazi katika taasisi inayotambulika, ambaye pia alisaini bondi ya Sh1
milioni. Hakimu Katemana aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 23, kwa ajili
ya kutajwa. Mahakimu na rushwa Kalala anakuwa hakimu wa nne kupandishwa
kizimbani katika Mahakama ya Kisutu kwa tuhuma za rushwa, katika
kipindi cha miaka mitano. Desemba mwaka 2007, aliyekuwa Hakimu Mkazi wa
Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Jamila Nzota alipandishwa kizimbani katika
Mahakama hiyo akituhumiwa kupokea rushwa ya Sh700,000. Nzota alikuwa
akikabiliwa na tuhuma za kuomba rushwa hiyo kutoka kwa Mollel, aliyekuwa
Mwakilishi wa Kampuni ya Amanarth Enterprises Ltd iliyokuwa na kesi ya
madai namba 33/207 mbele yake, ili amsaidie. Katika kesi hiyo, Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hanzron Mwankenja (mstaafu kwa sasa),
alimhukumu Nzota kwenda jela miaka kumi na moja kuanzia Mei 22, 2009,
baada ya kupatikana na hatia katika makosa manne yaliyokuwa yakimkabili.
Hata hivyo, Hakimu Mwankenja alisema mshtakiwa atatumikia adhabu zote
kwa pamoja, hivyo alitumikia kifungo cha miaka mitatu jela. Nzota
hakuridhika na hukumu hiyo na kupitia kwa Wakili wake, Majura Magafu
alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, lakini katika hukumu
iliyotolewa na Jaji Emilian Mushi, Aprili 30, 2010, alishindwa tena.
Wengine ni aliyekuwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Adolf Mahai, (2007) na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Ukonga, Ndovela
Kihenga, (Juni 2011). Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari
on Tuesday, September 25, 2012
Post a Comment