HALI si
shwari katika ofisi ndogo za Bunge zilizopo jijini Dar es Salaam, baada
ya watu wanaodaiwa kuwa watumishi wa Bunge, kuiba seti ya televisheni ya
kisasa (flat screen) ya nchi 42 ndani ya ofisi ya Spika wa Bunge, Anna
Makinda, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Habari
zinaeleza kuwa watu hao ambao hadi sasa wanaendelea kusakwa, walifungua
mlango wa ofisi ya Spika na kuishusha seti hiyo ya televisheni,
iliyokuwa ukutani na kutimka nayo.
Habari
kutoka ndani ya ofisi hiyo, zilisema kuwa tangu tukio hilo litokee
takriban wiki mbili zilizopita, ofisi hiyo imekuwa moto kutokana na
msako na uchunguzi unaoendelea kubaini waliohusika, huku watuhumiwa
wakubwa wakiwa baadhi ya watumishi wa idara mbalimbali, hasa walinzi
wanaofanya kazi katika ofisi hiyo.
Hata hivyo
taarifa zingine kutoka ndani ya ofisi hiyo zilisema kuwa jaribio la
kutaka kuiba seti hiyo ya televisheni lilikwama kwani mwizi huyo
alishindwa kuitoa nje na kuondoka nayo.
“Ukweli ni
kwamba kuna mtu au watu walifanya jaribio la kutaka kuiba seti ya
televisheni katika ofisi ya Spika kwani alifanikiwa kuharibu kitasa cha
mlangoni na kufanikiwa kuingia ndani, lakini pamoja na kufanikiwa
kuishusha chini, alishindwa kuitoa kutokana na uzito wake,” kilisema
chanzo chetu cha habari.
Kwa mujibu
wa habari hizo, haijajulikana kama watu hao walitaka kuchukua
televisheni hiyo pekee au na vitu vingine vilivyokuwa ndani ya ofisi
hiyo.
Mtoa
taarifa wetu, alilieleza gazeti hili kuwa mazingira hayo ya mtu
aliyetaka kuiba yanaonyesha kuwa hayakufanywa na mtu wa mbali bali ni wa
karibu kabisa na inawezekana na mmoja wa watumishi wa ofisi hiyo hiyo.
Taarifa za
awali zinaeleza kuwa, tayari kampuni moja ya ulinzi iliyokuwa inalinda
katika ofisi za Bunge za Dar es Salaam na kule bungeni Dodoma
imeondolewa.
Alipotafutwa
mmoja wa maofisa wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa Kimataifa wa
ofisi za Bunge, Prosper Minja, alikiri kuwapo kwa taarifa hizo za wizi
katika ofisi za Spika.
“Ni kweli
tukio hili nililisikia, lakini lilitokea zamani, tangu wakati ule wa
sensa… lakini haijajulikana ni nani aliyetaka kuiba,” alisema Minja..Alipoulizwa
juu ya kuwapo kwa taarifa za kufukuzwa kwa moja kati ya kampuni za
ulinzi zilizokuwa zikilinda katika ofisi hizo za Bunge na zile za
Dodoma, alishindwa kukubali wala kukataa.
Akifafanua
kuhusu hilo, alisema anachofahamu yeye ni kwamba Tume ya Maadili
inayoundwa na wenyeviti wa kamati za Bunge ndiyo inayoweza kuzungumzia
juu ya suala hilo kwa sababu lipo mikononi mwao.
Alisema
chini ya tume hiyo kuna kamati ndogondogo ikiwamo ile ya ajira na
utumishi ambayo kimsingi inashughulikia ajira zote za watumishi au
kampuni zinazopitishwa kufanya kazi katika ofisi za Bunge.
Kwa mujibu
wa Minja hata kampuni za ulinzi ajira zao zinapitishwa na kamati hiyo ya
ajira na utumishi kwa kushirikiana na Wizara ya Utumishi wa Umma.
“Kama kuna
kampuni imefukuzwa basi hilo linaweza kuzungumziwa na kamati hiyo,
lakini ninachofahamu mimi ni kwamba kampuni za ulinzi binafsi na
nyingine kama zile za usafi zinazoajiriwa chini ya mkataba wa Public
Private Partnership (PPP) zinaajiriwa kwa mkataba wa muda fulani.
“Kwa maana
hiyo mkataba ukiisha zabuni zinaitishwa upya, kampuni iliyokuwa labda
inalinda nayo inalazimika kuomba tena, sasa hapo inaangaliwa kampuni
ambayo ni bora zaidi ndiyo inayopewa zabuni… kama imeondolewa
inawezekana imeondolewa kwa sababu hiyo, sina uhakika na taarifa ya
kampuni ya ulinzi kuondolewa.
“Lakini
sidhani kama imeondolewa kwa sababu nilipofika hapa asubuhi mlinzi
aliyenifungulia mlango na kunifuata kunisainisha ni yule yule wa siku
zote,” alisema Minja.
Habari za
Ofisi ya Spika kutaka kuibiwa zimekuja ikiwa ni takriban zaidi ya miaka
mitatu tangu ufanyike wizi katika ofisi za aliyekuwa Spika wa Bunge
lililopita, Samuel Sitta.
Chanzo: tanzania daima.
Post a Comment