Rais
na Amiri Jeshi Mkuu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akitoa pole kwa mjane na
ndugu wa wa Meja Jenerali Mstaafu Anatoli Kamazima leo nyumbani kwa
marehemu Tegeta, Dar es salaam. Marehemu Kamazima, ambaye amefariki
dunia usiku wa kuamkia leo Jumatano ya Tarehe 26 Septemba, 2012
kutokana na mshtuko wa moyo, alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa kwanza wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU.
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini katika kitabu cha maombolezo
nyumbani kwa Marehemu Meja jenerali Kamazima Tegeta, Dar es salaam, leo.
………………………………………………………………..
Rais Jakaya Mrisho
Kikwete amemtumia salamu za pole Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis
Mwamunyange kufuatia kifo cha Meja Jenerali Anatory Ruta Kamazima
(Mstaafu) aliyefariki jana tarehe 25 Septemba, 2012 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Nimepokea kwa mshituko na huzuni
nyingi habari za kifo cha Meja Jenerali Kamazima, ni pigo kubwa sana
kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Taifa kwa ujumla” Rais
amesema katika salamu hizo.
Mchana wa leo Rais ameitembelea familia ya marehemu nyumbani kwao Tegeta kuwafariji wafiwa.
Marehemu alizaliwa mwaka 1946
katika kijiji cha Maruku, Mkoani Kagera. Alijiunga na Jeshi mwaka 1967,
mara baada ya kuhitimu Chuo Kikuu mwaka 1966.
Marehemu Kamazima amesoma kozi
mbalimbali za kijeshi hapa nchini na nchi za China, India, Uingereza na
Misri na kulitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika ngazi
mbalimbali ambapo mwaka 1989, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Tume ya
Kuzuia Rushwa Tanzania, hadi alipostaafu Juni 2003.
Rais amemuelezea marehemu
Kamazima kama mzalendo na mtu aliyeipenda na kuitumikia nchi yake kwa
weledi mkubwa, uaminifu na moyo mmoja.
“Nimemfahamu Marehemu kwa miaka
yote ya utumishi wake jeshini na serikalini kama mzalendo, muaminifu na
mwenye moyo wa kulinda nchi yake wakati wote” amesema “Marehemu Kamazima
alikua mtu wa kutumainiwa sana katika nchi yetu na kamwe hatutamsahau
kwa utumishi wake uliotukuka”.
“Tutamkumbuka na kumuenzi siku
zote, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote na tunamuombea mapumziko mema
Marehemu Kamazima. Amina”. Rais ameongeza.
Marehemu ameacha mjane, watoto na wajukuu.
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu.
DAR ES SALAAM
26 Septemba, 2012
Post a Comment