Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Ali Abdalla Ali akizungumza na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba (hayupo pichani) wakati wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala bora ilipotembelea Ofisi za Makao Makuu ya Tume hiyo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Mdungi Makame Mdungi na wengine ni wajumbe wa Kamati hiyo.
………………………………………………
Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesisitiza umuhimu wa wadau mbalimbali wakiwemo wanasiasa, asasi za kiraia na kidini kuwaacha wananchi kutoa maoni yao binafsi kuhusu Katiba Mpya.
Dar es Salaam
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesisitiza umuhimu wa wadau mbalimbali wakiwemo wanasiasa, asasi za kiraia na kidini kuwaacha wananchi kutoa maoni yao binafsi kuhusu Katiba Mpya.
Akizungumza na Wajumbe wa Kamati
ya Katiba, Sheria na Utawala ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar leo
(Jumatatu, Septemba 17, 2012), Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph
Warioba alisema katika mikutano ya ukusanyaji wa maoni inayoendelea,
na kukusisitiza kuwa makundi na taasisi mbalimbali vitapata nafasi ya
kukutana na Tume na kutoa maoni yao.
Aidha Jaji Warioba alisema kuwa
changamoto kubwa ambayo Tume hiyo inakabiliana nayo ni wananchi
kupewa mawazo ya kuzungumza na watu wengine, jambo ambalo haliwasaidii
wananchi .
“Makundi ya watu, Taasisi za kirai
na hata vyama vya siasa vimekuwa mstari wa mbele kuwalisha wananchi
mambo ya kuzungumza “ alisisitiza Jaji Warioba.
Mwenyekiti huyo wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba aliwataka wawakilishi hao kuisaidia Tume
kuwaelimisha wananchi kuwa tayari kutoa maoni yao ya moyoni na kukataa
kabisa kupokea mawazo ya watu wengine ili katiba itakayopatikana
iwe inawakilisha mawazo yao.
Jaji Warioba alikuwa akijibu swali
la Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Naibu Spika wa Baraza la
Wawakilishi Mhe. Ali Abdalla Ali ambaye alitaka kujua changamoto ambazo
Tume inakutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yake.
Jaji Warioba amesisitiza kuwa
viongozi wa makundi mbalimbali na vyama vya siasa wana wajibu wa
kuwaelimisha wananchi kutoa maoni yao binafsi badala ya kuwaelekeza aina
ya maoni wanayopaswa kuyatoa.
Akizungumzia kuhusu muda
uliopangwa katika kutekeleza kazi hiyo, Jaji Warioba alieleza kuwa
pamoja na changamoto hiyo lakini Tume imejipanga kumaliza kazi yake
ndani ya muda iliopewa kisheria.
“Tume imejipanga kuhakikisha
ifikapo April 26 2014 katiba mpya inakuwa tayari. Kimsingi mazingira
ya hali ya kisiasa nchini yanalazimisha kuwepo na katiba mpya kabla ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ili kuweka maelewano ya kitaifa”
alifafanua.
Wajumbe hao wa Baraza la Wawakilishi wapo katika ziara ya taasisi mbalimbali za Muungano zilizopo Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Kamati hiyo Mhe. Ali Abdallah Ali amesema Wajumbe wa Kamati watatumia
uzoefu na elimu waliyoipata katika ziara yao ili kuisaidia Tume
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Wajumbe hao walipata nafasi ya
kutembelea vitengo vya Utafiti na Taarifa Rasmi (Hansard) ambapo
waliweza kuona jinsi maoni yanavyopokelewa na na kufanyiwa kazi .
Post a Comment