PAMOJA na mfumo stakabadhi mazao
ghalani kulalamikiwa na wakulima wa zao la korosho kuwa ndiyo chanzo
kikubwa cha umasiki wao bado Bodi ya Korosho imedai kuwa mfumo huo ni
mkombozi kwa wakulima.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Anna
Margareth Abdallah, alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati wa
uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa korosho kwa mwaka 2012/13, unatarajiwa
kuanza Septemba 20 mwaka huu, kama ilivyoamuliwa na mkutano mkuu wa Bodi
hiyo uliyofanyika mkoani Morogoro hivi karibuni.
Alisema haamini kama kuna mkulima anayepinga mfumo huo, kama yupo basi atakuwa anamatatizo.
“Huu mfumo hauna matatizo bali
matatizo yapo kwa baadhi ya watendaji ambao wanashindwa kuwajibika hivyo
nawataka kumaliza kasoro hizo na kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi
kuhusu mfumo huu”alisema.
Akizungumzia kuhusu upangaji wa
bei ya mkulima, Anna alisem upangaji huo umezingatia gharama halisi za
uzalishaji pamoja na bei ya soko la korosho ghafi kimataifa.
Alisema baada ya
kuzingatia maoni ya wadau, Bodi imeamuwa kuwa bei ya mkulima itakuwa Sh.
1,200 kwa kila kilo moja ya korosho ya daraja la kwanza (Standard
Grade), Sh. 960 kilo moja ya daraja la pili (Under Grade), ambayo ni sawa na asilimia 80 ya bei ya daraja la kwanza.
Anna alibainisha kuwa mkulima
atalipwa malipo ya kwanza asilimia 70 ya bei sawa na sh 850 baada ya
kufikisha korosho katika maghala ya chama cha msingi, asilimia 30 sawa
na sh 350 kwa kilo zitalipwa baada ya kuuzwa mnadani.
Aidha, mkulima atastahili malipo ya tatu ya majaaliwa endapo korosho yake itauzwa kwa bei nzuri.
Alitoa angalizo kuwa ni vyama vya ushirika tu kuwa ndivyo vitakavyoruhusiwa kukusanya korosho kutoka kwa wakulima.
Anna alisisitiza kuwa korosho
zote zitakazonunuliwa nje ya utaratibu huo zitakuwa zimepatikana kwa
njia ya magendo (kangomba), na wahusika wote watachukuliwa hatua kali za
kisheria.
Post a Comment