MAMLAKA
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetoa bei kikomo mpya
ambazo zitaanza kutumika leo nchini kote ikiwa imeshuka kwa Sh 306, kwa
lita ya petroli, Sh 192 kwa lita moja ya dizeli huku mafuta ya taa bei
ikibaki bila kubadilika.
Taarifa
iliyotolewa jana na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus
Kaguo, ilisema bei za mafuta ya petroli kwa Dar es Salaam itakuwa Sh
1,994 kwa lita moja ikiwa imeshuka kutoka Sh2,300 ya bei ya Septemba.
Alisema
mafuta ya dizeli bei yake imeshuka hadi kufikia Sh1,950 kutoka Sh2,142,
wakati mafuta ya taa yanabakia Sh1,993 kutokana na kutoingia meli yoyote
ya mafuta hayo.
Taarifa
hiyo ilisema bei hizo, zitaendelea kuongezeka kutokana na gharama za
usafirishaji kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani, ingawa kwa ujumla
katika kila eneo punguzo litakuwa ni Sh 306 na Sh 192 kwa petroli na
dizeli kwa kila lita moja.
“Kwa
mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya
petroli zitaendelea kupangwa na soko na Ewura itaendelea kuhamasisha
ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta,”alisema
na kuongeza;
“Taarifa
hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya uamuzi stahiki kuhusu
ununuzi wa bidhaa za mafuta kulingana na bei anayoiona mteja inamfaa.”
Kaguo
alisema kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli
kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziwe chini ya bei kikomo na kama
mfanyabiashara atakiuka atapewa adhabu ya kulipa Sh3 milioni.
Pia
alivitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta
katika mabango yanayoonekana bayana ili mteja afanye uchaguzi wa kununua
mafuta akiwa anajua bei halisi ya mafuta katika kituo husika.
“Wanunuzi
wanashauriwa kuhakikisha kuwa wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha
jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita
kwani stakabadhi hiyo ya malipo itatumika kama kidhibiti cha ununuzi wa
mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya
juu kuliko bei kikomo; ama endapo utakuwa umeuziwa mafuta yenye kiwango
cha ubora kisichofaa,” aliongeza Kaguo.
Hivi
karibuni Baraza la Ushindani wa Haki (FCC), lilitupilia mbali rufani ya
kampuni 13 zinazojishughulisha na uuzaji wa mafuta, zilizokuwa zinapinga
kanuni mpya ya kukokotoa bei za mafuta iliyobuniwa na Mamlaka ya
Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).
Katika
hukumu hiyo iliyotolewa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa baraza hilo, Razia
Sheikh, alisema uamuzi wa kuitupa rufani hiyo ulitokana na warufani,
kushindwa kuthibitisha madai yao kikamilifu.
Alisema
baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, baraza liliridhika kuwa
Ewura ilikuwa imefuata taratibu zote zilizowekwa kisheria, kabla ya
kutangaza kanuni mpya za kukokotoa bei za mafuta nchini.
Katika usikilizaji wa shauri hilo, Mwenyekiti Sheikh alisaidiwa na wajumbe wawili ambao ni Malima Bundala na Ali Juma.
Kampuni
zilizokata rufaa ya kupinga uamuzi wa Ewura ni pamoja na BP Tanzania
Limited, Engen Petroleum Tanzania Limited, Camel Oil Tanzania Limited,
Oilcom Tanzania Limited, Total Tanzania Limited, Gapco Tanzania Limited
na Hass Petroleum Tanzania Limited.
Nyingine
ni Orxy Oil Company Limited, MSG International Tanzania Limites, GBP
Tanzania Limited, Lake Oil Limited, Moil Tanzania Limited and Acer
Petroleum Tanzania Limited.
Pamoja na kutupilia mbali rufani hiyo, Sheikh pia aliziamuru kampuni hizo kulipa gharama za kesi.
Kwa
mujibu nyaraka za baraza hilo, gharama za mawakili wa Ewura peke yake ni
zaidi ya Sh100 milioni. Pamoja na mambo mengine, kampuni hizo
zililiomba baraza hilo kuifuta kanuni hiyo mpya kwa vigezo kuwa, Ewura
haikufikiria mambo kadhaa kabla ya kuitangaza
Post a Comment