Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

JAJI MANENTO AMKAANGA RPC IRINGA KUHUSU RIPOTI YA UCHUNGUZI KIFO CHA MWANDISHI CHANEL TEN DAUD MWANGOSI.

*ASEMA RPC KAMUHANDA ALIVUNJA SHERIA YA VYAMA VYA SIASA KUZUIA MIKUTANO YA CHADEMA, AMSHUKIA TENDWA, KAMATI YA NCHIMBI YAPINGWA.
 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgchZNk08qZUrV3MXXXS_4eH4zM_eN_4WSJNjVaMl2n3zyTjcDzBHHRjeAITvxiu-I-vNOtNXfrcv6MawShZ29-7vvVwg9rhGEVWxJxW1mV93DFFwE17B34-hF6eK9PNe809Kd0LU9mgc4/s640/6-Jaji+Kiongozi+%28mstaafu%29+pia+ni+MK+wa+Tume+ya+Haki+za+Binadamu+na+Utawala+Bora+akionyesha+taarifa+kwwa+vyombio+vya+habari+jiji.jpg
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Jaji Kiongozi (Mstaafu) Amiri Ramadhan Manento akionyesha taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam kuhusu Muhtasari  wa Taarifa ya tume yake ya Uchunguzi wa tukio lililopelekea kifo cha Mwandishi wa habari wa kituo cha Chanel Ten Daudi Mwangosi kilichotokea Septemba 2, 2012 kijijini Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa.
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, imetoa ripoti yake kuhusu mauaji ya mwandishi wa habari wa Channel Ten, Daudi Mwangosi ikisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alikiuka Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2002, huku ikiisafisha Chadema kuwa haikukosea kufanya mkutano. 
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Kiongozi Mstaafu, Amiri Manento alisema jana alipokuwa akisoma ripoti hiyo kuwa Kamuhanda alikiuka sheria hiyo Sura ya 322 kwa kuingilia kazi za OCD wa Mufindi kuzuia shughuli za Chadema wakati hakuwa mkuu wa polisi wa eneo hilo. 
Ripoti hiyo ni ya tatu kutolewa, baada ya juzi, Kamati ya Kuchunguza Mauaji hayo iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi iliyokuwa chini ya Jaji Steven Ihema kuwasilisha ripoti yake pamoja na Baraza la Habari Tanzania, kuweka hadharani ripoti yake.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni taasisi huru ya Serikali iliyoanzishwa mwaka  2001 ikiwa na majukumu ya kulinda, kutetea na kuhifadhi haki za binadamu nchini.
Jaji huyo mstaafu alisema kutokana na hilo, amri ya RPC Kamuhanda kutaka yapigwe mabomu ya machozi, haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye hakuwa na mamlaka kisheria.
"Haya ni matumizi mabaya ya mamlaka na pia ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora," alisema.

Pia Tume hiyo imeishukia hatua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa kuviandikia vyama vya siasa kuvitaka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa kuwa inakinzana na Sheria ya Takwimu Na. 1 ya mwaka 2002, inayotoa fursa kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati wa sensa.
"Vilevile, ni kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2002 kifungu cha  cha 11(a) na (b) inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake bila ya kuingiliwa,"alisema.
Jaji Manento alisema wamejiridhisha kuwa tukio lililosababisha kifo cha Mwangosi, limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
"Tume imejiridhisha kuwa polisi wamevunja haki ya kuishi, haki ya kutoteswa na kupigwa, haki ya usawa mbele ya sheria na haki ya kukusanyika kutoa maoni,"  alisema Jaji Manento.
Alisema haki hiyo ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Azimio la Kimataifa Haki za Binadamu, Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Kiraia na Kisiasa na Mkataba wa Mataifa ya Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu.
Kuhusu Chadema

Jaji Manento alisema Chadema kama chama cha siasa chenye usajili wa kudumu chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa, kinaruhusiwa kufanya maandamano na kuwa na mikutano ya kujitangaza baada ya kutoa taarifa kwa ofisa wa polisi wa eneo husika.

Alisema baada ya taarifa kutolewa chama husika kinatakiwa kipewe ulinzi na vyombo vya usalama.

Jaji Manento alisema Ibara ya 8(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza kwamba Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, aidha ibara 18(b) na (C) ya Katiba inaeleza kuwa kila mtu anayo haki ya kufanya mawasiliano yaani kutoa maoni au habari na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake.

"Haki hii imekiukwa kwa kiasi kikubwa na Jeshi la Polisi katika tukio la Kijiji cha Nyololo kwa kuwa waandishi wa habari na wafuasi wa Chadema walizuiwa na polisi kufanya shughuli zao za kupata habari na za kisiasa," alisema.

Jaji Manento alisema ukiukwaji wa misingi ya utawala bora unazorotesha au unafifisha uhuru wa habari.

Maoni na
Mapendekezo

Jaji Manento alisema tume yake imependekeza kuwa Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya, ziwe makini na vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora vinavyofanywa na mamlaka mbalimbali kwenye maeneo yao.

Jaji Manento alisema kamati hizo zihusike moja kwa moja na usalama wa wananchi na mali zao kwa kujadili masuala yote ya kiusalama kabla hatua hazijachukuliwa na vyombo vinavyotekeleza sheria.

Alisema viongozi wa Chadema na wafuasi wao waepuke malumbano na vyombo vya dola kwa kutii maagizo yanayotolewa na vyombo hivyo bila shuruti.
Jaji Manento alisema ni muhimu polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa waepuke kufanya uamuzi au vitendo vinavyoibua hisia za ubaguzi au upendeleo miongoni mwa jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria.

"Mfano Jeshi la Polisi lilizuia mikutano ya Chadema kwa sababu ya sensa wakati huohuo CCM walikuwa wakifanya uzinduzi wa kampeni huko Zanzibar,” alisema Jaji Manento na kuongeza:

"Rai ya Msajili wa Vyama vya Siasa haikuzingatiwa kwa upande wa CCM Zanzibar huku Chadema walishurutishwa na polisi kutii rai hiyo."

Ripoti ya Waziri
Nchimbi yapondwa

Siku moja baada ya kamati iliyoundwa na Dk Nchimbi kuanika ripoti yake, watu wa kada mbalimbali wametoa maoni tofauti, wengi wakiipinga kwa kile walichoeleza kuwa haikukidhi haja.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, walisema ripoti hiyo imeeleza mambo mengi, lakini haijakidhi haja kwa kuwa haikuweka wazi tukio hilo lililomuua Mwangosi.

CUF imesema kuwa ripoti iliyotolewa na Kamati, imepikwa kwa lengo la kuitetea Serikali, Polisi na Waziri husika.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top