Daniel Mjema,
Rombo
MKAZI wa Kijiji cha
Mahida Nguduni wilayani Rombo, Patrick Kimaro amependekeza watoto wa marais na
mawaziri wa sasa na wastaafu wasiteuliwe kugombea Urais wala kushika wadhifa wa
Uwaziri.
Kimaro alitoa kauli hiyo
jana katika eneo la Mamsera wakati akitoa maoni yake mbele ya Wajumbe wa Tume ya
Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Katiba Mpya iliyokuwa chini ya Profesa Mwesiga
Baregu.
“Hivi sasa dalili ya
viongozi wakuu na mawaziri kutaka kurithishana uongozi na watoto wao, kama baba
yako alishakuwa Rais au Waziri basi wewe mtoto usigombee tena Urais”alisema
Kimaro.
Hata hivyo mchango wake
huo ulionekana kutoeleweka vizuri, ambapo Profesa Baregu alimtaka afafanue kama
pendekezo hilo linaishia tu kwa watoto wa Rais ama linaenda mbali zaidi ya
hapo.
Kimaro alifafanua kuwa
pendekezo lake hilo anataka liwabane pia watoto wa watu ambao walishashika
wadhifa wa Urais na kwamba katiba imzuie Rais kuwateua kuingia katika baraza la
mawaziri.
Pia alitaka mikataba
inayoingiwa kati ya Serikali na wawekezaji iwe wazi na ichapishwe kwenye
magazeti, akisema usiri unaofanywa na serikali katika mikataba ndio chanzo cha
vitendo vya ufisadi.
Halikadhalika Kimaro
ambaye ni mwalimu kitaaluma, alipendekeza katiba ijayo imuondolee Rais kinga ya
kutoshitakiwa ili ashitakiwe anapotenda makosa kama inavyotokea kwa raia
wengine.
Pendekezo hilo liliungwa
mkono pia na Mkazi wa Mamsera Juu, Kamili Mariki huku mkazi wa eneo hilo pia
Jacob Shirima yeye akipendekeza Rais wa aina hiyo apigiwe kura ya kutokuwa na
imani naye
Post a Comment