Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), kimekutana na waandisihi wa habari makao makuu ya chama
hicho jijini Dar es Salaam jana, ambapo wajumbe wa Kamati Kuu, Profesa Abdallah
Safari na Mabere Marando, wameweka waziwazi msimamo wa chama hicho kuhusiana na
mgogoro kati ya waislamu na serikali na kukamatwa kwa Sheikh Farid huko
Zanzibar.
Wanasheria hao wa
CHADEMA wamesema kuwa kitendo cha serikali kumnyima dhamana Sheikh Ponda ni
kinyume cha katiba na kwamba Chadema kama chama kinachojiandaa kuchukua dola,
hakiwezi kuvumilia kuona haki za raia zikivunjwa.
“Tunaweza kuwa miongoni
mwetu, wapo watu wanaomchukia Sheikh Ponda, lakini hatuwezi kuficha ukweli
kwamba Sheikh Ponda kama raia wa Jamhuri ya Muungano au mkazi wa Jamhuri hii,
anayo haki ya kusikilizwa na kupewa dhamana. Makosa ambayo Sheikh Ponda
ameshitakiwa yanadhaminika kwa mujibu wa sheria, hivyo ni makosa kwa serikali
kufanya hila kumnyima dhamana kiongozi huyu wa kidini,” ameeleza Marando katika
mkutano huo.
Marando alifika mbali
zaidi kwa kusema tatizo lililopo sasa kati ya serikali na waislamu, limetokana
na hatua ya serikali kuwalazimisha waislamu wote kuwa waumini wa Bakwata, chombo
ambacho wengi wanakiona kinatumika kuwakandamiza.
Naye Profesa Safari
alionya matumizi ya nguvu za kijeshi yanayotumiwa na serikali kwa kisingizio cha
kulinda amani, huku akieleza kuwa matumizi ya kijeshi siyo suluhu ya kutatua
matatizo yaliopo.
Kuhusu kukamatwa kwa
Sheikh Faridi na kumzuia kwa siku tatu, wanasheria hao wamesisitiza kuwa kitendo
hicho hakikubaliki.
“Kitendo cha kumkamata
na kumshikiria Sheikh Faridi, huku serikali na vyombo vyake vikisema havihusiki,
wakati ukweli ni kuwa alikuwa anashikiliwa na watu wa USALAMA wa TAIFA, ni
uharamia mkubwa unaopaswa kulaaniwa na wote wanaolitakia mema taifa hili,”
ameeleza Marando.
Kuhusu uvunjwaji wa
makanisa, Profesa Safari amesema CHADEMA kimelaani hatua hiyo iliyotokana na
wananchi kujichukulia sheria mkononi. Amewataka waislamu kuvuta
subira.
Hata hivyo, Profesa
Safari amesena matatizo yanayotokea sasa, yameletwa na CCM kutokana na hatua yao
ya kuwatumia baadhi ya waislamu kupandikiza mbegu ya udini
nchini.
Post a Comment