Moja ya hadithi za Mtume Muhammad S.A. W ni
pale Mtume Muhammad alipokuwa msikitini na maswahaba wake. Mara akaingia
msikitini mtu wa kabila la Mabedui na kuanza kukojoa. Maswahaba wa Mtume
wakasimama kwa hamaki kutaka kumwadhibu Bedui
yule.
Mtume akawasihi maswahaba wake wasifanye
jambo lolote litakalomdhuru Bedui yule. Hapo ikavutwa subira. Bedui yule
akakojoa na akamaliza. Mtume Muhammad alipomuhoji Bedui yule ikabainika kuwa
alikuwa ni mtu wa hovyo na wala hakujua kuwa alimokuwa ni msikitini. Bedui yule
akaelimishwa, akaelewa. Akarudi kwenye ustaarabu.
Ndio mkojo ule ulifutwa kwa maji na amani
ikawepo. Wahenga walinena; Subira yavuta heri. Siku zote, hamaki si jambo jema.
Kwa kutanguliza subira na kutumia hekima Mtume Muhammad aliivuta heri na
kuepusha shari.
Maana, kama Mtume alisingewaasa maswahaba
wake kuvuta subira, basi, makubwa matatu yangetokea ndani ya msikiti ule; Mosi,
zingezuka vurugu na watu kuumizana na hata kutoana roho. Pili, mkojo wa Bedui
yule ungesambaa msikitini kwa vile alishaanza kukojoa na isingekuwa rahisi kwake
kukatisha mkojo wake. Tatu, Mkojo una madhara ya kiafya
pia.
Naam, kwa mwanadamu, ni muhimu kuwa na
subra na kutafakari kabla ya kufanya maamuzi. Kwa ndugu zangu Waislamu, tunaona
Mtume Muhammad ameweza kuonyesha hilo.
Na kwa ndugu zangu Wakristo, kuna mifano pia
ya Yesu Kristo kuonyesha subra.
Ndio, Uislamu, kama ilivyo kwa Ukristo na
dini nyingi za humu duniani, msingi wake ni amani na upendo. Kitendo cha mtoto
yule wa Mbagala kukojolea korani kitazamwe kwa sura ya kitendo kilichofanywa na
mtoto .
Na kama ilivyokuwa kwa Bedui yule, kama pale
Mbagala subira na hekima vingetangulizwa, basi, yumkini tungebaini kuwa mtoto
yule hakujua madhara ya kitendo chake. Naye angekanywa kama tuwakanyavyo watoto
wetu. Na hata kitendo hicho kingefanywa na mtu mzima, bado tulikuwa na haja ya
kutanguliza subira na hekima kumhoji aliyetenda, yaweza akawa kama Bedui yule
kwenye msikiti alimosali Mtume na maswahaba wake.
Na kwa kuangalia picha zile za Mbagala
naiona hatari iliyopo sasa, kuwa tuna vijana wengi wasio na kazi; Wakristo kwa
Waislamu. Vijana wasio na dogo. Ni kama moto uliofifia. Akipatikana kwa
kuchochea kuni wanalipuka.
Ni vijana wanaopatikana wakati wowote na
mahali popote. Hata jambo likianza saa tatu asubuhi wao wapo. Hawana ofisi wala
bosi wa kumwomba ruhusa ya kwenda kuandamana na kurusha mawe. Ndio hawa
wanaonekana wamevaa ‘ Kata kiuno’ na wengi wao hawajahi hata kuingia misikitini
au makanisani.
Inakuawaje kijana wa kweli wa Kiislamu
achome kanisa na kuiba kompyuta. Inakuawaje kijana na muumini wa kweli wa
Kiislamu aonekane saa mchana wa jua kali akivamia baa na kukimbia na kreti za
bia? Ni maswali yanayotutaka tutafakari kwa makini.
Maana, ninavyoamini mimi, uchumi na elimu
duni ndio hasa vinavyochochea vurugu za kijamii, iwe za kidini au kisiasa, na
hususan inapohusisha vijana. Vijana wetu hawana misingi mizuri ya elimu, na
wengi hawana ajira pia. Haya ni sawa na makombora yasiyo na gharama kubwa kuweza
kutumiwa na wanasiasa wasio waadilifu na hata viongozi wa kidini wenye mitazamo
mikali. Ni makombora yaliyoanza kutulipukia. Tuliziona ishara,
tukazipuuzia.
Leo Kuna vijana watakaotumiwa au kutumia
fursa hiyo kutenda maovu kwa kisingizio cha dini. Ni hawa wataoshiriki kuchafua
taswira za dini husika pia. Tujiadhari, kabla ya hatari kubwa inayotujia.
Hatujachelewa.
Na hilo ni Neno La
Leo.
Maggid
Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765
http://mjengwablog.com
http://mjengwablog.com
Post a Comment