Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiongea na wazee waishio Katumbasongwe, kando ya Ziwa Nyasa ndani ya Wilayani Kyela, Mkoani Mbeya.
Wakazi wa Katumbasongwe walimiminika kwa wingi kumsikiliza Mhe. Membe.
Wazee wa Katumbasongwe wakinyoosha mikono kujitambulisha umri wao wakati wa Mkutano wao na Waziri Membe uliofanyika jana Wilayani Kyela, Mkoani Mbeya. Waziri Membe alikuwa Mkoani humo kwa ziara ya siku mbili ambapo alitembelea maeneo na makazi ya wananchi waishio ufukweni mwa Ziwa Nyasa.
WAZIRI MEMBE AKIWA MATEMA
Waziri Membe akiongea na wakazi wa Matema, Wilayani Kyela ambapo aliwasihi waendelee na shughuli zao za kujiletea maendeleo. Aidha, Mhe. Membe alisema Serikali inajitahidi kadri iwezavyo kutafuta suluhisho la mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi.
Wakazi wa Matema, waishio katika ufukwe wa Ziwa Nyasa, Wilayani Kyela wakimsikiliza Waziri Membe alipowatembelea jana.
Waziri Membe (hayupo pichani) pia alipata fursa ya kuongea na wazee wa Matema ikiwa ni sehemu ya mwisho wa ziara yake ya siku mbili Mkoani Mbeya. Katika mazungumzo yake na wazee hao, Waziri Membe aliwaeleza kuwa ziara hii ni sehemu ya kukusanya ushahidi muhimu kutokana na maelezo ya historia watakazochangia hususan tangu enzi ya ukoloni kuhusu Ziwa Nyasa.
“Hakuna mtu kusema Ziwa lote ni lake,” alisema Waziri Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kuongeza kuwa lazima kuwe na dhamana inayoonesha mipaka, kanuni na sheria ili kuondoa wingu la shaka yoyote hususan kwa Taifa lolote na wananchi wake.
Aidha, Waziri Membe aliongeza kuwa Serikali ina jukumu la kumaliza mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati yake na Malawi, na jitihada muhimu zinafanyika ili kuumaliza kwa amani na utulivu.
Waziri Membe aliyasema hayo jana mjini Mbeya alipokuwa akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya, ambayo hiko chini ya Uenyekiti wa Mhe. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Akiainisha jitihada hizo, Mhe. Membe alisema kuwa Kamati ya Taifa inayojumuisha timu ya wanasheria na wataalamu wa mipaka imeundwa kwa madhumuni ya kutatua mgogoro huo na timu ya Malawi. Pia kuna timu ya Kikosi Kazi chini ya Waziri Membe, ambayo jukumu lake ni kukusanya nyaraka na kumbukumbu muhimu za mgogoro huo tangu miaka ya 1890 hadi leo.
Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri, baada ya Kikosi Kazi kumaliza kazi yake, kitawasilisha rasmi nyaraka kwa Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete na kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili hatua muhimu za Serikali zifanyiwe kazi.
Aidha, Mhe. Waziri alisema kuwa kuna umuhimu wa kutumia vyombo vingine ili kusaidia kutatua tatizo hili kama vile Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Baraza la Uongozi wa Wakuu wa Afrika la SADC (Leadership Forum – SADC), Umoja wa Afrika (AU) na ikiwezekana kuipeleka kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).
Kwa upande wake, Mhe. Kandoro alisema kuwa hali Mkoani Mbeya ni tulivu na kwamba maisha yanaendelea vizuri. Alikanusha kuhusu taarifa zisizo za kweli zilizotangazwa kwenye mitandao kwamba mabomu yamerushwa Mkoani Mbeya hususan kwenye maeneo ya mpaka wa Ziwa Nyasa.
Aidha, Mkuu wa Mkoa aligusia ukamatwaji wa wavuvi na mitumbwi kutoka Malawi ambayo ilikuja ufukweni mwa Tanzania, na kusisitiza kuwa hatua muhimu zilichukuliwa kwa kuzingatia na kuheshimu ujirani mwema.
Katika ziara yake, Waziri Membe pia alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Bibi Margareth Malenga, ambapo alipata taarifa kuhusu hali ya ulinzi na usalama katika mipaka ya Ziwa Nyasa, pamoja na mahusiano kati ya Wilaya ya Kyela na Wilaya ya Karonga nchini Malawi. Wilaya ya Kyela iko mpakani mwa Wilaya ya Karonga nchini Malawi.
Akisoma taarifa ya Wilaya yake, Bibi Malenga alisema “hali ya mipaka ni tulivu na kueleza kuwa hivi karibuni, mnamo tarehe 11 Oktoba, 2012 walipata ugeni wa Mhe. Mganda Chiume, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi na ujumbe wake akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Karonga nchini humo.”
Kwa mujibu wa Bibi Malenga, lengo la ziara ya Waziri Chiume lilikuwa ni kukagua mpaka wa Ziwa Nyasa kwa upande wao lakini waliona ni vizuri waje Wilayani Kyela kuona hali ya mahusiano ilivyo baina ya wananchi wa upande wa Kyela na wale wa Karonga.
Akiendelea na ziara yake, Waziri Membe pia alipata fursa ya kuongea na wazee alipotembelea maeneo ya Katumbasongwe na Matema yaliyopo katika ufukwe wa Ziwa Nyasa.
“Tumekuja hapa kupata ushahidi wenu wa kihistoria tangu enzi ya ukoloni ambao utazisaidia Kamati zilizoteuliwa kutatua mgogoro huu ili ziweze kukusanya kumbukumbu na kufanya kazi ipasavyo,” alisema Waziri Membe.
Aidha, Waziri Membe aliwahakikishia amani na utulivu wananchi wa Kyela, na kusema kuwa “Serikali inajitahidi kadri iwezavyo kutatua mgogoro huu kwa njia ya kidiplomasia na hata kama ikiwezekana kwenda ICJ.”
Aidha, Mhe. Membe kabla ya kumaliza ziara yake ya siku mbili Mkoani Mbeya jana, pia alitembelea mipaka ya Kasumulu Katumbasongwe na Matema kwenye ufukwe wa Ziwa Nyasa, katika Wilaya ya Kyela ambapo alizungumza kwa kina na wananchi waishio ufukweni mwa Ziwa hilo.