MLEZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa
mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya, Thomas Nyimbo, ametangaza kujivua uanachama wa
chama hicho kwa madai ya kuchoshwa na siasa za ‘Umangimeza’ ndani ya vyama vya
siasa hapa nchini.
Nyimbo ambaye amewahi kuwa mbunge wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) kwa miaka 10 katika Jimbo la Njombe Magharibi kabla ya kukimbilia Chadema
mwaka 2010, amesema hivi sasa atabaki kuwa mwanasiasa huru asiyefungamana na
vyama.
Akitoa taarifa ya kuachana na siasa ndani ya vyama jana,
Jijini hapa, huku akiwa ameambatana na mkewe Mary Mwenga, alisema amechukua
uamuzi huo baada ya kuona siasa za kushabikia vyama hazina tija kwa watanzania
walio wengi na badala yake zinawanufaisha viongozi wachahe wanaojineemesha wao
wenyewe kwa kutumia jasho la wananchi.
Akifafanua zaidi alisema alichojiuzulu ni siasa za vyama,
lakini sio siasa, huku akitamba kuwa yeye alizaliwa akiwa ni mwanasiasa,
kiongozi na mtu ambaye mawazo yake yanahitajika kwa ajili ya maendeleo ya nchi
yake, hivyo atabaki kuwa mwanasiasa asiyekuwa na chama cha
siasa.
Katika taarifa hiyo aliyoitoa kwa vyombo vya habari
mithiri ya Mhadhara, Nyimbo alitumia zaidi ya saa moja na nusu kuelezea
mustakabali wa taifa na vijana kutokana na vyama vya siasa kuelekea
kuwatumbukiza kwenye machafuko.
“Nimeachana na Chadema baada ya kubaini kuwa siasa za
vyama havina tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla na ni wakati huu sasa wa
kuachana na dhana ya vyama vya siasa vituandalie sera na tunahitaji sasa itungwe
sera ya kitaifa ambayo mgombe inabidi atueleze tukimchagua ataitekeleza vipi”
alisema Nyimbo.
Alisema hata nchi zenye wigo mpana wa Demokrasia kama
Marekani ambao hivi sasa wapo kwenye mchakato wa uchaguzi Mkuu huwezi kuwasikia
wagombea wake wakisifia vyama vyao, bali wanawaeleza wananchi wa Marekani
watatekeleza vipi sera ya nchi yao .
Alisema kuwa ikiwa katiba mpya inayoandaliwa hivi sasa
itakuruhusu mgombea huru, atakuwa tayari kugombea ubunge tena kwenye jimbo lake
la Njombe Magharibi, lakini kama katiba hiyo itazuia fursa hiyo hatogomea tena
wadhifa huo maisha yake yote.
Aliongeza kuwa baada ya kupatikana kwa katiba mpya, inabidi itungwe sera ya Taifa itakayolindwa kisheria, ambayo kila chama kitakachofanikiwa kuingia madarakani kilazimike kuifuata badala ya ilivyo sasa vyama vinaogelea hovyo.
Alisema kuwa ndoto za kuwa mwanasiasa huru alikuwa nazo tangu zamani, na ndiyo sababu katika mabango yake ya kuhamasisha achaguliwe wakati akigombea ubunge kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, alikuwa na kauli mbiu ya ‘Mtu kwanza, chama baadaye.
Alisema kuwa ikiwa katiba mpya inayoandaliwa hivi sasa itakuruhusu mgombea huru, atakuwa tayari kugombea ubunge tena kwenye jimbo lake la Njombe Magharibi, lakini kama katiba hiyo itazuia fursa hiyo hatogomea tena wadhifa huo maisha yake yote.
“Nitapenda kushauriana na watanzania wanaopenda maendeleo ya taifa letu nje ya mlolongo wa vyama, hivyo hata kama naipenda vipi Chadema, nalazimika kuresighn (kujiuzulu) uanachama ili niweze kutimiza azma hiyo,” alisema Nyimbo.
Kilicho mkimbiza Chadema.
Alisema ameamua kujiondoa ndani ya chama hicho baada ya
kubaini kuwa kinaenda kinyume na malengo yake kama kinavyojipambanua mbele za
watu.
Alisema licha ya kuwaaminisha wananchi, hususani vijana
kuwa ndio chama chenye kuleta mabadiliko ya kweli,lakini viongozi wake wa daraja
la juu akiwataja Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dk. Wilbroad Slaa
wamekuwa wakijinufaisha binafsi.
Alisema viongozi hao pia wamekuwa si watu wa kushaurika
ndani ya chama hicho, lakini kibaya zaidi ni kuendesha siasa katika mfumo mbaya
wa kushawishi na kuaminisha bila kuwa na suluhisho (Mob
Politics).
Alisema siasa za namna hiyo ni hatari kwa taifa kwa kuwa
baada ya kuungwa mkono kwa kiwango cha juu na kundi la vijana kwa imani ya
kukombolewa pale watakapofanikiwa kuingia madarakani na kushindwa kuwatimizia
kutazua vurugu.
Kuhusu CCM.
Nyimbo alidai kuwa chama hicho kinajimaliza chenyewe
kutokana na kuacha suala la rushwa kwenye chaguzi zake za ndani kuwa ndio kigezo
muhimu cha kuwapata viongozi wake.
Hata hivyo alisema ili tatizo hilo limalizike ni wananchi
wenyewe kuamua kuikataa rushwa kwa kupokea rushwa isiyoleta matunda kwani
wakifanya hivyo watakuwa wamemaliza tatizo hilo .
“Mfano wewe ukipokea rushwa na kuamua kufanya tofauti na
aliyekuhonga kwa kuwa baadaye atakuwa hajapata kile alichotaka kukinunua toka
kwako, unafikiri kesho atarudia”.
Vijana.
Amewataka vijana nchini kupigania maslahi yao kwa mtazamo hasi wenye kuleta mstakabali mzuri wa Taifa, badala ya kufikiri kuwa mabadiliko ni kuiondoa CCM madarakani na kuiweka Chadema.
Alisema kuna mambo mengi ya msingi ambayo kama vinana
wanapaswa kuwahoji viongozi waliowachagua kama wameyatekeleeza , ikiwemo
kupigania katiba mpya kuwa na sera ya inayoweza kuruhusu mgombea binafsi kwa
kuwa huko wanaweza kupata viongozi bora.
Kujiengua kwa Nyimbo linaweza kuwa ni pigo kubwa kwa
Chadema, kwani baada ya kujiunga na chama hicho mwaka 2010, alikuwa ni mlezi wa
Chadema kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, huku pia akiwa ni miongoni mwa
wanasiasa wenye mvuto na wahamasishaji wazuri wa Chadema katika mkoa mpya wa
Njombe.
-Awaasa vijana kuwa mabadiliko ndani ya Tanzania si
kuiondoa CCM na kuiweka Chadema.
|
Post a Comment