Mwenyekiti mpya wa CCM mkoa wa Singida Mgana Izumbe Msindai akitoa shukurani zake kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi (hawapo kwenye picha) kwa kumpa kura za kutosha.Kulia ni mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone.
Mwenyekiti mpya wa CCM mkoa wa Singida Mgana Izumbe Msindai(kulia) akipongezwa na mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa CCM mkoa wa Singida Mkutano huo ulifanyikia kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo cha uhazili mjini Singida.
Kikundi cha burudani cha Nyota njema cha Utemini mjini Singida kikitoa burudani muda mfupi kabla mkutano wa uchaguzi wa CCM mkoa haujaanza.(Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Mkutano Mkuu wa uchaguzi CCM mkoa wa Singida umemchagua Mgana Izumbe Msindai kuwa mwenyekiti wake kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Msindai maarufu kwa jina la CRDB benki, ameshinda kiti hicho baada ya kupata kura 673 dhidi ya 41 za mpinzani wake Amari Rai.
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Joramu Allute, ameangukia pua mapema baada ya kupata kura 194 kwenye duru ya kwanza.
Baada ya kupata kura ambazo hazikutosha mzee Allute aliondoka wakati mkutano huo u kiwa unaendelea.
Kura zilizopigwa awali, Msindai aliongoza kwa kupata kura 407 na Amani Rai kuambulia 238.
Zoezi hilo lilirudiwa kwa kile kilichodaiwa kuwa hakuna mgombe aliyepata nusu ya kura za wajumbe kama inavyoainishwa kwenye katiba ya CCM.
Rai baada ya kubaini kuwa sio rahisi kumbwaga Msindai, aliomba kujitoa na kwamba kura alizopata, apewe Msindai kwa madai anamheshimu sana.
Hata hivyo, msimamizi wa uchaguzi huo makamu mwenyekiti wa pili CCM Tanzania bara John Chiligati, alitupilia mbali ombo la Rai kwa madai kwamba katiba ya CCM hairuhusu mgombea kujitoa katika hatua iliyofikiwa.
Kura ziliporudiwa mara ya pili kama ilivyotarajiwa Msindai aliibuka na ushindi.
Katika hatua nyingine, msimamizi wa uchaguzi huo Chiligati,aliwatangaza washindi wawili kutoka kila wilaya kuwa wajumbe wa halmashauri kuu mkoa ambao ni Duda Juma Mughenyi na Sara Abel Mkumbo kutoka manispaa ya Singida.
Alitaja wengine kuwa ni Manase Sabasaba na Abdala Ghamayu kutoka Singida vijijini, Chambo Yahaya na Omari Mohammede(Ikungi), Hamisi Kinota na Lyanga Timoth (Iramba), Rehema Cizuma na Amosi Budodi (Manyoni) na kutoka wilaya mpya ya Mkalamani William Nyalandu na Mlingi Salima Selemani.