Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Donan Mmbando na
Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), Bw. Klaus Brendes wakipewa
maelezo na Meneja wa Mradi Bi. Grace Mwang'onda jinsi watakavyokata utepe
kuzindua Jengo la huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD) katika hospitali ya Cardinal
Rugambwa.
Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani
(KfW) Bw. Klaus Brendes akifungua Kitambaa kuashiria ufunguzi wa jengo hilo la
huduma kwa wagonjwa wa ndani (OPD) katika hospitali ya Cardinal Rugambwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya
Huduma za Jamii (CSSC), Bw. Peter Maduki akisoma ripoti fupi ya mradi kwa mgeni
rasmi Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Donan Mmbando ambaye alimwakilisha
waziri wa afya na ustawi wa jamii Dk. Hussein Mwinyi
Meneja
wa Mradi Bi. Grace Mwang’onda akiongea na waandishi wa habari mara baada ya
uzinduzi huo.Kwa picha na habari zaidi www.afyamtandaonetwork.ning. com, www.cssc.or.tz
---
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema itaendelea kuboresha zaidi
ushirikiano na sekta binafsi yakiwemo mashirika ya dini, kwa kuboresha zaidi
mazingira yatakayowezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika utoaji wa
Huduma za afya.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa afya na ustawi wa jamii Dk. Hussen Mwinyi katika hotuba
iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Donan Mmbando
wakati wa ufunguzi wa jengo jipya linalohudumia wagonjwa wa nje (OPD)
liliojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya maendeleo ya
Ujerumani iitwayo KfW na kusimamiwa na Tume ya Kikristo ya Huduma za jamii
(CSSC) kwa lengo la kuboresha Huduma ya afya na elimu
nchini.
Dk.
Mwinyi amesema uboreshaji wa mazingira ambao serikali inatekeleza ni pamoja na
kutoa ruzuku kadiri hali ya fedha inavyoruhusu, kushirikisha sekta binafsi
katika kupanga, kutekeleza na kutathimini utoaji wa Huduma za afya
nchini.
Aidha
Dk. Mwinyi amebainisha kuwa kwa sasa serikali inatumia hospitali Teule za wilaya
zinazomilikiwa na Kanisa 39 na hospitali mbili kama hospitali za rufaa za Kanda.
Dk. Mwinyi amefafanua kuwa hivi karibuni Serikali imezipandisha hadhi hospitali
10 za mashirika ya dini na kuzifanya hospitali za rufaa ngazi ya
mkoa.
Akiwasilisha ripoti fupi ya ujenzi wa jengo
hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa CSSC, Bw. Peter Maduki amesema kuwa ujenzi wa jengo
hilo katika hospitali ya Cardinal Rugambwa ulianza rasmi mwaka 2008, chini ya
usimamizi wa CSSC na mshauri msanifu wa ujenzi kutoka Kampuni ya Landplan Icon
Architects wa Dar es salam na Mkandarasi M/S Build All
Contractors.
Bw.
Maduki amefafanua kuwa kazi ya kukamilisha ujenzi huo imegharimu kiasi cha
shilingi za Kitanzania milioni 900 na fedha hizo zote zimetolewa na serikali ya
Ujerumani.
Akielezea jengo hilo la kisasa, Bw. Maduki
amesema kuwa lina vyumba vya matibabu kulingana na mwongozo wa wizara ya Afya,
vyumba hivyo ni kwa ajili ya Huduma za maabara, upasuaji mdogo, dawa, sindano,
ushauri, mikutano uchunguzi (scanning) na mapumziko Aidha vyumba vingine ni kwa
ajili ya mazoezi ya viungo, ofisi na sehemu kubwa kwa ajili ya
kusubiria.
Naye
Mkurugenzi wa Benki ya maendeleo ya Ujerumani KfW, Bw. Klaus Brendes akizungumza
katika ufunguzi huo kwa niaba ya balozi wa Ujerumani nchini, amesema serikali ya
Ujerumani inafadhili miradi mingi ya maendeleo Tanzania kama vile; maji, afya,
elimu nk. inafarijika kuona miradi hii inafanikiwa vizuri ukiwemo mradi huo wa
ujenzi wa jengo hilo la hospitali ya Cardinal Rugambwa, na kuahidi kuendelea
kusaidia, miradi mingine ya maendeleo.
Akitoa
neno la shukrani Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Dar es salaam ambao ndiyo
wamiliki wa hospitali hiyo, Mhashamu Eusebius Nzingilwa amewashukuru wafadhili,
serikali na CSSC kwa jitahada kubwa walizoonyesha katika ujenzi
huo.
“Tunashukuru Serikali ya Tanzania kwa
ushirikiano na msaada mkubwa wanatoa katika kuboresha huduma za afya nchini pia
wafadhili kwa msaada wao wa kifedha pamoja na CSSC kwa utendaji wenu wa kazi
katika kusimamia ujenzi huo” amesema Askofu Nzigilwa.
Askofu
Nzigilwa amebainisha kuwa Huduma za afya ambazo zinatolewa na Makanisa ni kwa
ajili ya watu wote bila bila kubagua dini ya mtu yeyote yule, hivyo amewataka
watumishi wa hospitali ya Cardinal Rugambwa kuendelea kutoa Huduma bora yenye
kujaa tunu ya upendo kwa wagonjwa.
Hospitali ya Cardinal Rugambwa inamilikiwa na
Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, ilianza kama zahanati na baadaye
kupandishwa na hadhi na kuwa hospitali mwaka 2005. Inahudumia watu kutoka
manispaa ya Ilala na maeneo mbalimbali kama vile Kisarawe, Mkuranga pia na watu
wengine kutoka maeneo ya Unguja na Pemba.
Kwa
habari zaidi tembelea; www.afyamtandaonetwork.ning. com;
www.cssc.or.tz
Post a Comment