Ninaandika kwa masikitiko sana, jinsi ambavyo Watanzania tumelichukulia swala la machafuko yaliyotokea na kufikia hatua ya makanisa kuchomwa moto, misikiti kunajisiwa na askari, vurugu na matamko mengi mbalimbali. Wapo wanaofanya mzaha, wapo walioanzisha ligi waziwazi na kwenye mitandao, wapo wanaonyamaza kimya lakini wana hasira balaa n.k. Kati ya mambo yasiyohitaji mzaha, mashindano, hamaki, ghadhabu ni swala la kutoweka kwa upendo uliokuwepo kati ya watu wawili. Upendo kati ya Watanzania umejengwa kwa misingi imara kabla hata hawa watu weupe hawajaja kwetu, tulikuwa weusi lakini mioyo yetu ilikuwa myeupe pe. Bwana mmoja alisema hatukuwahi kugombea matambiko, hata kama tulipigana vita vya kikabila mwisho wa siku tulibaki kuwa watani, Wapare kwa Wachaga, Wasukuma kwa Wazaramo, Wahaya kwa Wakurya n.k. Ukifanya uchunguzi utakuta kuwa hawa wanaohitana watani walishawahi kupigana vita wakigombea mifugo, ardhi n.k. Mwalimu aliposhirikiana na wenzake kudai uhuru wa Tanganyika walikaa pamoja na kukubali kuendelea kujenga ule msingi ulioanzishwa na jamii mbalimbali kabla ya kuja weupe. Wakawaza na kuwazua kuondoa hata zile chembe chembe zilizopunguza upendo kati ya jamii moja na nyingine. Mwalimu aliyeonekana na kutajwa zaidi kwani ndie aliyekabidhiwa jukumu hili la kuwa kiranja wa kulinda na kuuimarisha upendo wetu. Pamoja na madhaifu ya Muungano tunayoyafahamu lakini sababu na hoja(motive) za msingi za kuanzisha muungano ni kuongeza upendo, mimi binafsi ndivyo ninavyoamini. Katika kujenga upendo huu mwalimu alishirikiana na baadhi ya wakuu wa makabila mbalimbali ya Tanzania, viongozi mbalimbali wa dini na madhehebu yake(Mashekhe na Maaskofu). Wakati mwingine Mwalimu na waliokuwa nyuma yake walitumia nguvu kulinda upendo wetu, na wengine kwa haraka wanamwita Dikteta. Leo hii tumeanza kufanya mzaha na upendo ulioasisiwa na wahenga, tunalumbana, tunachochea gadhabu, tunajitahidi kupunguza upendo na kuchochea chuki kwa bidii tukitumia gharama kubwa, eti! Ili iwe nini? Nilipotafakari nikaona nijiulize maswali kadhaa. Hivi! Sisi Waislamu tunapendana zaidi wenyewe kwa wenyewe leo kuliko miaka ya 70 na 80? Hivi sisi Wakristo tunapendana zaidi wenyewe kwa wenyewe leo kuliko miaka ya 70 na 80? Mbona leo madhehebu yanaongezeka kila uchao mtaa mmoja nyumba za ibada 7 na cha ajabu Biblia ile ile na Mbinguni wanakotaka kwenda kule kule lakini hawawezi kukaa pamoja, wanapigana vijembe; hapo kuna upendo kweli? Unajua, kabla ya kuanza kuwaza upendo wa kijiji kizima twapaswa kutakari upendo katika familia kwanza. Waislamu pia, siku za nyuma tuliweza kukaa kwa pamoja lakini leo hii kila dhehebu lina yake na kila mmoja anajifanya mjuaji kuliko mwenzake. Kama Mwislamu huelewani na unamchukia Mwislamu mwenzako huyu asiye Mwislamu utampendaje? Wewe Mkristo humpendi Mkristo mwenzako, huyo asie Mkristo unawezaje kumpenda? Matamko yametolewa mengi yenye jumbe mahsusi, sina ugonvi nazo, lakini nilitegemea viongozi hawa wa dini waanze kutoa matamko juu ya chuki zilizoko kwenye dini na madhehebu yao kwanza na wapendekeze namna ya kuondoa hizo chuki na mipasuko, ndipo waweze kumnyooshea mwenzake wa dini nyingine kidole. Amani ni tunda linalozaliwa mahali penye upendo; nina maana chuki ikishaingia mahali hakuna amani tena. Tanzania ya leo kuna harakati zinazoendelea kwa nguvu sana kuhakikisha UPENDO unapungua na kutoweka kabisa. Vikundi vya dini kwa dini nyingine, dhehebu moja kwa dhehebu jingine, chama kimoja cha siasa kujitahidi kwa nguvu kujenga chuki juu ya chama kingine na taasisi za umma na serikali za mitaa na kuu, taasisi moja kujenga chuki juu ya taasisi nyingine, mtu mmoja mmoja kwa mtu mwingine, n.k. Vinatumika vyombo vya habari(redio, magazeti, mitandao ya jamii, tovuti, tv n.k), hizo gharama zote na miguvu yote kwa nini tusitumie kujenga upendo? Watu twasimama kwenye majukwaa tunahubiri chuki, Wachungaji, Mashekhe wasimama Misikitini na makanisani badala ya kuhubiri upendo wanahubiri chuki, na sisi tunawatazama tu na wakati mwingine kuwashangilia. Tukumbuke kujenga nyumba ni ghali sana, lakini kubomoa unahitaji nguvu kidogo na muda mfupi tu. Ukiangalia hata kwenye uchumi, tafsiri yangu ya kuongezeka kwa pengo kati ya walionacho na wasionacho ni matokeo ya chuki ambayo itaendelea kuongeza chuki. Kwa sababu ya chuki mtu mmoja au kikundi cha watu wachache kinazuia mianya yote ya jamii ya wengi kunufaika na uchumi wa nchi yao, badala yake wachache ndio wanaonufaika na rasilimali za taifa. Kwa hiyo hawa wachache wenye fursa ya kuweza kuzuia wengine kiuchumi hawawezi kuwazuia kabla ya kuwachukia, wakishakusanya mali nyingi wakati hawa wengi wanateseka, ipo siku watagundua kuwa walichukiwa na wale waliowapa dhamana wakawazuia kufaidi kwa usawa rasilimali za Taifa. Nao hawa wengi wataanza kuwachukia hawa wachache waliowachukia mwanzo na kuwanyima hata mkate wao wa kila siku. Chuki hizi mwisho wake zitazaa ubaguzi, fitina, fujo na mwisho uuaji. Uuaji wa mtu mmoja, utazaa uuaji wa watu wawili, kasha kumi na mwisho mauaji ya kimbari. Chuki huzaa chuki. Watanzania, tusiiachie serikali kupigana kulinda upendo na amani ya jamii ya Tanzania, nasi kukaa kando. Upendo huu ni kwa manufaa yetu wananchi mmoja mmoja, kabla ya kuwa kwa manufaa ya serikali na vyombo vyake. Tuulinde, tuuenzi na kuupalilia upendo wa jamii za Tazania kwa gharama yeyote. Nasema na nasisitiza, HAKUNA AMANI PASIPO NA UPENDO.
chanzo: Maggid Mjengwa
Post a Comment