TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametaka wananchi wa Kenya wapewe nafasi ya
kuamua ni viongozi gani wanawataka katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika
Machi mwakani.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa wananchi
wa Kenya wanayo haki ya msingi kabisa kuamua hatma ya taifa lao katika Uchaguzi
Mkuu huo.
Mheshimiwa Rais aliyasema hayo leo Oktoba
21, 2012 alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa wabunge wa vyama
mbalimbali vya siasa vya nchini Kenya uliomtembelea Ikulu jijini Dar es
salaam.
Ujumbe huo uliongozwa na Naibu Waziri Mkuu
wa Kenya na Waziri wa Fedha Mhe. Uhuru Kenyatta ambaye pia ni Mwenyekiti wa
chama cha TNA na Waziri wa Sheria wa Kenya Mhe Eugene Wamalwa wa chama cha New
Ford Kenya. Wote wawili ni wagombea wa nafasi ya Urais katika uchaguzi
ujao.
Wengine katika msafara huo walikuwa ni
Naibu Waziri wa Afya na mbunge wa Mombasa Mhe. Kambi Kazungu, Mbunge wa
kuteuliwa wa chama cha TNA Bi Rachel Shebesh, na Mbunge wa Kajiado kwa tiketi
ya TNA Moses ole Sakuda na mbunge wa zamani Mhe Abdullahi
Alli.
Rais Kikwete aliwapongeza kwa kuamua
kufanya kazi kwa pamoja licha ya kuwa watakuwa washindani katika kinyang’anyiro
cha uchaguzi mkuu huo.
Mheshimiwa Rais ameitakia heri nchi ya
Kenya katika uchaguzi huo ujao, na kusisitiza kwamba nchi hiyo ya jirani ina
umuhimu katika mustakabali wa kiuchumi kwa nchi za Afrika
Mashariki.
Rais Kikwete wakati huo akiwa Mwenyekiti wa
Umoja wa Afrika (AU) alikuwa miongoni mwa viongozi walioshughulika sana kutafuta
ufumbuzi wa ghasia na vurugu zilizozuka kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007
nchini Kenya.
Rais Kikwete alikaa siku tatu nchini Kenya
akitafuta usuluhishi wa vurugu hiyo ya kisiasa nchini humo, ambayo katika
mazungumzo yake leo ameyataja kama ajali iliyolipata Taifa la Kenya, na ambayo
majirani wake hawaitarajii kutokea katika uchaguzi ujao.
Mwisho
Imetolewa na:
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA
RAIS
DAR ES SALAAM,
21 Oktoba, 2012
Post a Comment