WABUNGE wameigeuzia kibao Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa ndiyo inaongoza kwa vitendo vya rushwa.
Wakizungumza kwa jazba jana jijini Dar es Salaam katika semina ya siku moja iliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa, ikiwa ni harakati ya mapambano ya rushwa, wabunge hao waliwashutumu vikali watendaji wa TAKUKURU na kuwatupia lawama kuwa ni vinara wa rushwa.
Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Assumpter Nshiyu Mshama, alisema kuwa TAKUKURU ndio wala rushwa wakubwa, huku akiwataka wabunge kuamua rushwa iishe kwani inawezekana.
Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msingwa, alisema kuwa rushwa iko kila mahali, lakini kikubwa TAKUKURU watakasike, kwani wao ndio wanaoongoza kwa kukumbatia rushwa.
“TAKUKURU wao ndio vinara wa rushwa. Kwa mfano katika uchaguzi uliopita wakati wa kampeni ukiwapigia simu kuna rushwa sehemu fulani wao ndio wanakuwa wa kwanza kuwapigia watoa rushwa wakimbie eneo husika, baadaye wanajifanya kwenda na kukwambia hakuna wala rushwa, wajitakase wao kwanza,” alisema Msigwa.
Hata hivyo Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy, alizitupia lawama nchi za Magharibi kwa kukumbatia wala rushwa, hasa wanaoficha fedha benki za nje.
“Mataifa yaliyoendelea ndio waficha rushwa, ni wabaya sana, watu wanaweka fedha katika mabenki ya Ulaya nao wana wakumbatia, kesi za TAKUKURU hakuna hata moja serikali imeshinda, ifike wakati mwenye mali kuliko uwezo wake akamatwe,” alisema Keissy.
Pia Keissy alisema kuwa TAKUKURU wanatakiwa watende haki katika suala zima la rushwa, ikiwemo kuacha kuwakumbatia na kuwasafisha wala rushwa.
Katika hatua nyingine, wabunge hao waliijia juu TAKUKURU kwa kutoa chapisho linalomuonesha Mbunge wa Bahi, Omari Badwel, ambaye anatuhumiwa kwa rushwa wakidai kuwa ni kuingilia Mahakama.
Akijibu shutuma hizo, Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Mashitaka TAKUKURU, Donasian Kessy, alisema watalifanyia kazi suala hilo, ikiwamo kuwataka wabunge wasiiogope TAKUKURU pindi wanapokuwa na ushahidi.
Kessy pia alisema kuwa tayari TAKUKURU wameshawakabidhi Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba mapendekezo mapya ya sheria kuhusiana na rushwa.
Akizungumzia utoaji wa picha ya Badwel, Kessy alisema kuwa picha hiyo haijengi mazingira ya kuingilia uhuru wa Mahakama na utendaji kazi wake, bali ni moja ya matukio yaliyotokea katika kipindi cha mwezi Aprili, mwaka huu, hivyo ni kawaida kwa TAKUKURU kuchapisha matukio hayo.
Awali akiwasilisha mada katika semina hiyo, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Andrew Mbwambo, alisema kuwa vyama vya siasa vinatakiwa kujiendesha kwa haki, si rushwa, ikiwamo kuacha uchakachuaji.
Pia alisema kuwa uchaguzi wa ndani wa vyama unatakiwa utungiwe sheria ya kuzuia rushwa, ikiwamo kutochaguana kwa kuheshimiana, bali waangalie uwezo wa mtu.
Prof. Mbwambo pia aliwataka wabunge hao kutambua umuhimu wa wanahabari, hivyo hawapaswi kuwafukuza wala kuwaogopa pindi wanapotimiza wajibu wao.
chanzo: Tanzania Daima
Post a Comment