*******************
Na Mahmoud
Zubeiry
YANGA SC
imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya
jioni ya leo kuichapa Mgambo JKT ya Handeni, Tanga mabao 3-0 kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo,
unaifanya Yanga sasa iwe na pointi sawa na mabingwa watetezi, Simba SC waliotoa
sare ya 1-1 na Polisi mjini Morogoro leo, ingawa inazidiwa bao moja tu katika
wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Hadi
mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na beki Nadir
Haroub ‘Cannavaro’ na mshambuliaji Didier
Kavumbangu.
Cannavaro
alifunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Oscar Joshua dakika ya pili kutoka
wingi ya kulia, wakati Kavumbangu alimalizia pasi ya Hamisi Kiiza dakika ya
39.
Pamoja na
kutoka uwanjani wamelowa kipindi cha kwanza, lakini Mgambo JKT walicheza soka ya
kuvutia na mara mbili walikaribia kufunga kupitia kwa Juma
Mwinyimvua.
Yanga
walicheza vema dakika 45 za kipindi cha kwanza, tofauti sana na mechi za awali
ambazo wamekuwa ‘wakichezewa’ sana na wapinzani.
Ilishuhudiwa
katika kipindi hicho, Yanga wakimiliki zaidi mpira na kupeana pasi za uhakika,
ingawa mashambulizi yao mengi walipitisha pembeni, hasa upande wa
kulia.
Hamisi
Kiiza, Msuva na Kavumbangu walicheza kwa uelewano mkubwa pale mbele na kulitia
misukosuko haswa lango la Mgambo.
Kipindi cha
pili, Yanga walirudi na moto wao tena na kuendelea kuwachachafya
Mgambo.
Hata hivyo,
iliwachukua Yanga dakika 34 kupata bao la tatu, mfungaji akiwa ni Jerry Tegete
aliyeingia dakika ya 68 kuchukua nafasi ya
Kavumbangu.
Tegete
alifunga bao hilo akiunganisha krosi maridadi ya beki wa kushoto, Oscar
Joshua.
Pamoja na
kufungwa, Mgambo waliendelea kusukuma mashambulizi langoni mwa Yanga, ingawa leo
mabeki wa timu hiyo, inayofundishwa na Mholanzi, Ernie Brandts walicheza kwa
uelewano mkubwa na kudhibiti hatari zote langoni mwao.
Mgambo
inayofundishwa na Mohamed Kampira, ilipata pigo dakika ya 85, baada ya beki wake
wa kulia, Salum Mlima kutolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumchezea
rafu mbaya Mbuyu Twite.
Baada ya
mchezo huo, Brandts alisema dakika 10 za mwanzo timu yake ilikuwa inashindwa
kumalizia vizuri mashambulizi yake, lakini baadaye ikatulia na hatimaye kupata
ushindi huo, ambao ameufurahia kwani unamuweka katika nafasi nzuri kwenye
msimamo wa Ligi Kuu.
Kwa upande
wake, Kampira wa Mgambo alisema kufungwa ni sehemu ya mchezo, akawasifu Yanga
kwa kutumia nafasi walizopata, huku akijutia nafasi walizopoteza wachezaji wake
leo.
Kikosi cha
Yanga leo kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Nsajigwa Shadrack/Kevin Yondan dk
46, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athumani Iddi ‘Chuji’,
Simon Msuva, Frank Domayo/Nurdin Bakari dk 76, Didier Kavumbangu/Jerry Tegete
dk68, Hamisi Kiiza na Haruna Niyonzima.
Mgambo JKT;
Godson Mmasa, Salum Mlima, Yassin Awadh, Salum Kipanga/Godfrey Komba dk80,
Bakari Mtama, Ramadhani Malima, Chande Magoja, Mussa Ngunda, Issa Kandulu/Nassor
Gumbo dk 60, Fully Maganga na Juma Mwinyimvua/Omar Matwiko
dk76.
Katika
mchezo wa utangulizi, timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Yanga,
imeifunga Mgambo JKT ya vijana pia 1-0, bao hilo pekee la Clever Charles dakika
ya 65.
Katika mechi
nyingine, Simba ilitoka sare ya 1-1 Polisi kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro,
wenyeji wakitangulia kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa Mokili Rambo kabla ya
Amri Kiemba kusawazisha dakika ya 57.
Post a Comment