Wizara ya Nishati na
Madini imelizuia Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) kupandisha bei ya umeme kama
lilivyokuwa limepanga kufanya hivyo Januari, mwakani.
Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Sospeter
Muhongo, alisema hayo juzi wakati akihojiwa kwenye kipindi cha dakika 45
kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya ITV.
“Kumekuwa na madai kwamba, Tanesco watapandisha
bei ya umeme ifikapo Januari 2013. Lakini nimewaelekeza Tanesco na Ewura
(Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji) wasipandishe bei ya umeme,”
alisema Profesa Muhongo.
Alisema ameielekeza Tanesco isipandishe bei kwa
sababu katika deni la dola za Marekeni milioni 250 inazodaiwa, serikali imekuwa
ikilisaidia kulipa.
Profesa Muhongo alisema hadi sasa serikali
imekwishatoa dola za marekani milioni 50 kupunguza deni hilo, ambalo limebaki
dola za Marekani milioni 200.
Alisema serikali imepunguza bei ya kuunganisha
umeme wananchi ili ifikapo mwaka 2015 asilimia 30 ya Watanzania wawe wanapata
nishati hiyo tofauti na sasa, ambapo wanaopata ni asilimia 18.4 tu.
Profesa Muhongo alisema wizara yake imejipanga
kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme kifikie megawati 2,780 kutoka megawati
1,438 zinazozalishwa hivi sasa ifikapo mwaka 2015.
Alisema uzalishaji huo utaongezeka kutokana na
mkakati uliopo wa kuongeza vyanzo vya uzalishaji umeme na kwamba, hivi sasa
matumizi ya umeme kwa nchi nzima ni megawati 830.
“Mgawo wa umeme haupo na wala hautakuwapo,
wengine wanaufurahia uwapo kwa sababu zao binafsi za kibiashara na kisiasa.
Lakini nawahakikishia wananchi hakutakuwa na mgawo wa umeme,” alisema Profesa
Muhongo.
Akizungumzia suala la gesi, alisema wizara yake
imewasilisha sera ya gesi katika Baraza la Mawaziri na rasimu ya sera hiyo
imepelekwa kwa wakuu wa mikoa ili wananchi waweze kutoa maoni yao kabla ya
kupelekwa bungeni Februari, mwakani.
Profesa Muhongo alisema rasimu ya sera hiyo
imepelekwa katika mikoa, ambayo gesi na mafuta inapatikana na, ambayo inatumia
gesi hiyo kwa wingi ni Lindi, Mtwara, Tanga, Pwani, Rukwa (Sumbawanga), Katavi,
Mbeya na Arusha.
habari na THOBIAS
MWANAKATWE
SOURCE:
NIPASHE
Post a Comment