Said Morad, kweli kahujumu timu? |
Na Mahmoud
Zubeiry
AZAM FC
imewasimamisha wachezaji wake watatu wa safu ya ulinzi, kipa Deo Munishi ‘Dida’
na mabeki Said Mourad na Erasto Nyoni kwa tuhuma za kuihujumu timu hiyo katika
mechi zake za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya vigogo Simba na Yanga
hivi karibuni.
Azam
ilifungwa na Simba mabao 3-1 Oktoba 27, mwaka huu kabla ya kufungwa mabao 2-0 na
Yanga Novemba 4, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi za Ligi
Kuu.
Baada ya
kufungwa na Simba, Azam FC ilimfukuza kocha wake Mserbia, Boris Bunjak na
kumrejesha Muingereza, Stewart Hall.
Habari
kutoka ndani ya Azam zimesema kwamba baada ya kupata taarifa hizo, uongozi
ulizifanyia kazi taratibu na kujiridhisha kabisa wachezaji hao watatu walikula
njama za kuihujumu timu katika mechi hizo.
Kwa sababu
hiyo, uongozi kwanza umewasimamisha wachezaji hao na hatua zaidi zitafuatia
baadaye.
Hata hivyo, Dida hakucheza mechi hata moja kati ya
hizo, kwani Oktoba 27, kikosi cha Azam kilikuwa; Mwadini Ali, Ibrahim Shikanda, Samir Hajji Nuhu, Said
Mourad, Aggrey Morris, Abdulhalim Humud, Jabir Aziz aliyempisha Abdi Kassim,
Himid Mao aliyempisha Kipre Balou, John Bocco ‘Adebayor’ aliyempisha Khamis Mcha
‘Vialli’, Kipre Herman Tcheche na Salum Abubakar.
Siku hiyo,
Azam walitangulia kufunga dakika ya nne, kupitia kwa Adebayor ambaye alimtoka
beki Mkenya Paschal Ochieng na kumchambua Juma Kaseja, kabla ya Felix Mumba
Sunzu Jr., kuisawazishia Simba dakika mbili baadaye, akiunganisha kwa kichwa
krosi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa kutoka wingi ya kulia.
Okwi
aliifungia Simba bao la pili dakika ya 40, baada ya kutokea kizaazaa langoni mwa
Azam kufuatia mpira uliopigwa langoni mwa timu hiyo na Mwinyi Kazimoto na dakika
tano tu tangu kuanza kipindi cha pili, Mganda huyo tena akawainua vitini
mashabiki wa Simba, akifumua shuti la umbali wa mita 19, baada ya kuwatoka
mabeki wa Azam.
Katika mechi
na Yanga, kikosi cha Azam kilikuwa; Mwadini Ally, Erasto Nyoni aliyempisha Samir
Hajji Nuhu, Ibrahim Shikanda, Aggrey Morris na Said Mourad, Jabir Aziz
aliyempisha Ibrahim Mwaipopo, Kipre Balou, Khamis Mcha ‘Vialli’ aliyempisha Abdi
Kassim ‘Babbi’, Salum Abubakar, John Bocco na Kipre Tcheche.
Siku hiyo,
mabao ya Yanga yalitiwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Didier
Kvumbangu aliyeunganisha krosi ya Simon Msuva kutoka wingi ya kulia dakika ya
tisa na Mganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ dakika ya 68, akiunganisha krosi ya
Athumani Iddi ‘Chuji’ kutoka wingi ya kulia.
Habari zaidi
zinasema kwamba, uchunguzi unaendelea kufanywa juu ya wachezaji wengine
wanaotuhumiwa kuwa katika mkumbo huo wa kuihujumu timu na ikithibitika ni
ukweli, watachukuliwa hatua pia bila kujali majina
yao.
Azam tayari
iko Tanga tangu saa 8:00 mchana wa leo kwa ajili yao ya mchezo wao wa mwisho wa
mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara keshokutwa dhidi ya
Mgambo JKT, Uwanja wa Mkwakwani.
Post a Comment