CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitafutia
dawa migogoro inayotokana na baadhi ya makada wake kuonyesha nia ya kuwania
urais na ubunge mwaka 2015, baada ya kuanzisha utaratibu maalumu wa wanachama
wake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gageti hili, mpango huo unakuja wakati Naibu Katibu
Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe ametangaza nia ya kugombea urais katika
uchaguzi mkuu ujao, kitendo ambacho kiliwashtua vigogo wa chama hicho akiwamo
mwasisi wake, Edwin Mtei.
Mara kadhaa Mtei amekuwa akimwonya Zitto kuwa kitendo chake
cha kutangaza nia yake ya kugombea urais kitasababisha mzozo na mpasuko ndani ya
chama hicho.
Mtei
amekuwa akisema kuwa Zitto anatakiwa kuwaunganisha wanaChadema na siyo kuwagawa,
au kuwavuruga na kwamba siyo shida kuonyesha hisia za kuwania urais, lakini
tatizo ni kuwa hali hiyo inatengeneza mzozo mkubwa.
Mtei
ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu (BOT) enzi za utawala
wa Mwalimu Julius Nyerere, alisema wakati mwafaka ukiwadia, Chadema kitaamua ni
nani mwenye sifa za kugombea urais akisema kina utaratibu wake wa kuwapata
wagombea mbalimbali wa uongozi.
Akizungumza wakati akijibu hoja mbalimbali katika mtandao
wa Jamii Forum katikati ya wiki hii, Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, alisema viongozi wa chama hicho walikutana mjini Morogoro hivi
karibuni na kutengeneza utaratibu wa watu kutangaza nia wanapotaka kugombea
nafasi yoyote ya uongozi.
“Nadhani huu ni uamuzi mzuri wa chama maana watu wengine
wana wasiwasi usio na msingi wowote kwamba kuwa na wagombea wengi kwenye chama
ni kuvuruga chama,” alisema Zitto na kuongeza:
“Lakini watu haohao wanashangilia kweli wakiona demokrasia
inavyotekelezwa kwenye nchi nyingine kama Marekani.”
Alisema kuwa tatizo la Watanzania wanapenda kuona
demokrasia inatekelezwa, lakini wao wanaogopa kuitekeleza, hivyo mwongozo kwa
wagombea ambao walipitisha Morogoro utasaidia sana.
“Uamuzi wa Morogoro kuhusu mwongozo kwa wagombea
utatusaidia sana kuondoa mashaka kama haya,” alisema Zitto.
Mwananchi Jumapili lilipomuuliza Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi wa chama hicho, John Mnyika kuhusu jambo hilo alionyesha kutofahamu lolote kuhusu utaratibu
huo, wala ulipofanyika huo mkutano wa Morogoro.
“Mkutano upi wa Morogoro?” alihoji Mnyika. Alipoelezwa kuwa
suala hilo lilizungumzwa na Zitto katika Mtandao wa Jamii Forum alisema:
“Muulize kwanza Zitto akupe ufafanuzi ni kikao gani cha chama, pia juu ya huo
utaratibu, akikueleza ndiyo urudi tena kwangu.”
Juhudi za kumpata Zitto kueleza kwa undani kuhusu utaratibu
huo hazikuzaa matunda, kwani simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila majibu,
baadaye kuzimwa kabisa.
Akizungumzia azma yake ya kuachana na ubunge kama
alivyoahidi mwaka 2005 kuwa, atagombea vipindi viwili pekee Zitto, alisema kuwa
aliwaambia wapigakura wake kwamba nia yake ni kuwa rais wa nchi.
“Nia yangu ni kupisha wengine nao wakimbize kijiti cha
maendeleo ya jimbo letu na mkoa wetu,” alisema Zitto na kufafanua, “ Nimeshasema
mara kwa mara kwamba ukiachana na siasa kazi ninayoipenda zaidi ni
ualimu.”
Alisema kuwa akiachana na ubunge atakwenda kufundisha kwa
kuwa anapenda kufanya tafiti, kusoma, kuandika na kufundisha.
“Hivi sasa tunaandaa mpango wa kuanzisha Chuo Kikuu cha
Ziwa Tanganyika (Lake Tanganyika) mkoani Kigoma, nitafurahi kama nitakuwa mmoja
wa wahadhiri wa mwanzo wa chuo hiki,” alisema Zitto.
Katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Mwenyekiti wa Chama
hicho, Freeman Mbowe alisimama kugombea nafasi ya urais akishindana na Rais
Jakaya Kikwete ambaye alikuwa akisimama kwa mara ya kwanza.
Mwaka 2010, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willbrod Slaa
aligombea nafasi hiyo na kuibuka mshindi wa pili kwa kupata asilimia 26.34 nyuma
ya Rais Kikwete ambaye alipata asilimia 61.17.
Hivi sasa tayari kumetokea maneno ya chinichini miongoni
mwa wabunge waliopo madarakani wakiwatuhumu baadhi ya wanachama wa chama hicho
ambao wameaanza kuingia katika majimbo yao kutaka kugombea viti hivyo katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Wabunge hao wanahoji kama wanachama hao wanaofanya hivyo
wanataka kugombea ubunge katika uchaguzi ujao ili kukifanya chama kiongeze idadi
ya wabunge bungeni, kwa nini wasiende kugombea katika majimbo ambayo hayana wabunge wa chama hicho?
Vilevile, chama hicho kilipata msukosuko katika mchakato wa
kupata wabunge wa Viti Maalumu katika uchaguzi uliopita na kulazimika kuweka
vigezo ambavyo viliondoa manung’uniko hayo.
Baadhi ya vigezo hivyo ni elimu, mchango wa mgombea katika
chama, wanawake waliogombea katika majimbo na uzoefu katika ubunge.
Chanzo:Gazeti la Mwananchi.
Post a Comment