Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), kimesema kauli iliyotolewa na Mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), Tundu Lissu, kuwa anakusudia kumshtaki Rais bungeni ni yake binafsi
na kwamba chama makini hakiwezi kutoa msimamo huo mzito bila kufanya tafakari
makini.
Kauli hiyo inakuja siku
moja baada ya Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, kueleza
kuwa anakusudia kupeleka bungeni hoja maalum ya kumshtaki Rais ikiwa atashindwa
kuchukua hatua dhidi ya ukiukwaji wa Katiba katika uteuzi wa
majaji.
Akizungumza na waandishi wa
habari nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma jana, Makamu Mwenyekiti wa Chadema,
Said Arfi, alisema hakuna kikao chochote cha chama kilichomuidhinishia Lissu
kutoa tamko hilo.
“Chama chochote makini cha
siasa hakiwezi kuchukua maamuzi kama hayo bila kufanya tafakari ya kina
kuhusiana na jambo hilo…kama halitafanikiwa jambo kama hilo litakidhalilisha
chama. Ni vizuri jambo lolote ambalo chama kinakusudia kulifanya liungwe mkono
na wananchi,” alisema.
Arfi ambaye pia ni Mbunge
wa Mpanda Mjini, alisema katika kikao cha chama hicho watakachokaa wakati wowote
kabla ya mwishoni mwa mwaka, watatoa tamko kwamba matamko yote lazima yapate
ridhaa ya chama husika.
Alisema suala hilo
linahitaji kuungwa mkono na wabunge kutoka vyama vingine kwa kuwa idadi ya
wabunge wa Chadema ni 48 tu wakati idadi ya wabunge wanaohitajika kutia sahihi
katika hoja ili ipelekwe bungeni ni 72. Idadi ya wabunge wote
kutoka vyama vya upinzani ni 91.
Kuhusu Lissu kulizungumzia
jambo hilo ambalo lilifanyiwa kazi na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge na bado halijawasilishwa bungeni, Arfi alimtaka Mbunge huyo kufuata sheria
za nchi.
Alisema Sheria ya Haki,
Kinga na Madaraka ya Bunge inataka kutotolewa hadharani kwa jambo lolote
lililojadiliwa faragha na kwamba anayekiuka anakabiliwa na kosa la
jinai.
Hata hivyo, alisema Lissu
kama walivyo wabunge wengine anayo haki ya kuzungumzia jambo lolote ili mradi
havunji kanuni na sheria za nchi.
LISSU
AJIBU
Lissu alipoulizwa kuhusiana
na jambo hilo, alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge, suala la kupeleka hoja
binafsi ni la Mbunge mwenyewe na wala sio chama.
“Kama yeye (Arfi) anaamini
ni vyema tuache majaji wafanye kazi hivyo hivyo bila kuwa na elimu inayostahili
hayo ni yake mimi siwezi kusema kitu,” alisema Lissu.
Juzi Lissu aliwaambia
waandishi wa habari kuwa, hoja hiyo anakusudia kuiwasilisha katika mkutano ujao
wa Bunge wa Februari mwakani iwapo Rais hatafuta uteuzi wa majaji
hao.
“Tunamtaka Rais afute
uteuzi wao haraka iwezekanavyo kama hatafuta uteuzi basi sisi kama Kambi ya
Upinzani tutaanzisha mchakato wa kumshitaki,” alisema na kuongeza: “Tunaenda
kuandaa hoja maalumu na hoja hiyo inatakiwa kusainiwa na asilimia 20 ya wabunge
(wabunge 72 na zaidi).”
Lissu ambaye ni Mnadhimu
Mkuu wa Kambi ya Upinzani, alidai kusudio hilo linatokana na taarifa waliyoipata
kwamba Spika wa Bunge, Anne Makinda, amekataa kutoa taarifa ya uchunguzi wa
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo
(CCM), Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Ngwilizi dhidi ya tuhuma alizozitoa
bungeni kuhusu ukiukwaji wa uteuzi wa majaji.
Lissu alisema Oktoba 30,
mwaka huu wabunge walifanya kikao cha ndani ili kuzungumzia ratiba ya kikao cha
Bunge na Spika alipoulizwa kuhusu taarifa mbili za ripoti za uchunguzi kuhusu
tuhuma za rushwa dhidi ya wajumbe waliokuwa Kamati ya Nishati na Madini na ile
ya kwake, alikataa na kusema ni za kwake na kwamba halazimishwi kuzitoa na yeye
ndiye atakaye jua atazitoa wakati gani.
Katika Mkutano wa Bunge
Julai 13, mwaka huu, Lissu alisema baadhi ya majaji walioteuliwa na Rais hawana
sifa, uwezo na wala hawakufaa kushika madaraka ya Jaji Mahakama Kuu na Mahakama
ya Rufani, kauli ambayo ilimsababisha ashitakiwe kwenye Kamati ya
Ngwilizi.
Lissu aliwataja kwa majina
majaji wanane akisema wanafanya maamuzi yanayowapendelea jamaa zao wa karibu na
wengine hawajui kuandika hukumu.
Juzi Lissu alimtaka Spika
kutoa matokeo au taarifa ya Kamati ya Ngwilizi ili Bunge lifahamu ukweli ni upi
baada ya yeye kutoa ushahidi kwenye Kamati hiyo.
“Kwa maoni yangu, ushahidi
wa nyaraka nilizowapa hawawezi kusema nilichosema ni uongo,” alisema na
kuongeza:“Kama majaji wetu hawana
sifa, hawana maadili si suala la kuachwa na Spika wala waandishi wa habari
kuripoti.”
Alihoji kuwa Jaji ambaye
hana hata shahada ya sheria anakaaje mahakamani kutoa haki.
Alisema baadhi ya majaji
wameongezewa mkataba kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
habari NA SHARON
SAUWA
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment